• HABARI MPYA

    Saturday, August 03, 2013

    NGUVU HII TUIHAMISHIE KWENYE MATUMIZI YA NEMBO, HUSUSAN SUALA LA JEZI, SIMBA NA YANGA ZINAUMIA

    IMEWEKWA AGOSTI 3, 2013 SAA 3:07 ASUBUHI 
    KLABU za Yanga na Simba ni tajiri mno katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, kwani zina rasilimali nyingi sana kama rasilimali watu na majengo.
    Rasilimali watu ni nguzo kuu ya timu yoyote ulimwenguni, ndio maana timu za Ulaya zinakwenda Asia kujiongezea mashabiki zaidi, kwa sababu chanzo kikuu cha utajiri wao ni  matumizi ya Nembo yao kwa kuuza vifaa vyao kama jezi, skafu, kofia, opena, bangili, wakati mwingine hata shuka na nguo za ndani.
    Huwezi kufanya yote hayo bila kuwa na mashabiki, hizi timu za Yanga na Simba tayari zinao na ndiyo mtaji wenyewe. Pamoja na hivyo, lakini ajabu zimeshindwa kutumia hiyo fursa na sasa kuonekana ombaomba.

    Vifaa vinauzwa, tena mbele ya macho ya viongozi tangu enzi na enzi mpaka leo na timu ni masikini, eti zinaendeshwa kwa fedha za wafadhili na hakuna bajeti Msimbazi wala Jangwani.
    Haijulikani kwa mwaka wanatumia Sh ngapi na vyanzo vyao vya mapato ni vipi. Bora liende, asubuhi jioni siku ya kwanza, mwezi, mwaka na wanashitukia miaka minne inakatika, viongozi wanamaliza muda wao madarakani, zinaanza kampeni tena zenye maneno matamu matamu, lakini ukiwaona wahusika usoni, waona kabisa hakuna ushurikiano wa mioyo na midomo yao. Kwani tamko la mgomo haliko moyoni, ila kwa kuwa moyo hauwezi kuuzuia mdomo usiseme, unabaki kusononeka kwa usaliti unaofanyiwa na mgombea, utaona sononeko la moyo kupitia uso wa mgombea.
    Pamoja na Moyo wa wagombea kujidhihirisha, sononeko lao kupitia uso wa wagombea huchaguliwa kwa kishindo mno, hii yawezekana ikawa kutokuwa na umakini wa wapiga kura kuchunguza sura za wagombea, au kuamini mtu yoyote mwanye elimu ya chuo kikuu, anaweza uongozi au kuamini mtu yoyote aliyecheza mpira kwa mafanikio anaweza uongozi.
    Ingawa wengi wao kile kigezo cha angalau uwe na elimu ya Kidato cha nne kiliwaondoa, kwani wengi wao hawana elimu hiyo na si kwa kupenda ni kutokana na mfumo wa elimu wa Tanzania, huwezi kufanikiwa vyote, wapo waliokua na vipaji vilikufa na sasa ni watumishi wa wananchi katika Idara mbalimbali, mpira basi tena na wale waliochagua michezo, elimu basi tena.
    Au wanafikiri mtu akiwa na fedha na tajiri ataisaidia timu tu, bila kunufaika yeye kwa imani tu tajiri haibi, kwa kuwa ana fedha, hayo yote huwagubika wapiga kura, kuchagua viongozi wetu katika timu zetu za Yanga na Simba na kutokuwachunguza usoni, ili kuona kama mioyo yao ina ushirikiano na midomo yao.
    Leo biashara ya vifaa (jamii ya jezi) za Simba na Yanga inaonekana haina maana kabisa mbele ya viongozi wetu na sio vitu vya kuingizia timu fedha. Hii dhana sio sahihi na wanajua ni mali yenye fedha nyingi mno, kwa kuwa wananufaika nayo, wanajifanya hiyo biashara haipo na kama ipo haina kipato cha kuingizia timu.
    Ninasema wanajua, kwa jinsi suala la haki ya matangazo lilivyojitokeza. Simba SC wamekubali haraka, inawezekana wana sababu zao za msingi, ila Yanga wameng'aka kwa kutoa sauti kubwa na kuwashirikisha viongozi wa matawi nao wakawaunga mkona wakapiga kelele kama viongozi wao.
    Sisemi kama ni vibaya, la hasha, wapo sahihi kwa jinsi waonavyo pia ni jambo zuri wa kuwashirikisha wanachama na ni matumizi mazuri ya Rasilimali watu, ila kwa nini haki ya matangazo tu ndiyo wanachama washirikishwe?
    Hawa wanachama wakishirikishwa pia kumjua mwizi wa matumizi ya Nembo kwa vifaa vya hizi timu na wezi wanajulikana, kwani hawaviuzi kama madawa ya kulevya au bangi kwa siri, hapana wanauza mchana kweupe na duka lao kubwa la kuuzia ni uwanjani siku za mchezo hasa timu zao zinapocheza tena na viongozi wapo wanawaona wauzaji wakipita mbele yao. Inakuwaje hawawakamati kama hawamtambui muuzaji anayetumia Nembo kwa manufaa yake na si kwa timu?
    Uuzaji wa vifaa (jezi) vya hizi timu kwa mtazamo wangu, viongozi wanajua kabisa nani muhusika wa usaliti wa hivi vilabu na wahujumu wakubwa kwa maendeleo ya hizi timu na Taifa kwa ujumla.
