• HABARI MPYA

    Thursday, November 15, 2012

    MGOSI ACHUKUA NAFASI YA BAHANUZI CHINA

    Mussa Mgosi

    Na Mahmoud Zubeiry
    MUSSA Hassan Mgosi ameondoka jana kwenda China kucheza soka ya kulipwa, akichukua nafasi ya Said Bahanuzi, ambaye klabu yake, Yanga imemzuia.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mgosi ambaye amesajiliwa JKT Ruvu ya Pwani msimu huu, akitokea DC Motemba Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ameondoka na wachezaji wengine wawili wa ‘mchangani.
    “Baada ya Yanga kuwazuia Cannavaro (Nadir Haroub) na Bahanuzi, nafasi zao wamechukua Mgosi na vijana wengine wawili, mmoja kipa na mwingine beki, kutoka mchangani tu, lakini wanajua sana,”kilisema chanzo cha habari.
    Mgosi hakucheza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kutokana na kukosa hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka DRC.
    Cannavaro na Bahanuzi waliotarajiwa kuondoka juzi saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways kwenda China, kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa, walizuiwa na klabua yao.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba, sababu za kuzuiwa kwa wachezaji hao ni kutokana na klabu inayowataka kutofuata taratibu.
    “Hawajatuma barua, hawa wanataka kwenda kienyeji tu, na sisi si kama tumewazuia, tumeitaka kwanza hiyo klabu ifuate taratibu kwa kutuma barua huku na kujitambulisha, ili hata hao wachezaji wakipata matatizo tujue tunaanzia wapi,”alisema Bin aKleb.
    Mapema wiki hii, Cannavaro, Nahodha Msaidizi wa Yanga aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba wanakwenda China kwa wiki mbili na baada ya majaribio kama wakifuzu, klabu inayowataka itafanya mazungumzo na klabu yao.
    “Sisi wote tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu jamaa itabidi watuhamishe Yanga,”alisema  beki huyo kati aliyezaliwa Februari 10, mwaka 1982.
    Cannavaro yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Malindi ya Zanzibar wakati Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Mwaka 2009, Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi leo anakwenda kujaribu bahati yake China.
    Bahanuzi ameingia na zali la aina yake Yanga SC, kwani katika mashindano ya kwanza kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame.
    Hadi sasa, Said Bahanuzi   maarufu kama Spider Man, ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatau ya penalti tangu ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
    Kwa sasa China ni nchi ambayo mastaa wengi waliokuwa Ulaya wanakwenda kumalizia soka yao, mfano washambuliaji wawili wa zamani wa Cheslea, Didier Drogba na Nicolas Anelka waliopo Shenghua Shanghai. Anelka ni kocha mchezaji.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MGOSI ACHUKUA NAFASI YA BAHANUZI CHINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top