TZ One, Juma Kaseja |
Na Mahmoud Zubeiry
REJEA bao alilofungwa kwenye mechi na Ruvu Shooting. Achana nalo,
kumbuka bao alilofungwa kwenye mechi na Prisons. Unaona nini?
Si Kaseja yule ambaye wengi tunamjua, hodari zaidi na mwenye
hesabu kali katika mipira inayotokana na mashambulizi ya watu wanaokuja moja
kwa moja wakitazamana naye.
Alikuwa mzito wa kuamua na hakujishughulisha kabisa kwenye
mabao yote. Alikuwa tayari kufungwa. Baada ya kumuanzia mpira Nyosso kwenye
eneo la hatari na beki huyo kuchelewa kuucheza hadi akapokonywa na Seif Rashid,
Kaseja hakujisumbua kwenda kumsaidia beki wake, alirudi golini kusubiri kufungwa
na akafungwa.
Nasema alirudi kusubiri kufungwa, kwa sababu zile zinaitwa
nafasi ambazo zinaamua uhodari wa kipa na uzembe wa mtu aliyepata nafasi. Kama Seif
Rashid angepiga nje, angelaumiwa na kama Kaseja angeokoa angesifiwa.
Rejea bao la Prisons, mfungaji alipiga shuti la kawaida sana
na sidhani kama hata yeye mwenyewe alikuwa ana matumaini ya kufunga- maana kwenye
soka kuna neno moja linaitwa kujaribu, nadhani alikuwa anajaribu. Akafanikiwa.
Kweli mpira ulimgonga Shomary Kapombe, lakini haukuwa wenye
madhara bado- kama Kaseja angekuwa makini zaidi, bado tu angeucheza ule mpira. Mabao
haya mawili pekee hayatoshi kusema Kaseja hayuko vizuri kwa sasa, rejea mabao
aliyofungwa na Azam kuanzia Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame hadi Ngao, bado utaendelea kukataa kwamba Juma hayuko vizuri sana kwa
sasa?
Na unaweza kuona presha ya kubadilisha mabeki Simba kwa sasa,
inatokana na hali ya kipa wao Kaseja- amekuwa si yule Juma ‘Mahakama ya Rufaa’
ya kufungwa bao na amekuwa kipa wa kawaida.
Berko, Yanga One |
Hata hivyo, bado kuelekea mpambano wa watani wa jadi
Jumatano, Kaseja anabebwa na uzoefu wake, akiwa mchezaji aliyecheza mechi
nyingi zaidi za Simba na Yanga na kwa muda mrefu kwa wachezaji wa sasa wa timu
hizo, tangu mwaka 2003.
Kwa misimu miwili iliyopita, Yanga walikuwa wanamlalamikia
Yaw Berko anawaringia kwa sababu hawakuwa na kipa mwingine wa kushindana naye. Msimu
uliopita alisajiliwa Shaaban Kado akiwa vizuri sana, lakini naye mwisho wa siku
akashindwa kuufikia ubora wa Berko.
Yanga waliendelea kuumiza kichwa juu ya kipa huyo na msimu
huu wamemsajili Ally Mustafa ‘Barthez’ kutoka Simba. Ni kama kuna hali fulani ya
kulazimisha Barthez adake hata kama hafikii ubora wa Berko, ili kupunguza kile
wanachoamini maringo ya Mghana huyo.
Na kweli, Barthez anadaka, lakini hadi mechi ya jana dhidi ya
African Lyon bado vigumu kumshawishi mtu kwamba kipa huyo anaweza akaanzishwa kwenye
mechi ngumu kama ya Simba, Berko akiwa mzima.
Na kama umeweza kufuatilia, katika siku za karibuni, tangu
baada ya Kombe la Kagame, Berko amekuwa hodari zaidi anapopewa nafasi langoni,
akiamini upinzani wa kweli umekuja hivi sasa.
Kwa nini? Katika Kombe la Kagame, Berko hakumaliza Robo Fainali
dhidi ya Mafunzo aliumia na kutoka, Barthez akaenda kumalizia hadi kwenye penalti
Yanga ikashinda. Berko hakurudi tena langoni hadi Yanga inatwaa ubingwa- hilo hakika
kama alikuwa ana maringo kweli, basi lilimtia adabu.
Ila, pamoja na yote. Panga, pangua vikosi vyote hawa ndio
makipa wanaostahili kupewa dhamana Jumatano.
0 comments:
Post a Comment