• HABARI MPYA

    Thursday, November 15, 2012

    YONDAN: HAIKUWA KAZI NYEPESI KUMDHIBITI OLIECH

    Kevin Yondan

    Na Prince Akbar
    BEKI wa Yanga, Kevin Yondan amesema kwamba licha ua kuwafunga Kenya, Harambee Stars, lakini wapinzani wao hao ni wazuri na zaidi akamsifia mshambuliaji wa klabu ya Daraja la Pili Ufaransa, AJ Auxerre, Dennies Oliech kwamba ni mtu hatari.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Mwanza jana, Yondan alisema kwamba walifanya kazi kubwa mno kumdhibiti Oliech, kwani mtu huyo ni hatari.
    “Yule jamaa anajua, mimi binafsi ilinibidi nitulize sana akili katika kukabiliana naye, ndiyo maana hakufunga, bila hivyo Yule mtu angefunga,”alisema Yondan.
    Hata hivyo, beki huyo wa kati alisema timu yao ilicheza vizuri kwa ujumla jana na anaamini hizi ni dalili nzuri za kuwapa Watanzania.
    “Tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu, lakini tunaendelea kuomba mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti ili tufanye vizuri zaidi,”alisema.
    Taifa Stars, jana iliibwaga Kenya, Harambee Stars bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza katika mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Hadi mapumziko, Stars ilikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na beki Aggrey Morris katika dakika ya nne, baada ya kupanda kusaidia mashambulizi.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa anayetambuliwa na FIFA, Oden Mbaga, Kenya walitawala dakika 10 za mwanzo, lakini baada ya hapo Stars wakafunguka nao na kuanza kula nao sahani moja na Harambee Stars.
    Kipindi cha pili, Kenya walianza na mabadiliko kocha Henri Michel akiwapumzisha James Situma, Jerry Santo na Wesley Kemboi na kuwaingiza Christopher Wekesa, Anthony Akumu na Timbe Ayoub.
    Pamoja na mabadiliko hayo, mambo yaliendelea kuwa magumu kwa Harambee Stars, kwani wenyeji waliendelea kucheza kwa makini, wakishambulia na kujilinda zaidi.
    Kocha wa Stars naye, Mdemnark, Kim Poulsen aliwatoa Amir Maftah, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Mbwana Samatta, Mrisho Ngassa na Thomas Ulimwengu na kuwaingiza Nassor Masoud ‘Chollo’, Amri Kiemba, Simon Msuva, John Bocco ‘Adebayor’, Shaaban Nditi  na Issa Rashid.  
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Harambee, Mfaransa Michel alionyesha kukerwa na matokeo hayo na kusema timu yake haikucheza vizuri, wakati Polusen, amefurahia ushindi huo akisema timu yake haijacheza kwa miezi miwili na baada ya siku mbili za mazoezi wameifunga Kenya. 
    Taifa Stars; Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah/Nassor Masoud ‘Chollo’ dk70, Aggrey Morris, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar/Amri Kiemba dk69, Mwinyi Kazimoto/Simon Msuva dk69, Mbwana Samatta/John Bocco dk 84, Mrisho Ngassa/Shaaban Nditi dk72 na Thomas Ulimwengu/Issa Rashid dk 89.  
    Harambee Stars; Frederick Onyango, Brian Mandela, Eugene Asike, James Situma/Christopher Wekesa dk 46, Edwin Wafula, Jerry Santo/Anthony Akumu dk 46, Peter Opiyo/Charles Okwemba dk 67, Patrick Obuya, Patrick Osaika/Mulienge Ndeto dk 73, Dennis Oliech na Wesley Kemboi/Timbe Ayoub dk 46.

    REKODI YA STARS MWAKA HUU NA RATIBA YA MECHI ZIJAZO:
    Februari 23, 2012
    Tanzania 0 – 0 DRC (Kirafiki)
    Februari 29, 2012
    Tanzania 1 – 1 Msumbiji   (Kufuzu Mataifa ya Afrika)
    Mei 26, 2012
    Tanzania 0 – 0 Malawi
    Juni 2, 2012
    Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 10, 2012
    Tanzania 2 – 1 Gambia      (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 17, 2012
    Msumbiji 1 – 1 Tanzania   (Tanzania ilitolewa kwa penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
    Agosti 15, 2012
    Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
    Novemba 14, 2012
    Tanzania 1-0 Kenya (Kirafiki)
    Machi 22, 2013
    Tanzania Vs Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 7, 2013
    Morocco Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 14, 2013    
    Tanzania Vs Ivory Coast    (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Septemba 6, 2013
    Gambia    Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YONDAN: HAIKUWA KAZI NYEPESI KUMDHIBITI OLIECH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top