• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2012

    DIDIER KAVUMBANGU MTAMBO MPYA WA MABAO JANGWANI ULIOFUNIKA MASTRAIKA WOTE LIGI KUU MZUNGUKO WA KWANZA

    Didier Kavumbangu akishangilia moja ya mabao aliyoifungia Yanga katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu

    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKATI mwingine ipo haja ya kukubali ushauri wa kitaalamu, kuwaachia walimu wafanya usajili. Bila shaka katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka huu Dar es Salaam, Didier Kvumbangu pamoja na kuwafunga Yanga akiwa Atletico ya Burundi jina lake halikuvuma sana kwa sababu hata timu yake haikufanya vizuri sana.  
    Kavumbangu aliwafunga Yanga mabao mawili, wakilala 2-0 katika mchezo wa kwanza wa makundi wa Kagame na zaidi ya hapo, Yanga haikufungwa tena hadi inachukua ubingwa.
    Lakini mabao ya Didier hayakuchukuliwa kama yalitokana na umahiri wa ufungaji, hapana- bali yalichukuliwa kama ya bahati na pia kuikuta timu hiyo ikiwa haiko sawa kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wapya.
    Hata hivyo, mwisho wa msimu Yanga ilipoona inahitaji kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, viongozi waliomba kocha wa timu yao wakati huo, Tom Saintfiet awapendekezee jina la mchezaji kutokana na michuano hiyo ya Kagame.
    Mtakatifu Tom aliwashangaza sana viongozi wa Yanga kwa kuwatajia mchezaji aliyewafunga mabao mawili katika mechi ya kwanza, wakati kuna wachezaji wengine wanang’ara kutoka klabu za AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), APR ya Rwanda na nyinginezo.
    Uzuri tu viongozi wa Yanga walikubaliana na ombi la kocha huyo Mbelgiji na wakamleta mshambuliaji huyo Dar es Salaam. Awali, kidogo ulitaka kuanza kujitokeza wasiwasi juu ya mchezaji huyo kutokana na kuchelewa kuanza kufunga mabao, hadi minong’ono ikaanza labda jamaa galasa.
    Lakini leo unaposoma makala haya, Didier amekwishaifungia Yanga mabao 10 katika mechi 17 alizocheza, zikiwemo za kirafiki tatu za kirafiki.
    Amefunga mabao nane kwenye Ligi Kuu, akiwa anamaliza mzunguko wa kwanza huku anaongoza na amemudu kujihakikishia namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Yanga, mbele ya washambuliaji wengine mahiri kama Said Bahanuzi na Jerry Tegete.
    Didier amewafunika washambuliaji wa kigeni wa timu nyingine pia, akiwemo Felix Mumba Sunzu Jr. kutoka Zambia, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji ghali zaidi Tanzania akiwa analipwa Sh. Milioni 5 kwa mwezi.
    Akiwa katika mwaka wa kwanza wa mkataba wake wa miaka miwili, dhahiri Kavumbangu sasa amewafanya viongozi wa Yanga wamtazame kwa jicho la tatu, kwani hiyo tayari ni lulu kwao. Kuna habari pia, ofa zimeanza kumiminika Jangwani, zikiwemo za klabu za Ulaya kwa ajili ya mchezaji huyo.
    Pamoja na hayo, Kavumbangu, mshambuliaji mrefu, mwenye uwezo wa kumiliki mpira, kasi, nguvu, mbinu na maarifa, bado anahitaji muda kidogo japo kumalizia mzunguko wa pili Tanzania, ili kututhibitishia zaidi uwezo wake. Ila kwa sasa hakuna shaka kabisa kusema, amewafunika washambuliaji wote wa kigeni Tanzania akiwemo Sunzu, mchezaji ghali Tanzania.
    Add caption



    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: DIDIER KAVUMBANGU MTAMBO MPYA WA MABAO JANGWANI ULIOFUNIKA MASTRAIKA WOTE LIGI KUU MZUNGUKO WA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top