• HABARI MPYA

    Saturday, October 13, 2012

    KAZI IPO MKWAKWANI LEO COASTAL NA SIMBA SC LIGI KUU

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo kwa timu 10 kupambana kwenye viwanja vitano tofauti katika raundi ya saba ya ligi hiyo yenye timu 14, macho na masikio ya wengi yakielekezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambako mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wakimenyana na mabingwa wa 1988, Coastal Union.
    Vigogo wa Friends Of Simba (F.O.S) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Zacharia Hans Poppe wamekodi ndege kwenda Tanga kuwaongezea morali washinde mechi ya leo, ambayo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana wenyeji kupania kuwa timu ya kwanza kuifunga Simba msimu huu.
    Ikumbukwe Simba imetoa sare moja ya kufungana 1-1 na Yanga, Oktoba 3, mwaka huu katika mechi zake sita ilizocheza sasa na nyingine zote tano imeshinda, jambo ambalo linawafanya waendelee kuwa kileleni mwa Ligi Kuu.
    Simba, ambayo kwenye mechi hiyo itawakosa nyota wake saba, Emanuel Okwi ambaye amekwenda kujiunga na timu yake ya taifa, Uganda, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Khalfan Ngassa wanaosumbuliwa na Malaria, Haruna Shamte, Kiggi Makassy Kiggi, Hamadi Waziri na Komabil Keita ambao ni majeruhi ipo Tanga tangu Jumatano.
    Wachezaji 22 walio na timu Tanga ni makipa Juma Kaseja, Wilbert Mweta, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyoso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Hassan Khatib, Paulo Ngalema, Komabil Keita, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Salim Kinje, Ramadhani Singano, Uhuru Suleiman, Haruna Moshi ‘Boban’ na washambuliaji Felix Sunzu, Edward Christopher, Haroun Chanongo, Daniel Akuffo na Abdallah Juma.
    Katika kujiandaa na mechi ya leo, ambayo itachezeshwa na refa Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Abdallah Uhako wote kutoka Arusha, Simba Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kuifunga Azam FC mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
    Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya 2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Azam na Simba zitakutana tena katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.     
    Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
    Katika mechi ya leo, Simba SC inawahofia zaidi wachezaji wake wa zamani ambao kwa sasa wanachezea Coastal.
    Gumzo ndani ya Simba kuelekea mchezo huo ni namna ambavyo wachezaji wao waliowatema na sasa wanachezea Coastal watakavyojituma katika mechi hiyo ili kuonyesha wao bado wachezaji wazuri.
    Wachezaji wa zamani wa Simba kwenye kikosi cha Cosatal ni mabeki Said Swedi ambaye ni Nahodha wa timu, Juma Jabu, kiungo Jerry Santo na washambuliaji Nsa Job na Sali Aziz Gilla.
    Wachezaji wote hao huwa wanaanza kwenye kikosi cha kwanza cha Cosatal na leo pia, kuna uwezekano Swedi ‘Panucci’ akaanza beki ya kulia na JJ akacheza kushoto, wakati kwenye kiungo Mkenya, Santo ataichezesha timu.
    Kuna uwezekano mkubwa sana Salim Aziz Gilla akatokea benchi, lakini ‘piga ua’, mkali wa mabao, Nsa Job lazima ataanza kwenye mechi hiyo kujaribu kufanya kile alichokifanya msimu uliopita akiwa Villa Squad, kutikisa nyavu za Simba kwa bao muhimu.  
    Lakini pia, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu 1988, kina wachezaji wengine wa kutisha kama kiungo Razack Khalfan aliyewahi kucheza Yanga na mshambuliaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Atupele Green, ambaye huenda akaanza na Nsa leo pale mbele.
    Katika mechi nyingine, Polisi Morogoro itaikaribisha Azam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati refa wa FIFA, Oden Mbaga atakuwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuchezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na Oljoro JKT.
    Mechi nyingine za leo ni Ruvu Shooting dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, na Mtibwa Sugar watacheza na Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAZI IPO MKWAKWANI LEO COASTAL NA SIMBA SC LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top