KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) ilikutana Oktoba 11, 2012 kujadili michakato ya chaguzi mbalimbali za
wanachama wa Shirikisho. Katika kikao chake, Kamati ilijadili michakato ya
chaguzi za viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Rukwa (RUREFA),
Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT), Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa
wa Shinyanga (SHIREFA) na Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es salaam
(DRFA),.
Pia Kamati ilijadili mchakato wa chaguzi za Chama cha Madaktari
wa Michezo (TASMA) na kupokea mchakato wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa
Mbeya (MRFA).
Baada ya kujadili chaguzi hizo kwa kina, Kamati ilifikia
uamuzi ufuatao:
1. FRAT
Uchaguzi wa FRAT haukufanyika baada ya wajumbe kugoma
wakipinga kuondolewa kwa baadhi ya wagombea. Kamati ilikubaliana kuiagiza
Kamati ya Uchaguzi ya FRAT kuhakikisha uchaguzi unafanyika Novemba 17, 2012 na
kufanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na sehemu ambako uchaguzi huo
utafanyika. Mkutano utatakiwa kuwapigia kura wajumbe waliopitishwa kugombea
uongozi tu.
2. RUREFA
Baada ya kufuta uchaguzi wa viongozi wa RUREFA na kuivunja
Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeitaka Kamati ya
Utendaji ya RUREFA kuteua kamati mpya ya uchaguzi ya chama hicho kabla ya
Oktoba 20, 2012 na kuiagiza kamati mpya kuwa imeshatangaza mchakato wa uchaguzi
ifikapo Oktoba 24, 2012.
3. SHIREFA
Kamati ilipokea pingamizi dhidi ya baadhi ya wagombea uongozi
wa SHIREFA na hivyo kuagiza walioweka pingamizi na waliowekewa pingamizi pamoja
na mwakilishi wa Kamati ya Uchaguzi ya SHIREFA kuhudhuria kikao cha Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Alhamisi ya Oktoba 18, 2012 kwa ajili ya
maamuzi ya mwisho.
4. MRFA
Kamati ilipokea rufaa na pingamizi kutoka kwa baadhi ya
wagombea walioenguliwa kuwania uongozi wa chama hicho na hivyo imewataka
walioweka pingamizi na waliokata rufaa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uchaguzi
ya TFF kitakachofanyika Oktoba 18, 2012 jijini Dar es salaam.
5. TASMA
Kamati iliona mapungufu katika mchakato wa uchaguzi wa
viongozi wa TASMA na kuamua chama hicho kifanye uchaguzi ifikapo Desemba mosi
badala ya uchaguzi kufanyika Oktoba 27,
2012 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaiagiza
Kamati ya Uchaguzi ya TASMA kuhakikisha kasoro zilizojitokeza zinarekebishwa
ili uchaguzi ufanyike kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na Kanuni za
Uchaguzi.
6. DRFA
Awali, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilitangaza kuwa hatma ya
uchaguzi wa DRFA itajulikana baada ya kikao cha leo, lakini kutokana na wajumbe
kutoweza kuhudhuria kwa sababu tofauti, mustakabali wa suala hilo sasa
utajulikana baada ya kikao cha Oktoba 18, 2012.
Wagombea na wadau wanaotakiwa kuhudhuria kikao cha Oktoba 18,
2012 wanataarifiwa kuwa kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
ofisi za TFF kuanzia saa 08:2012.
Kamati inawaomba wajumbe wote kuhudhuria bila ya kukosa.
Angetile Osiah
Katibu Mkuu TFF