• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2012

    YANGA SC KUTOKA KUZIDIWA POINTI SABA HADI KUONGOZA LIGI KUU KWA POINTI SITA ZAIDI MZUNGUKO WA KWANZA

    Yanga wamemaliza kileleni

    Na Mahmoud Zubeiry
    MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, rasmi umemalizika jana ukiacha mechi mbili za viporo za Tanzania Prisons, dhidi ya Mgambo JKT na Ruvu Shooting.
    Prisons walipata ajali wakiwa njiani kuelekea Tanga kwa ajili ya mechi yao na Mgambo JKT, hivyo mechi hiyo na ile iliyofuata dhidi ya Ruvu Shooting zikaahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine, ili kuwapa wachezaji wake nafasi ya kupona majeruhi.
    Mzunguko wa kwanza umemalizika na matokeo yamekuwa tofauti na mwelekeo wa ligi hiyo katika mzunguko huo, hadi katikati yake.
    Yanga SC, ambayo haikutarajiwa kushika hata nafasi ya pili, ndiyo imemaliza kileleni kwa pointi zake 29, baada ya mechi hizo 13, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 24 na Simba SC yenye pointi 23.
    Presha ilikuwa upande wa mashabiki wa Yanga ndani ya mechi tano za mzunguko wa kwanza, kutokana na kuanza vibaya, kiasi cha kufikia kumfukuza kocha wake aliyewapa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Mbelgiji, Tom Saintfiet.
    Saintfiet alifukuzwa baada ya mechi mbili za Ligi Kuu, akitoa sare na Prisons mjini Mbeya na kufungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
    Azam nayo ilianza vema ikiwa nyuma ya Simba SC, lakini ilifukuza kocha wake Mserbia Boris Bunjak baada ya kufungwa mabao 3-1 na Wekundu hao wa Msimbazi.
    Naam, Tanzania mechi moja au mbili za kufungwa zinatosha kumfukuzisha kocha na watu sasa wanasubiri hatua itakayochukuliwa na Simba dhidi ya kocha wake, Mserbia pia, Profesa Milovan Cirkovick baada ya klabu hiyo kufungwa mechi mbili mfululizo, 2-0 na Mtibwa Sugar  na 1-0 na Toto.
    Tayari kundi la Friends Of Simba ambalo linasaidia sana uendeshwaji wa klabu hiyo limeripotiwa kushinikiza Milovan afukuzwe na Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amesema Ijumaa wiki hii atachukua maamuzi magumu. Tusubiri.
    Lakini tumeshuhudia timu mpya iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, ambayo imeleta changamoto mpya, JKT Mgambo pamoja na kuimarika kwa Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, ambazo zinatoa upinzani katika ligi hiyo hata kwa vigogo.
    Kwa kiasi kikubwa msimu huu tuna ligi tofauti na ya msimu uliopita na kama timu zitafanya maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili, ni matarajio ya wengi Ligi Kuu itaisha vizuri zaidi.      

    Yanga SC 2012
    YANGA SC:
    Wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni mwa Ligi Kuu, wakiwa na pionti zao 26, baada ya kucheza mechi 13, kufungwa mbili dhidi ya Mtibwa Sugar 3-0 na Kagera Sugar 1-0, zote ugenini, kutoa sare mbili 1-1 dhidi ya Simba SC na 0-0 dhidi ya Prisons.
    Yanga ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya tatu Ligi Kuu, ilipanda kileleni Novemba 4, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0 na kuwashusha mabingwa watetezi, walioongoza ligi hiyo tangu mwanzoni.
    Katikati ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilifikia kuzidiwa pointi saba na Simba lakini Oktoba 31, ikafanikiwa kuwafikia Wekundu hao wa Msimbazi, siku hiyo wao wakiifunga Mgambo JKT 3-0 Dar es Salaam na wapinzani wao wakilazimishwa sare ya bila kufungana na Polisi Morogoro.    
                               P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    1      Yanga SC   13     9      2     2       25   10     15   29
    KOCHA; Ernie Brandts (Uholanzi)

