• HABARI MPYA

    Thursday, November 15, 2012

    HATIMA YA MILOVAN SIMBA LEO, KIKAO KIZITO MNO CHAFANYIKA

    Kocha wa Simba SC, Milovan Cirkovick kushoto akiwa ameishiwa nguvu baada ya kufungwa na Toto Africans mwishoni mwa wiki katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kulia ni wachezaji wake, Shomary Kapombe na Jonas Mkude.

    Na mahmoud Zubeiry
    KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Simba ya Dar es Salaam inatarajiwa kuwa na kikao kizito leo, kujadili mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa klabu hiyo na mwenendo wa timu yao ya soka kwa ujumla.
    Habari kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba kikao hicho kitashirikisha Wajumbe wote wa Kamati hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage.
    Miongoni mwa ajenda zinazotarajiwa kuwa mjadala mzito na matokeo ya timu hiyo kushika nafasi ya tatu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, licha ya kuanza vema na kufikia kuongoza kwa wastani wa pointi saba zaidi.
    Aidha, katika kikao hicho, habari zinasema Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ atawasilisha rasmi barua ya kujiuzulu kwake uongozi, kufuatia kuibuka watu wanaompinga na kushinikiza ajiuzulu.
    Lakini pia bado mjadala mpana utakuwa kuhusu mustakabali wa timu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Litajadiliwa suala la kipa Juma Kaseja kuomba kung’atuka baada ya kufanyiwa fujo na mashabiki.
    Litajadiliwa suala la kusimamishwa kwa beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’. Litajadiliwa suala la kuboreshwa kwa timu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa mwakani.
    Lakini pia habari zinasema litajadiliwa pendekezo la kutaka kocha wa timu hiyo, Mserbia Profesa Milovan Cirkovick aondolewe na masuala mengine ya msingi, kama salio la malipo ya kiwanja, ambacho klabu hiyo inataka kujenga uwanja wake wa michezo. 
    Kwa ujumla, hamkani si shwari ndani ya Simba hivi sasa, baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya tatu, tena wakizidiwa pointi sita na wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HATIMA YA MILOVAN SIMBA LEO, KIKAO KIZITO MNO CHAFANYIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top