• HABARI MPYA

    Sunday, October 07, 2012

    AKINA SAMATTA WANG'ANG'ANIWA NA ESPERANCE NYUMBANI, SUNZU ALIMWA NYEKUNDU

    Samatta kushoto katika moja ya mechi za Mazembe zilizopita

    Na Prince Akbar
    TOUT Puissant Mazembe imelazimishwa sare ya bila kufungana na mabingwa wa Afrika, Esperance ya Tunisia katika Nusu Fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo kwenye Uwanja wa Stade du TP Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Katika mchezo huo, Mazembe ilipata pigo kutokana na beki wake tegemeo, Stopila Sunzu kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano (nyekundu) dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida.
    Awali, Sunzu kaka wa mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu, alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
    Washambuliaji wote wawili wa Kitanzania walicheza mechi hiyo, Mbwana Ally Samatta alicheza hadi dakika 83 alipompisha Sinkala, wakati Thomas Emanuel Ulimwengu alitokea benchi dakika ya 58 kwenda kuchukua nafasi ya D. Kanda.
    Matokeo haya yanamaanisha Nusu Fainali ya pili mjini Tunis itakuwa kali zaidi na hata sare yoyote ya mabao itaipeleka Mazembe fainali.  
    Katika Nusu Fainali nyingine ya kwanza iliyochezwa jana, mabingwa mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri walilazimisha sare ya kufungana mabao 3-3 na Sunshine Stars ya Nigeria katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana iliyopigwa huko Ijebu-Ode kwenye Uwanja wa kimataifa wa Dipo Dina.
    Nahodha wa Sunshine, Godfrey Oboabona aliikosa mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Esperance ya Tunisia, wakati Mohamed Aboutrika anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi miwili na Ahly.
    Ahly ilipata bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Mohamed Nagy, aliyefumua shuti kutoka nje ya boksi na kumtungua Moses Ocheje, kabla ya Mahdy El Sayed kuifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 30, wakati Sunshine ilipata bao la kwanza dakika ya 40, kupitia kwa kiungo Mcameroon, Tamen Medrano aliyemtungua kwa shuti la mbali kipa wa Ahly, Sherif Elkramy.
    Wenyeji walisawazisha dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti wa Dele Olorundare baada ya Ajani Ibrahim kuangushwa kwenye eneo la hatari na Mohamed Nagy.
    Pamoja na hayo, Mashetani Wekundu wa Cairo walipata bao lililoelekea kuwa la ushindi, dakika moja badaaye kupitia kwa kijana mwenye umri wa miaka 25, Nagy ambalo lilikuwa bao lake la pili kwenye mechi hiyo.
    Beki wa Sunshine, Precious Osasco aliisawazishia timu yake dakika ya 83 kwa shuti la mpira wa adhabu lililomshinda kipa Elkramy.  Nagy alipata nafasi ya kukamilisha hat-trick dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho, lakini kichwa chake kiliupaisha mpira alipokuwa anaunganisha kona. Mechi za marudiano zitachezwa wiki ijayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AKINA SAMATTA WANG'ANG'ANIWA NA ESPERANCE NYUMBANI, SUNZU ALIMWA NYEKUNDU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top