![]() |
Samatta anayetarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji Stars leo hapa akidhibitiwa na kolo Toure Jumamosi iliyopita Abidjan |
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inashuka
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Gambia katika mechi ya pili
ya Kundi C, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014
nchini Brazil.
Stars ambayo mechi ya kwanza ilifungwa 2-0 na wenyeji Ivory
Coast mjini Abidjan Jumamosi iliyopita, itacheza mechi ya tatu chini ya kocha
mpya, Kim Poulsen, aliyerithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
Poulsen amekiri kucheza mechi mbili bila kufunga hata bao
moja, sare ya bila kufungana na Malawi na kichapo cha 2-0 cha Ivory Coast, lakini
amesema timu yake imebadilika mno na anatarajia mabao katika mchezo wa leo.
Poulsen amesikitishwa na kitendo cha Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kushindwa kumpatia DVD za mechi za Gambia kuelekea mechi ya leo
na jana alisema hiyo ni mara ya pili anaomba DVD, lakini anashindwa kupatiwa, baada
ya awali kuomba DVD za Ivory Coast.
Pamoja na kukosa DVD hizo, lakini Poulsen amesema amewaandaa
vizuri vijana wake kwa ajili ya mechi hiyo, ili washinde na kujiweka kwenye
nafasi nzuri ya kuwania tiketi ya Brazil 2014.
Poulsen alisema kambi yake iko vizuri na anafurahi kiungo
mshambuliaji Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ aliyekuwa mgonjwa kiasi cha kukosa
safari ya Ivory Coast, anaendelea vizuri na anaweza akaanza leo.
Kwa upande wake, kocha wa Gambia, Mtaliano, Luciano Machini amesema
mechi ya leo itakuwa ngumu kwa sababu wapinzani wao ni wazuri.
Machini aliyechukua nafasi ya aliyekuwa bosi wake, Peter
Bonu Johnson, Mei mwaka huu, amesema kwamba Taifa Stars ni wazuri na wana kasi
uwanjani, hivyo mechi hiyo hata wachezaji wake wanajua itakuwa ngumu.
Alisema wao walicheza vizuri dhidi ya Morocco kwenye mechi
yao ya kwanza, lakini wanaingia kwenye mechi ngumu na wenyeji leo.
Nge wa Gambia waliotoka sare ya 1-1 nyumbani na Morocco
kwenye mechi ya kwanza Jumamosi, wamecheza mechi nne bila kushinda, tangu washinde
kwa mara ya mwisho Agosti 10, mwaka jana mabao 3-0 katika mchezo wa kirafiki
dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ilifungwa 1-0 na Namibia Septemba 3, mwaka jana, ikatoka
sare ya 1-1 na Burkina Faso Oktoba 8, mwaka jana, ikafungwa 2-1 na Algeria
Februari 29, mwaka huu kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Morocco nyumbani Jumamosi
iliyopita.
Rekodi ya Tanzania pia si nzuri katika mechi za nyumbani na
tangu iifunge Jamhuri ya Afrika ya Kati Machi 26, mwaka jana haijashinda tena
mechi kwenye Uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 na imecheza saba
baada ya hapo.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwa; J.
Kaseja, Kelvin Yondan, Amir Maftah, Juma Nyosso, K. Yondan, M. Ngassa, S. Nditi,
M. Kazimoto, M. Samata, H. Moshi na S. Abubakar.
Gambia: C. Allen, A. Jammeh, O. Koli, M. Danso, T. Jaiteh, Y.
Ceesay, P. Jagne,
P. Kujabi, M. Jarju D. Savage na M. Ceesay.
Kikosi cha Stars kilichoifunga Afrika ya Kati |
MATOKEO YA STARS TAIFA TANGU ISHINDE MARA YA MWISHO:
Machi 26, 2011: Tanzania 2 – 1 Afrika ya Kati (Kufuzu CAN)
Mei 14, 2011: Tanzania 0
– 1 Afrika Kusini (Kirafiki)
Sept 3, 2011: Tanzania 1 – 1 Algeria (Kufuzu CAN)
Nov 15, 2011: Tanzania 0
– 1 Chad (Kufuzu Kombe la Dunia)
Des 3, 2011: Tanzania 1 – 2 Zimbabwe (Kirafiki)
Feb 23, 2012: Tanzania 0 – 0 DRC (Kirafiki)
Feb 29, 2012: Tanzania 1 – 1 Msumbiji (Kufuzu CAN)
Mei 26, 2012: Tanzania 0 – 0 Malawi (Kirafiki)
0 comments:
Post a Comment