• HABARI MPYA

    Wednesday, May 16, 2012

    HUU NDIO WEMBE ALIOULILIA NCHUNGA, ANANGOJA NINI KWENDA KUTIBU MAJERAHA?


    Nchunga kushoto

    SWALI moja nalojiuliza kwa sasa, wako wapi Ridhiwani Kikwete na Joel Bendera wakati huu wa vurugu zinazoendelea zenye lengo la kumng’oa Wakili Lloyd Baharagu Nchunga Yanga?
    Kwa nini najiuliza? Hawa ndio ambao walipigana kuhakikisha huyo anakuwa Mwenyekiti wa Yanga- wakifanya jitihada za kuwashawishi wanachama wa klabu hiyo wamchague.
    Mgombea Uenyekiti aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda, Francis Mponjoli Kifukwe alijitoa kwa hasira na kusababisha vurugu kubwa kwenye ukumbi wa Mkutano, PTA, Saba Saba, Dar es Salaam.
    Baada ya tukio lile niliandika makala- Nchunga hatakaa kwa raha Yanga- na kweli, sasa yametokea. Yametimia.
    Nchunga anapigwa vita- kwa sababu hakuwa chaguo la hiari la wana Yanga katika uchaguzi.
    Alijitahidi kujenga umoja ndani ya klabu na kuvunja makundi kwa maana ya kambi za uchaguzi, baada ya kuchaguliwa, akiwachagua wapinzani wake Mbaraka Igangula na Kifukwe katika Kamati mbalimbali.
    Aliingia madarakani na watu ambao si wa kambi yake- watu ambao wameendelea kutamani kufanya kazi na watu wao walioanguka, akiwemo Kifukwe.
    Huo ndio mwanzo au chanzo cha mgogoro unaoendelea hivi sasa Yanga- kwamba makovu ya uchaguzi yanaitafuna Yanga.
    Watu wamepania kuhakikisha Nchunga anaondoka Yanga kwa gharama zozote, bila kuzingatia klabu itaingia katika matatizo gani.
    Kukosa ubingwa wa Ligi Kuu, kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa jadi si kitu kwa waliopania kumng’oa Nchunga madarakani- kwani wanataka aonekana ameshindwa.
    Wanamhujumu, huo ndio ukweli ambao dalili zake zinatokana na kauli za wanaompiga vita.
    Kujiuzulu kwa Wajumbe mbalimbali mfululizo wakiwemo Ally Mayay, Seif Ahmad Magari na Abdallah Bin Kleb na kauli ya leo ya kocha Fredy Felix Minziro kwamba hatafanya kazi hadi alipwe malimbikizo ya misharaha yake- yote hii ni vita ya kumchafua Nchunga aonekane ameshindwa ang’oke kwa urahisi.
    Hii ni fitina iliyotengenezwa kitaalamu na inahitaji mweledi wa mambo haya ili kuing’amua. Matatizo ya Yanga yanayoainishwa hivi sasa si wa mwezi mmoja- ni ya muda mrefu hata kabla akina Seif, Bin Kleb hawajajiuzulu- lakini kwa nini iwe lawama ya Nchunga na si uongozi?
    Hatakiwi na anatakiwa tu ajiuzulu, ili wajipange upya na amini nakuambia Francis Mponjoli Kifukwe atakuwa Mwenyekiti pale Yanga, mara tu Wakili Nchunga akisalimu amri.
    Hakuna jinsi- hiki ndicho kipindi cha Yanga kujipanga kwa ajili ya msimu ujao, wakianzia Julai kutetea taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, hivyo katika hali ya vurugu zinazoendelea, itawezekana vipi?
    Nchunga hana ‘sapoti’ na bahati mbaya ana fedha ya kulisha familia yake na kusaidia ndugu na jamaa zake tu- lakini si kununua wanachama wa kumuunga mkono, ataweza vipi hii vita?
    Na atawezaje wakati wapinzani wake wanaonekana wana nguvu kubwa ya fedha na wenye kujua kupangilia fitina- kama hizi za makocha na wachezaji kudai wanaidai klabu Milioni 270, wakati huo huo wao wanasema aondoke wana Milioni 750 za kumaliza matatizo ya klabu.
    Umeona hiyo? Nini suluhisho hapa? Wakati mwingine hata kujitoa kwenye mapambano kwa manufaa ya wengi ni ushindi pia. Nchunga anangoja nini? Kuendelea kuukumbatia wembe ambao mapema tu aliambiwa anaachiwa umkate?
    Na umekwishamkata sasa- kwa nini asiuachie akatibu majeraha?
    Waliombeba kwenye uchaguzi Ridhiwani na Bendera ni kama hawasikii kinachoendelea kwa sasa na mbaya zaidi TFF inayosistiza Katiba za klabu kuheshimiwa na kupiga vita mapinduzi, wamekaa kimya. Nini maana yake, wanasubiri kuifungia Yanga wanachama wakifanya mapinduzi? Sijui!
    Huu ndio wembe alioulilia Nchunga, wakamuachia na sasa umemkata, anangoja nini kuachia ngazi Yanga?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUU NDIO WEMBE ALIOULILIA NCHUNGA, ANANGOJA NINI KWENDA KUTIBU MAJERAHA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top