![]() |
Ally Mayay Tembele |
Na Prince Akbar
KAMATI ya Uchaguzi ya klabu ya Yanga ya Dar es Salaam,
imemuengua mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Ally Mayay Temebele kwa sababu
mbili; kwanza pingamizi alilowekewa na pili kuidharau Kamati hiyo kwa kutofika
kwenye usikilizwaji wa pingamizi lake bila ya taarifa yoyote.
Katibu wa Kamati hiyo, Francis Kaswahili ameambia BIN
ZUBEIRY jioni hii kwamba pingamizi alilowekewa Mayay lilistahili majibu
yake, lakini kwa kuwa hakutokea Kamati imeona mambo mawili, mtoa pingamizi ana
hoja na pili Mayay ameidharau Kamati hiyo kwa kutofika bila taarifa.
Kaswahili alisema pingamizi dhidi ya ‘Meja’ Mayay, Nahodha
wa zamani wa Yanga lilikuwa kuhusu kushindwa kutekeleza majukumu yake awali,
akiwa kiongozi wa klabu hiyo na ndani ya muda mfupi anaomba tena uongozi.
“Wagombea wengine wote wamepitishwa kuendelea na usajili kwa
ajili ya uchaguzi, isipokuwa Ally Mayay pekee,”alisema Kasawahili.
Kuenguliwa kwa Mayay, kunafanya nafasi ya Makamu Mwenyekiti
ibakiwe na watu watatu, ambao ni Ayoub Nyenzi, Yono Kevela na Clement Sanga,
wakati wagombea Uenyekiti ni Yussuf Mehboob Manj, John Jambele, Edgar Chibura
na Sarah Ramadhani.
Katika nafasi za Ujumbe ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Mzimba
‘Kampira’, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Said, Edgar Fongo, Beda Simba, Ahmad Gao,
Mussa Katabaro, George Manyama, Aaron Nyanda, Abdallah Bin Kleb, Omary Ndula,
Shaaban Katwila, Jumanne Mohamed Mwammenywa, Abdallah Mbaraka, Peter Haule,
Justin Baruti na Abdallah Sharia.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu,
Mfanyabiashara Muzamil Katunzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eliakhim
Masu walichukua fomu za kugombea Ujumbe lakini wakashindwa kurudisha, wakati
Isaac Chanzi pia hakurudisha fomu ya Makamu Mwenyekiti hivyo moja kwa moja hao
hawamo katika kinyang’anyiro.
Uchaguzi huo, unaokuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya
Utendaji katika uongozi uliokuwa madarakani, akiwemo Mwenyekiti Wakili Lloyd Baharagu
Nchunga na Makamu wake, Davis David Mosha kujiuzulu utafanyika Julai 15, mwaka
huu Dar es Salaam.
Mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo,
walipokea pingamizi dhidi ya wagombea Uenyekiti, Manji na Sarah Ramadhani,
Makamu Mwenyekiti, Yono Kevella, Clement Sanga na Ally Mayay.
Lakini Jaji Mkwawa amesema Kamati yake inaweza kusikiliza na
kuamua kuhusu mapingamizi hayo bila ya kuwepo waliowekewa au walioweka, ila tu
amesistiza ni vema wakawepo ili watetee hoja zao.
Aidha, kuhusu tamko la mwanachama Abeid Abeid ‘Falcon’
kutaka ufafanuzi wa Katiba ipi itatumika katika uchaguzi huo, Jaji Mkwawa
alisema itatumika Katiba ya mwaka 2010 iliyowasilishwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) Juni 17, mwaka huo.
Amemtoa wasiwasi Abeid kwamba katiba ya 2011 iliyokuwa na
matatizo kiasi cha kupingwa mahakamani na wanachama wa klabu hiyo haitatumika.
Lakini pia, Mkwawa amesema pamoja na kwamba uchaguzi huu
unakuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji, wakiwemo Mwenyekiti na
Makamu wake kujiuzulu, Wajumbe waliojiuzulu kutoka kwenye uongozi huo
wanaruhusiwa kugombea.
Aidha, kuhusu wagombea kusaidia klabu katika masuala
yanayohusu fedha katika kipindi hiki kigumu, Jaji Mkwawa amesema hayana
matatizo yakifanyika katika taratibu zinazoeleweka.
Baada ya kusikiliza pingamizi kesho, Jaji Mkwawa amesema
usaili utafanyika Juni 22 na Uchaguzi wa Yanga utafanyika Julai 15 kama
ilivyopangwa, siku moja baada ya kuanza kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo, Yanga ni bingwa wake mtetezi.
0 comments:
Post a Comment