    Azam FC 2012
    AZAM FC:
    Imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili, kwa pointi zake 24, ikiwazidi pointi moja tu mabingwa watetezi, Simba SC. Azam walikuwa na mwelekeo wa kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kama si kufungwa mechi mbili mfululizo za mzunguko wa kwanza, dhidi ya Yanga 2-0 na Mgambo JKT 2-1.
    Azam ilianza vema tu ligi hiyo, ikiwa nyuma ya Simba tangu mwanzo hadi Oktoba 31, ilipoenguliwa na Yanga katika nafasi ya pili. Ikielekea kwenye mechi yake ya mwisho dhidi ya Mgambo, Azam ilifukuza wachezaji wake wanne, Deo Munishi ‘Dida’, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris kwa madai walipokea hongo waifungishe timu hiyo dhidi ya Simba na wanadai wana ushahidi hadi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Dhahiri kuondolewa kwa wachezaji hao tegemeo kikosini kulichangia matokeo ya kufungwa na Mgambo katika mechi ya mwisho.                     
                               P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    2      Azam FC     13     7     3      3      17     11    6     24
    KOCHA: Stewart Hall (Uingereza)

    Simba SC 2012
    SIMBA SC:
    Mabingwa hao watetezi, waliianza Ligi Kuu vema wakionyesha dalili zote za kutetea ubingwa wao kwa kufanikiwa kuwa kileleni hadi mwishoni mwa mzunguko huo, kabla ya mambo kugeuka ghafla.
    Zilianza sare kwanza, 1-1 na Yanga, 0-0 na Coastal Union, 2-2 na Kagera Sugar na baadaye 0-0 na Mgambo, 0-0 na Polisi Morogoro kabla ya kufungwa mechi ya kwanza msimu huu, mbele ya Mtibwa Sugar na kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha 1-0 kutoka kwa Toto Africans.
    Matokeo haya kwa kiasi kikubwa yameivuruga Simba SC na inasemekana Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ anafikiria kujiuzulu na baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar, hakujihusisha na chochote juu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Toto, wakati huo Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage yuko bize na shughuli za kisiasa Dodoma. Rage anasema amekwishawajua wanaosababisha matokeo mabaya Simba na Ijumaa atatangaza maamuzi magumu. 
                                    P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    3      Simba SC         13     6     5      2      20   11      9     23
    KOCHA: Milovan Cirkovick (Serbia)

    Mtibwa Sugar 2012
    MTIBWA SUGAR:
    Ilianza vizuri, katikati ikavurunda na mwishoni mwa mzunguko wa kwanza ikazinduka tena hatimaye imemaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
    Inaonekana Mtibwa Sugar inaanza kurejesha makali yake iliyoingia nayo katika soka ya Tanzania miaka ya 1990 hadi wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo mara mbili mfululizo 1999 na 2000, wakiweka rekodi ya kuwa timu pekee nje ya Simba na Yanga kutetea taji hilo.
    Hiyo si kwa sababu tu ipo nyuma ya Yanga, Azam na Simba, bali msimu huu imefanikiwa kuvifunga vigogo vyote vya soka nchini, Simba na Yanga. 
                                    P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    4      Mtibwa Sugar   13     6     4      3      18    12     6     22
    KOCHA: Mecky Mexime (Mzalendo)

    Coastal Union 2012
    COASTAL UNION:
    Wana Mangushi wamerudi tena kwenye makali yao yaliyowafanya wakawa mabingwa wa ligi hiyo mwaka 1988, kwani hadi sasa wameonyesha upinzani wa kutosha kwenye Ligi Kuu. Wagosi hao wa Kaya wamemaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zao 22 sawa na Mtibwa walio nafasi ya nne, lakini wanazidiwa wastani tu wa mabao ya kufunga na kufungwa.
    Hata hivyo, Coastal walianza Ligi Kuu kwa kusuasua kiasi cha kufikia kuwafukuza makocha wake wa awali waliosajili na kuandaa timu kwa ajili ya ligi hiyo, Juma Mgunda na Habib Kondo ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hemed Morcco na Ally Kiddy.
                                    P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    5      Coastal Union  13     6      4     3       16   14      2     22
    KOCHA: Hemed Morocco (Zanzibar)

