• HABARI MPYA

    Thursday, August 08, 2013

    SURE BOY, KIPRE TCHETCHE NA BOCCO WAMTOA UDENDA MOLOTO, ASEMA VIJANA WANAWEZA KAZI PSL

    Na Mahmoud Zubeiry, Johannesburg, Afrika Kusini
     IMEWEKWA AGOSTI 8, 2013 SAA 7:25 MCHANA
    MSAKA vipaji Mkuu wa klabu ya Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini, Trott Nchilo Moloto amevutiwa na wachezaji watatu wa Azam FC, kiungo Salum Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na washambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Herman Tchetche.
    Moloto aliyewahi kuifundisha Simba SC ya Dar es Salaam kwa mwezi mmoja tu mwaka 2005, alivutiwa na wachezaji hao baada ya mchezo wa jana wa kirafiki baina ya timu hizo Uwanja wa Mamelodi, uliopo makutano ya barabara za Cnr Allandale na Dunlop, huko Chloorkop, Midrand mjini hapa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi, kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, alisema kwamba zaidi amevutiwa na kiungo Sure Boy, lakini akasema hata Bocco na Adebayor ni wakali.
    11 wa hatari; Kikosi cha Azam kilichoifunga mamelodi 1-0 jana. Sure ni wa katikati walioinama, Bocco wa kwanza kulia waliosimama na Tchetche wa kwanza kushoto waliosimama 


    PROGRAMU YA AZAM AFRIKA KUSINI:

    AGOSTI 3, 2013: 
    Kuwasili J’burg kutoka Dar 
    AGOSTI 4, 2013: 
    Mazoezi (Chuo Kikuu cha Wits)
    AGOSTI 5, 2013: 
    Azam 0-3 Kaizer Chiefs 
    AGOSTI 6, 2013: Mazoezi (Chuo Kikuu cha Wits)
    AGOSTI 7, 2013: 
    Azam 1-0 Mamelodi Sundwons 
    AGOSTI 8, 2013: 
    Mazoezi (Chuo Kikuu cha Wits)
    AGOSTI 9, 2013: 
    Azam Vs Orlando Pirates
    AGOSTI 10, 2013: Mazoezi (Chuo Kikuu cha Wits)
    AGOSTI 11, 2013: 
    Mazoezi (Chuo Kikuu cha Wits)
    AGOSTI 12, 2013: 
    Azam Vs Moroka Swallows 
    AGOSTI 13, 2013: Kuondoka Johannesburg kurejea Dar es Salaam 
    Alipoulizwa kuhusu wachezaji kuweza kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini, PSL yenye maslahi zaidi kuliko Tanzania, Moloto alisema klabu yoyote inaweza kukubali kuwasajili kwa uwezo wao wa sasa, lakini ili kufanya vyema katika ligi hiyo, wanatakiwa kufanya juhudi, kwa kuwa kuna ushindani mkubwa.
    “Ligi ya PSL ni suala lingine, unapokuwa hapa lazima uwe fiti sana, lazima uwe mshindani sana, hapa kuna wachezaji kutoka kila sehemu ya dunia na wanalipwa vizuri pengine kuliko Ulaya, ni pagumu sana, wanaweza kwa uwezo wao wa sasa, ila lazima wafanye kazi sana,”alisema.
    Baada ya kuondoka Simba SC mwaka 2005, Moloto alichukua wachezaji wawili, beki Victor Costa na mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi akaenda nao Meritzburg Classic alipohamia- hata hivyo baada ya muda mfupi wote walirudi na kuhusu hilo, amesema; “Walinishangaza sana,”.
    Lakini Moloto alimzungumzia zaidi Mgosi akisema ni mchezaji mzuri mno na anageweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa Afrika Kusini kama angebaki.
    Wachezaji wote walirejea Simba SC kabla ya kuachwa kwa misimu tofauti na Mgosi sasa amesaini Mtibwa Sugar, wakati Costa inasemekana amerejea Msumbiji.     
    Kiwango cha PSL; Sure Boy kulia akifanya vitu jana

    Azam jana iliibwaga Mamelodi 1-0, bao pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba, huo ukiwa mchezo wa pili katika ziara yao ya nchini hapa kujiandaa na msimu baada ya Jumatatu kufungwa mabao 3-0 na Kaizer Chiefs.
    Katika mchezo wa jana, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na wenyeji ndiyo waliotawala zaidi mchezo kipindi hicho, ingawa Azam walifanikiwa kutengeneza nafasi nzuri zaidi ya kufunga.
    Nabii hakubaliki nyumbani; Bocco amewahi kufanya majaribio SuperSport United ya hapa akafuzu, lakini ikashindwana na Azam katika manunuzi. Pamoja na kukubalika sana hapa, mashabiki nyumbani hawamfagilii sana Adebayor Chamazi, kiasi kwamba hasikii raha kuchezea timu ya taifa, Taifa Stars.

    Khamis Mcha ‘Vialli’ aliingia vizuri ndani kutokea pembeni kulia hadi ndani ya eneo la hatari na akampa pasi ya ‘hapa kwa hapa’ John Bocco ‘Adebayor’ akiwa anatazamana na lango, lakini akapiga juu ya lango dakika ya 43.   
    Kipindi cha pili Azam waliingia kwa ari mpya na kufanikiwa kuuteka mchezo hali ambayo ilisababisha wafanye mashambulizi mengi langoni mwa Mamelodi.
    Almanusra Bocco afunge dakika ya 65 kama si kichwa chake kupaa juu ya lango kufuatia krosi maridadi ya Kipre Herman Tchetche kutoka kushoto.
    Mfungaji bora; Kipre Tchetche ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara kwa sasa

    Mamelodi walijibu shambulizi hilo dakika ya 70 na shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 19 lililopigwa na Jabu Shongwe liligonga nguzo ya juu ya lango na kurejea uwanjani kabla ya Said Morad ‘Mweda’ kuondosha kwenye hatari. 
    Katika dakika ya 74, Mwaikimba aliyeingia uwanjani dakika ya 64 kumpokea Bocco aliunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya beki Joackins Atudo kutoka wingi ya kulia, ambaye pia alitokea benchi kipindi cha pili kuipatia Azam bao pekee kwenye mchezo huo.
    Dakika ya 89 Mwaikimba alikaribia tena kufunga kama si shuti lake kupaa juu ya lango akiwa ndani ya eneo la hatari kufuatia krosi nzuri ya Tchetche kutoka kushoto.
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall alifurahia matokeo na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na pia akasifu ushindani ulioonyeshwa na wapinzani. 
    Mshindi wa mechi; Mwaikimba alifunga bao pekee la ushindi jana. Hapa anapongezwa na Seif Abdallah.

    Kwa upande wake, Pitso Masomane kocha wa Mamelodi alisifu Azam na akasema kwa soka waliyoonyesha hastaajabu kwa nini wameshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Tanzania.  
    Azam iliyofikia katika hoteli ya Randburg Towers mjini hapa, leo imeendelea na mazoezi asubuhi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Wits mjini hapa na itashuka tena dimbani keshokutwa huko Soweto kumenyana na Orlando Pirates.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SURE BOY, KIPRE TCHETCHE NA BOCCO WAMTOA UDENDA MOLOTO, ASEMA VIJANA WANAWEZA KAZI PSL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top