• HABARI MPYA

    Wednesday, June 03, 2015

    MALINZI ‘AWAPA YA MOYONI’ SERIKALI FAINALI ZA VIJANA AFRIKA 2019

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameiomba Serikali iwashike mkono ili kufanikisha maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
    Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa jezi mpya za timu za taifa mchana wa leo ukumbi wa JB Belmenote, jengo la Golden Jubilee, Dar es Salaam, Malinzi alisema kwamba TFF inahitaji sana msaada wa Serikali kufanikisha hilo. 
    “Tunaomba Serikali itushike mkono katika hili ili tuweze kuandaa mashindano mazuri. Lakini haitakuwa vyema Tanzania kuandaa mashindano mazuri, halafu tusifanye vizuri” amesema.
    Aidha, Malinzi amesema haitakuwa vyema wakawa wenyeji wa fainali hizo za U17 mwaka 2019 na wakatolewa hatua ya makundi- ndiyo maana wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na timu bora.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kulia) akimkabidhi cheti cha heshima Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Leodegar Tenga (katikati). Kushoto ni Mbunge wa JImbo la Mchinga mkoani Lindi, Said Mtanda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo. Tenga pia ni Rais wa zamani wa TFF.
    Gwiji aliyecheza Taifa Stars tangu miaka ya 1960, Mzee Kitwana Manara 'Popat' (katikati) naye alipokea cheti cha heshima 

    Amesema Jumapili Juni 7, mwaka huu TFF itazindua mashindano ya taifa ya vijana umri chini ya miaka 13 mjini mwanza na kwamba wachezaji bora wa mashindano haya ndio wataunda kikosi cha awali cha taifa kwa ajili ya kushiriki fainali za U17 mwaka 2019. 
    “Tunaomba Serikali pamoja na wadau wote tushirikiane katika kukilea kikosi hiki ili mwaka 2019 tuwe na timu nzuri,”amesema.
    Malinzi pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufanikisha nchi kupata uenyeji wa fainali za Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake.
    Amemshukuru pia Waziri wa Habari VIjana Utamaduni na Michezo, Dk Fennela Mukangara kwa ushirikiano wanaowapatia katika hatua hizi na katika shughuli nyingine za kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.
    “Kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza soka la vijana, TFF tumejipanga vilivyo kwa mapambano ya hatua za awali za kucheza fainali za vijana za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2017,”amesma. 
    Mechi za kufuzu fainali za U17 2017 zitaanza katikati ya mwakani na tayari TFF imeunda kikosi cha awali cha vijana chini ya umri wa miaka 15 kujiandaa na michuano hiyo, kikosi kilichotokana na michuano ya Copa Coca Cola ya mwaka jana. 
    Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipatia Tanzania uenyeji wa fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
    Manaodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' kulia na Mbwana Samatta kushoto walikuwepo
    Malinzi akimkabidhi cheti Katibu wa zamani wa TFF, Michael Wambura
    Mwenyekiti wa zamani wa Yanga SC, DK Jabir Idrisa Katundu (wa pili kulia) naye alipewa cheti 

    Katika hafla hiyo, pia TFF ilitoa vyeti vya heshima kwa watu mbalimbali waliochangia maendeleo ya soka ya nchi hii kwa miaka 50 iliyopita. Miongoni mwao, ni Marais wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa zamani wa TFF tangu enzi za FAT, wachezaji wa zamani na wadau wengine, wakiwemo wadhamini.
    Nahodha wa kikosi cha Taifa Stars katika Fainali pekee za Mataifa ya Afrika ambazo Tanzania ilishiriki mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria, Leodegar Chilla Tenga alipokea vyeti viwili kwanza kama mchezaji wa kikosi hicho na nyingine kama Rais wa zamani wa TFF.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI ‘AWAPA YA MOYONI’ SERIKALI FAINALI ZA VIJANA AFRIKA 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top