IMEWEKWA JULAI 4, 2013 SAA 10:36 JIONI
WAKATI Phil Neville amerejea Manchester United kama kocha Msaidizi wa kikosi cha kwanza chini ya kocha mpya, David Moyes, Ryan Giggs naye ameingizwa kwenye benchi la Ufundi.
Beki wa zamani wa United, Neville aipigwa picha akiwasili Carrington mapema leo asubuhi, ambako anatarajiwa kutangazwa kuwa mtu mpya katika benchi la Ufundi chini ya Moyes sambamba na Chris Woods, Steve Round, Robbie Cooke na Jimmy Lumsden aliokuwa nao Everton.
Na gwiji wa klabu, Giggs, mwenye umri wa miaka 39, ambaye anatarajiwa kuhitimu mafunzo ya ukocha la leseni ya UEFA Pro msimu ujao, atakuwa kocha mchezaji baada ya kusaini Mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi.
Wameungana: Phil Neville atakuwa Msaidizi wa David Moyes kama kocha wa kikosi cha kwanza cha Manchester United
Kocha: Ryan Giggs atakusanya uzoefu chini ya Moyes huku akijiendeleza kielimu juu ya ukocha
Moyes alianza kuiongoza United mazoezini asubuhi ya leo Carrington na Neville aliingia kazini moja kwa moja sambamba na Lumsden na Round, ambako alipanga koni wakati wa mazoezi.
Neville, mwenye umri wa miaka 36, alihitimisha miaka yake 18 ya kucheza soka mwezi uliopita. Lakini ilikuwa ni Old Trafford ambako beki huyo wa zamani wa England alitengeneza jina lake tangu aibuke mwaka 1992.
Alicheza mechi 250 kwa mabingwa hao wa sasa wa Ligi Kuu England kabla ya kwenda kuishi kwa miaka nane Goodison Park chini ya Moyes.
Neville, ambaye amekuwa Nahodha wa Everton tangu mwaka 2007, amekuwa akipata mafunzo ya ukocha na tayari ana leseni B ya UEFA. Amekamilisha mafunzo yake ya kuchukua leseni A huko St George's Park mwishoni mwa Mei na licha ya ofa kadhaa wakati anaendelea kucheza na na nafasi ya kuingia vyombo vya habari, lakini alikataa.
Neville alikuwa sehemu ya benchi la Ufundi la timu ya vijana ya England chini ya umri wa miaka 21 ikiboronga kwenye michuano ya Euro majira haya ya joto.
Amerudi: Neville alicheza kwa miaka 10 kikosi cha kwanza Old Trafford kabla ya kutimkia Everton mwaka 2005