![]() |
Zena Chande anawania Ujumbe wa Mkutano Mkuu TFF kupitia TWFA |
Na Princess Asia
WAGOMBEA 13 kati ya 15 waliojitokeza kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi kwenye Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania
(TWFA) wamepitishwa baada ya usaili uliofanyika juzi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA,
Ombeni Zavala, waliopitishwa kwenye nafasi ya Uenyekiti ni Isabellah Huseein
Kapera, Joan Ndaambuyo Minja na Lina Paul Kessy.
Makamu Mwenyekiti ni Rose Kisiwa wakati wanaowania nafasi ya
Katibu Mkuu ni Amina Ali Karuma na Cecilia Oreste Makafu. Mgombea pekee wa
nafasi ya Katibu Msaidizi, Macky Righton Mhango naye amepita kwenye usaili huo.
Aliyepitishwa kwenye nafasi ya Mhazini ni Rose Stewart Msamila.
Furaha Francis na Zena Chande wamepitishwa kuwania nafasi ya
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati
waliopita kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TWFA ni Triphonia Ludovick
Temba, Rahim Salum Maguza na Sophia James Charles.
Hivi mchakato wa uchaguzi wa TWFA uko katika kipindi cha
kukata rufani ambapo ni kuanzia Oktoba 15-17 mwaka huu. Rufani zinatakiwa
zifike kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 kamili jioni ya Oktoba 17 mwaka
huu.
Wagombea wawili ambao hawakupitishwa kwa ajili ya uchaguzi
huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 4 mwaka huu ni Julliet Mndeme na Jasmin Soud
walioomba ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF. Wagombea hao ambao pia walikuwa
wamewekewa pingamizi hawakufika kwenye usaili.
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeupongeza
uongozi mpya wa Chama cha Soka Pwani (COREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi
uliofanyika Oktoba 14, mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama
hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa COREFA walivyo na imani kubwa
kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Pwani.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya COREFA chini ya Uenyekiti wa Hassan Othman Hassan ‘Hassanoo’ ambaye
amechaguliwa tena kuongoza chama hicho.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Pwani kwa kuzingatia
katiba ya COREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
TFF pia imetoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya COREFA na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu
wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Hassan Othman
Hassan (Mwenyekiti), Riziki Majala (Katibu), Geofrey Irick Nyange (Mjumbe wa
Mkutano Mkuu TFF), Juma Haruna Kisoma (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Abubakar
Allawi (Mhazini).
Waliochaguliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji katika
uchaguzi huo uliofanyika kisiwani Mafia ni
Mussa Bakari Athumani, Godfrey Magnus Haule na Gwamaka Oden Mlagila.
Mwakilishi wa Wanawake ni Florence Ambonisye.