    Kagera Sugar 2012
    KAGERA SUGAR:
    Kagera Sugar wamemaliza katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 21 na wangeweza kumaliza juu ya hapo, kama wangeutumia vizuri mchezo wao wa mwisho kwenye Uwanja wa nyumbani dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
    Wakipewa nafasi kubwa ya kushinda, katika mastaajabu ya wengi, Kagera wakalazimishwa sare ya bila kufungana na Maafande hao wa Morogoro kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, hivyo kuwapa nafasi Coastal na Mtibwa kuendelea kuwa juu yao.
    Kagera inajivunia kutofungwa na vigogo wa soka nchini, kwani waliifunga Yanga 1-0 na wakatoa sare ya 2-2 na Simba na Dar es Salaam.  
                                     P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    6      Kagera Sugar   13      5     6      2      15   10      5      21
    KOCHA: Abdallah Athumani Seif ‘Kibadeni’ (Mzalendo)

    Ruvu Shooting 2012
    RUVU SHOOTING:
    Katika timu zote za majeshi kwenye ligi hiyo, Ruvu Shooting ndio inaonekana kuwa imara zaidi na ndiyo maana ipo katika nafasi nzuri zaidi, ikiwa imebakiza mechi moja ya kiporo dhidi ya Prisons kumaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza.
    Ruvu ipo katikati ya msimamo wa ligi, nafasi ya saba kwa pointi zake 17 na inaweza kumaliza na pointi 20 iwapo itaifunga Prisons, lakini itaendelea kubaki kwenye nafasi hiyo hiyo, kwani Kagera Sugar waliopo juu ya wana pointi 21.
    Timu hii inayotumia Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani ni moja kati ya timu zilizoonyesha kandanda safi ya kuvutia, tena ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, kama Seif Abdallah anayegombea kiatu cha dhahabu.  
                                     P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    7      Ruvu Shooting  12     5      2     5      17     17     0    17
    KOCHA: Charles Boniface Mkwasa (Mzalendo)

    JKT Ruvu 2012
    JKT RUVU:
    Imeshuhudiwa katika msimu mwingine, timu hii inazidi kupoteza makali yake, baada ya kumaliza katika nafasi ya nane mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
    Siyo JKT ile ambayo ilikuwa tishio kwa vigogo, Simba na Yanga bali hii ya sasa ni ‘urojo’ na hali hii inatokea huku ikiwa inaundwa karibu na asilimia kubwa ya wachezaji wake wale wale, walioifanya iwe tishio misimu michache iliyopita, tena wakiwa chini ya kocha yule yule, kiungo wa zamani wa Yanga, Charles Killinda.
                                P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    8      JKT Ruvu     13     4     3      6      13     20    -7    15
    KOCHA: Charles Kilinda (Mzalendo)

    TZ Prisons 2012
    TZ PRISONS:
    Imerejea Ligi Kuu msimu huu na hadi sasa unaweza kusema inapambana kuhakikisha inabaki kwenye ligi hiyo msimu ujao. Prisons wana mechi mbili za viporo dhidi ya Mgambo JKT na Ruvu Shooting ambazo zote watacheza ugenini, lakini hadi sasa inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo.
    Timu hiyo iliahirishiwa mechi zake  baada ya kupata ajali, ikiwa inaelekea Tanga kumenyana na Mgambo na wachezaji wake sita wakaumia. Inaweza kupanda juu kiidogo iwapo itashinda mechi zake mbili zilizobaki.  
                            P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    9      Prisons     11     3     5      3      8      9      -1    14
    KOCHA: Jumanne Charles (Mzalendo)

    JKT Oljoro 2012
    JKT OLJORO:
    Haina makali yake iliyoingia nayo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita yaliyowafanya wamalize mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni. Msimu huu JKT Oljoro imemaliza katika nafasi ya 10 kwa pointi zake 24 na huwezi kusita kusema ipo kwenye hatari ya kushuka daraja hadi sasa.
    Ina pointi 14, sawa na Toto Africans iliyo nafasi ya 11 na inabebwa juu kwa wastani wa bao moja tu katika mabao ya kufunga na kufungwa, huku ikiwa inaizidi kwa pointi mbili tu Africans Lyon iliyo nafasi ya 12- JKT Oljoro hakika imemaliza mzunguko wa kwanza katika eneo baya. 
                               P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    10   JKT Oljoro   13      3     5      5      13    16     -3    14
    KOCHA: Mbwana Makatta (Mzalendo)

