• HABARI MPYA

    Monday, July 08, 2013

    YANGA SC WAPANDA NDEGE HADI UGANDA KUMALIZANA NA KIIZA, WAKUBALIANA KILA KITU SAFI, BADO KUMPA FEDHA TU AMWAGE WINO...ILA URA NAO WANAMSAKA ILE MBAYA KWA DAU KAMA LA JANGWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 8, 2013 SAA 6:55 MCHANA
    MFANYABIASHARA mwenye jina mjini, Mussa Katabaro amekwea pipa hadi Uganda na kufanya mazungumzo ya kina na mshambuliaji Hamisi Friday Kiiza ili abaki Yanga na hatimaye amekubali kuendelea kuvaa jezi za kijani na njano kwa miaka mingine miwili.
    Katabaro ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Mashindano, chini ya Mwenyekiti Abdallah Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba wamemalizana na Kiiza na atabaki Jangwani.
    Anabaki?; Mussa Katabaro kushoto, akimpongeza Kiiza baada ya mechi na Simba Mei mwaka huu. Mfanyabishara huyo yupo katika jitihada za kumbakiza Kiiza Jangwani. Atafanikiwa? 

    “Siwezi kuzama ndani juu ya makubaliano yetu sisi na yeye, ila nachoweza kusema ni kweli nilikwenda Uganda na tukazungumza naye, tumekubaliana na muda si mrefu atasaini na kuja Dar es Salaam kuendelea na kazi,”alisema.
    BIN ZUBEIRY inafahamu Katabaro alikuwa Kampala Jumanne iliyopita na katika mazungumzo yake na Diego wamekubaliana kumuongezea Mkataba wa miaka miwili kwa dau la dola za Kimarekani 40,000.
    Lakini Katabaro akaomba Kiiza akubali kuchukua dola 20,000 kwa sasa na dola 20,000 nyingine atampa katika mwanzo wa mwaka wa pili wa Mkataba wake. Kiiza akasema anataka dola 40,000 kamili kwa sababu ana kitu anataka kufanya na ndiyo maana alikataa kupokea dola 35,000 na gari, ilia pate fedha kamili.
    Pamoja na hayo, Yanga SC watalazimika kumalizana na Kiiza haraka, kwa sababu URA ya Uganda inataka kumsaini kwa mshahara wa dola 1,000 na dau la usajili dola 40,000 kama ambazo ameahidiwa Jangwani. Yanga watampa Kiiza mshahara wa dola 1,500 kwa mwezi, ikiwa ni dola 500 zaidi kutoka wanazotaka kumpa URA.
    Ni marafiki; Kiiza akiwa na Katabaro na familia yake baada ya mechi na Simba SC.

    Awali, Kiiza aligoma kusaini Yanga kutokana na kulazimishwa achukue dola 35,000 na dola 5,000 nyingine apewe gari.
    Kiiza anaishi Uganda na Tanzania yupo kwa ajili ya kazi na haoni umuhimu wa kumiliki gari Dar es Salaam, hivyo anataka fedha, lakini Yanga watu wanaohusika na usajili Yanga iliadaiwa walikuwa wanamlazimisha achukue na gari.
    Kiiza alimaliza vizuri Mkataba wake wa kwanza wa miaka miwili Yanga SC kwa kufunga bao zuri la ushindi dhidi ya mahasimu, Simba SC miezi miwili iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wana Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0, bao la kwanza likifungwa na Mrundi, Didier Kavumbangu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC WAPANDA NDEGE HADI UGANDA KUMALIZANA NA KIIZA, WAKUBALIANA KILA KITU SAFI, BADO KUMPA FEDHA TU AMWAGE WINO...ILA URA NAO WANAMSAKA ILE MBAYA KWA DAU KAMA LA JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top