    Viongozi wanahusika kwa mazingira ya biashara hii, tena kuna uwezekano wana hisa katika hizi kampuni zinazohujumu au wana ushirikiano bila kutilia shaka, vinginevyo wangepiga kelele tena wangewahimiza wanachama kukamata au kutoa taarifa Polisi, kwani ni wezi kama wezi wengine.
    Ila wapo kimya wanafurahia timu kuwa masikini, kuwa ombaomba na wao kuchangia waonekane wana msaada mkubwa kwa timu, ila huo ni msaada wa udhalilishaji, kwa kuwa huwezi kupanga maendeleo ya msingi kwa fedha iliyo mfukoni kwa jirani yako, eti ana huruma na wewe anakupenda ukiwa na shida atakusaidia.
    Hutaendelea kamwe, utakuwa tu mtu wa kuomba omba maisha yako yote. Kwa nini uombe wakati una akili na nguvu, basi hata jirani umuazime vitendea kazi kwa muda, fanya kazi kwa juhudi na maarifa, baadaye nawe uwasaidie wengine, lakini ukiona jirani yako anafurahia hali yako ya kuomba omba, ujue ananufaika na hiyo hali.
    Na hata ukimuomba vitendea kazi, hata kama anavyo, hatakupa maana yake hataki ujitegemee, yawezekana wewe ndiye chanzo cha utajiri wake, ukijitegemea yeye atakuwa ombaomba.
    Narudia tena kusema, Yanga na Simba si masikini hata kidogo, ni matajiri wa kutupwa hawastahili kuwa omba omba, ila sehemu kubwa ya viongozi wetu, yawezekana hawajui namna ya kwatumia Rasilimali watu na hawajui ni utajiri huo au ni wabinafsi tu, wanakwenda kujiongezea kipato.
    Kama alikuwa ni mtu wa kipato cha kawaida na kama ni tajiri, basi kuongezea utajiri wake watu wanasema ukiwa tajiri, hutamani kuiba, si kweli, wizi ni tabia na Mzee Mengi kasema juzi juzi hapa, kwa mazingira ya Tanzania, huwezi kuwa tajili bila kuiba, au bila kutoa rushwa na ukiingia huko huwezi kuacha.
    Sina maana viongozi wa Yanga na Simba ni wezi, watoa rushwa, la hasha, ila ni kwa nini wasomi, tena wakati mwingine ni wanasheria na wengine matajiri hawaonekani kuzitendea haki hizi timu ziondokane na udhalilishwaji wa kuomba omba.
    Karibu zinatimiza umri wa miaka 80 sasa bila kujitegemea na hakuna dalili hizo, leo wala kesho zimebaki ni propaganda tu, wengine wanaomba miaka mingine 50 ili wajenge uwanja kama Serikali ilivyofanya, ila wamesahau Uwanja wa Serikali ulijengwa mara tu tulipopa Uhuru.
    Ndio maana waitwa uwanja wa Uhuru, ulikidhi mahitaji kwa wakati ule na ulikuwa bora pia kwa muda ule, leo watu wameongezeka na teknolojia pia imekuwa ndio maana wakaamua kujenga Uwanja mwingine mkubwa zaidi.
    Nao miaka 50 ijayo si kitu tena ingawa leo wasifika kila pembe ya nchi na wanawaambia wanachama wao, tumieni akili ya kawaida eti miaka miwili haitoshi, hiyo si njia sahihi ya kujibu hoja za wanachama.
    Pia wanachama nao wanapenda mafanikio ya timu bila kujua pengine yanatokana na matakwa ya uongozi, wakiwa na nia ya mabadiliko ya kweli yatakuwepo, ila wagombea wote wenye nia ya dhati ya mabadiliko hawawezi kuhonga, anahonga ili iweje?
    Ukiona mtu anahonga kupata uongozi wa huduma tu, basi ana walakini mkubwa, anakuja kujinufaisha mwenyewe, hana lingine. Ila Tanzania ili upete uongozi, lazima uhonge na wapiga kura wanafurahia, wanasahau wanahitaji maendeleo na muhongaji atafanya yake. 
    Nawasihi wabadilike, wachgue mtu ambaye mchango wake wa kimaendeleo katika mpira unajulikana kuanzia mtaani kwake. Leo Simba na Yanga unachukua kadi leo, kwa kuwa unahonga, unakuwa kiongozi. Huyo mtu hana mapenzi ya kweli, hata kwenye viwanja haendi, atajuaje mazuri na matatizo ya mpira?
    Anakuja kufanya biashara tu na timu zitaendelea kuwa ombaomba. Nimalize kwa kusema, viongozi wawaambie wanachama wao, mwizi wa matumizi wa nembo zao ni nani?
    Ikiwezekana, wawashirikishe wanachama wao kupiga kelele kukamata na kuwaambia, hata ikibidi wagomee kuzinunua kama walivyowashirikisha kugomea haki ya matangazo kwa Yanga. 
    Hata hivyo, bado swali langu ni nani muuza jezi zenye nembo ya hizi timu na wao viongozi wa timu hawachukui hatua na lini hizi Nembo zitazinufaisha hizi timu?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGUVU HII TUIHAMISHIE KWENYE MATUMIZI YA NEMBO, HUSUSAN SUALA LA JEZI, SIMBA NA YANGA ZINAUMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top