    Mgambo JKT 2012
    MGAMBO JKT:
    Ligi Kuu ya Bara imepokea timu mpya tushio ambayo imeongeza ladha katika ligi hiyo. Hiyo si nyingine zaidi ya JKT Mgambo ua Handeni, Tanga inayotumia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga pamoja na Coastal Union. Ikiwa na mechi moja ya kiporo mkononi dhidi ya Prisons, Mgambo ipo nafasi ya 11 kwa pointi zake 14 na kama ikifanikiwa kushinda mchezo huo, inaweza kupanda hadi nafasi ya saba, itategemea pia na matokeo ya mchezo mwingine wa kiporo kati ya Ruvu Shooting na Prisons. Mgambo walianza kwa kusuasua na watu wakaitabiria itashuka daraja, ila ilipokuja kuzinduka mwishoni mwa msimu, watu wamebadilisha kauli zao. 
                                  P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    11   Mgambo JKT   12     4     2      6      9      13     -4    14
    KOCHA: Mohamed Kampira (Mzalendo)

    Toto Africans 2012
    TOTO AFRICANS:
    Wana Kishamapanda bado wapo katika wakati mgumu, kwani wamemaliza Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya 12, ambayo ni ndani ya nafasi tatu za kushuka Daraja.
    Washukuru sana ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wao wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, kwani umewainua kidogo, vinginevyo wangemaliza ligi hiyo vibaya zaidi.
    Lakini hii ni timu ambayo inacheza kwa ushindani zaidi inapokutana na timu tishio, ila kwa timu ambao zinaonekana si tishio, Toto hufanya vibaya. Bila shaka kuna kudharau mechi, ambako ndiko kunawaponza na kama watabadilika mzunguko wa pili, wanaweza kmufanya vizuri na kubaki Ligi Kuu. 
                                     P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    12   Toto Africans      13     2     6      5      10     15    -5    12
    KOCHA: John Tegete (Mzalendo)

    African Lyon 2012
    AFRICAN LYON:
    Hali bado ni tete African Lyon, ikiwa imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu katika nafasi ya 13 kwa pointi zalke tisa. Licha ya kunolewa na kocha Muargentina, Pablo Ignacio Velez, lakini Lyon wamekuwa vibonde tu hadi sasa.
    Mmiliki wa timu hiyo, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ amesema kwamba ametenga dau la dola za Kimarekani 200,000 kwa ajili ya kufanya usajili dirisha dogo ili kuimarisha kikosi na miongoni mwa wachezaji aliowalenga ni Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa wa Simba na Mbuyu Twite wa Yanga. Amesema kwa Twite atatoa dola 100,000, Ngassa dola 40,000 na Okwi dola 60,000. Tusubiri, ila hadi sasa hali tete Lyon.
                                 P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    13   African Lyon   13     2     3      8       9      20    -11  9
    KOCHA: Pablo Ignacio Velez (Argentina)

    Polisi Morogoro 2012
    POLISI MOROGORO:
    Imerejea Ligi Kuu msimu huu, lakini haitakuwa ajabu mwishoni mwa msimu ikarudi tena kucheza Ligi Daraja la kwanza. Timu ya Morogoro, imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inashika mkia. Polisi haijashinda mechi hata moja zaidi ya kutoa sare nne na kufungwa mechi nyingine tisa.
    Sijui maajabu gani yatokee, msimu ujao tuendelee kuwa na timu ya Morogoro, kwani kulingana na ushindani wa Ligi Kuu msimu huu, hakuna dalili za Polisi kupona.
                                     P      W    D     L      GF   GA   GD  Pts
    14   Polisi Morogoro   13     0     4      9      4      16    -12   4
    KOCHA: John Simkoko (Mzalendo)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC KUTOKA KUZIDIWA POINTI SABA HADI KUONGOZA LIGI KUU KWA POINTI SITA ZAIDI MZUNGUKO WA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top