Sasa atakaa Bernabeu hadi 2016

KOCHA Jose Mourinho amesaini mkataba mpya wa miaka minne wa kuendelea kuikochi Real Madrid hadi mwaka 2016.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 49, alianza kazi Real mwaka 2010 na kuiongoza timu kutwaa mataji ya Kombe la Mfalme katika msimu wake wa kwanza.

MATAJI YA LIGI YA MOURINHO:

  • Porto, Ureno: 2002-03 and 2003-04.
  • Chelsea, England: 2004-05 and 2005-06
  • Inter, Italia: 2008-09 and 2009-10
  • Real Madrid, Hispania: 2011-12
Msimu huu, ameiongoza Real kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu Hispania, baada ya miaka minne.
Mourinho aliyeshinda mataji mawili ya Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea, pia ameshinda mataji ya ligi za nyumbani na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Porto ya kwao Ureno na Inter Milan ya Italia.
Real ilitolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Mfalme msimu huu, baada ya kufungwa kwa jumla ya mabao 4-3 na Barcelona na ikatolewa kwa penalti kwenye Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Bayern Munich.
Lakini wametwaa La Liga kwa kuwazidi mabingwa watetezi, Barca pointi tisa, taji lao la 32 kwa jumla, lakini la kwanza tangu msimu wa 2007-08. Idadi ya jumla ya pointi zao 100 na mabao 121 katika msimu huu, ni rekodi mpya katika La Liga.