![]() |
Hans Poppe, Mwenyekiti wa F.O.S. |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI
wa Friends Of Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba jana walikutana
kujadili mechi ya juzi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga na wakagundua kuna
wachezaji walicheza chini ya viwango vyao, hivyo watatoa pendekezo kwa Kamati
ya Utendaji ya klabu, wachezaji hao waitwe kuhojiwa juu ya hilo.
“Kama mtu
alishindwa kucheza kwa sababu alikuwa anaumwa, au kitete au vipi, lazima tujue,”alisema
Hans Poppe alipozungumza na BIN ZUBEIRY ‘mida hii’.
Aidha, Hans
Poppe alisema F.O.S. walikubaliana pia kutoa pendekezo kwa wachezaji Emmanuel
Okwi, Amir Maftah na Haruna Moshi ‘Boban’ wachukuliwe hatua za kinidhamu kwa rafu
za ‘kipuuzi’ walizocheza siku za karibuni.
“Msimu
uliopita tulikuwa tuna rekodi nzuri sana ya nidhamu katika timu yetu, lakini
msimu huu hali ni tofauti, sisi hatuungi mkono hii kitu, mechi tano tu, lakini
tuna kadi nyekundu mbili, lazima tuifanyie kazi, ili timu icheze soka ya
kiungwana,”alisema Hans Poppe.
Kapteni huyo
wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba Friends Of Simba
haina mamlaka wala maamuzi ndani ya Simba zaidi ya kutoa ushauri kwa Kamati ya
Utendaji, ambayo ndio inaweza kuamua kuchukua hatua, hivyo haya yote bado si
hatua rasmi ya klabu.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka Simba zimesema miongoni mwa
wachezaji wanaotajwa kucheza chini ya viwango vyao juzi ni Mrisho Ngassa, wakati
beki Shomary Kapombe atazawadiwa na ‘kwa kujituma ile mbaya’ kwenye
mechi hiyo.
Katika kundi
la Ngassa wamo pia Haruna Moshi ‘Boban’, Mwinyi Kazimoto na Daniel Akuffo,
wakati upande wa waliopiga ‘mzigo wa uhakika’, mbali na Kapombe, wengine ni Juma
Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Jonas Mkude, Amri
Kiemba, Felix Sunzu na Edward Christopher, ambao pia watazawadiwa.
Simba
itafanya mazoezi leo kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam kuanzia
saa 10:30 na baada ya hapo wachezaji wataingia kambini kwa ajili ya mechi ya
Jumapili dhidi ya JKT Oljoro, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba juzi
ilishindwa kuendeleza ubabe wake kwa Yanga, baada ya kulazimishwa sare ya
kufungana bao 1-1 na wapinzani wao hao wa jadi, katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa
1:02 usiku.
Yanga ambao
walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi
nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha
kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.
Hadi
mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo
Amri Kiemba dakika ya pili.
Simba
walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na
kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya
kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
Pasi zao
zilikuwa nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa
nguvu na wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa
ya mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
Katika
kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya
kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.
Kabla hata
ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts
alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo,
ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan
Cirkovick.
Kipindi cha
pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar
Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza
nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Angalau,
kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi
yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa
Msimbazi ilikuwa kikwazo.
Katika
dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na
refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na
Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Katika
dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja
Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’.
Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa
kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na
hasira za kitoto.
Pamoja na
Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya
pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi
yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya
beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake
ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia
hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na
alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
Alipingia
Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza
na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Baada ya
mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na
Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema
Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu
msimu huu itakuwa ngumu.
Kwa upande
wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na
kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi
nyingi,”alisema Brandts.
0 comments:
Post a Comment