IMEWEKWA SEPTEMBA 8, 2013 SAA 4:17 ASUBUHI
MGOGORO unanukia Yanga SC. Unanukia kwa sababu ya msuguano unaoendelea katika klabu hiyo, baina ya Wazee wa klabu hiyo na uongozi, yaani Kamati ya Utendaji.
Uongozi katika kutekeleza wajibu wake wa kuiletea maendeleo klabu, upo katika mchakato wa kuboresha Sekretarieti kwa kuajiri wataalamu wa kiwango cha juu kwa ajili ya shughuli za Utendaji za klabu na Wazee wanaonekana kutotaka mgeni aajiriwe katika klabu hiyo.
Baada ya mmoja wa wawania ajira katika Sekretareti ya Yanga SC kufika makao makuu ya klabu, Wazee walimbana kwa maswali na hatimaye kumfukuza. Huyo ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya (FKL), Patrick Nyaggi ambaye ni mwanasoka na kocha wa zamani nchini Kenya.
Hoja kuu ya Wazee kukataa mgeni ni kwamba, shughuli za klabu yao zinapaswa kufanywa na wanachama wa klabu hiyo- hivyo wanaamini mgeni hatakuwa mwanachama na hawamtaki. Nilisikiliza maoni ya Wazee, kwa kweli kwa maono yao hakuna wanapokosea, ila ukienda kwenye hali halisi ya uendeshwaji wa klabu kisasa na wakati tulionao na kama kweli wanataka mabadiliko ndani ya Yanga SC, lazima wabadilishe fikra zao.
Sisi wa vyombo vya habari ndio tumekuwa mstari wa mbele kuzikandia hizi klabu kwa kutobadilika miaka nenda, rudi kiasi cha kuzidiwa na klabu zinazokuja karibuni mfano Azam FC.
Nimewahi kutoa mfano, Yanga SC haina tofauti na Barcelona ya Hispania, zote ni timu za wanachama, tofauti ni mifumo ya uendeshwaji tu. Na kwa sababu hiyo, ipo haja ya kuutazama mara mbili mfumo wa uendeshwaji wa Yanga SC kama kweli ipo siku utaleta mabadiliko katika klabu hiyo.
Nasi wa vyombo vya habari tuna wajibu kabisa wa kuunga mkono jitihada zozote za maendeleo ndani ya Yanga na kuwaelimisha wale ambao tunaamini wanaweza kuwa kikwazo. Niende mbali zaidi, ugumu wa uelewa wa wanachama wachache wa Yanga ni jambo ambalo linafahamika dhahiri na ingekuwa vyema basi uongozi kabla ya kuingia kwenye mchakato huu, ukawaita hao wanachama na kuwaelewesha unataka kufanya nini na kwa sababu gani.
Nawaheshimu sana wale wanachama ambao kila kukicha wapo pale makao makuu ya klabu na siku zote wamekuwa wakifanya shughuli za klabu hiyo- ingawa watu wengine wanawashangaa kwa nini hawafanyi shughuli zao na kubaki kugandana na klabu tu muda wote.
Naona watu kama wale lazima wawepo na kuna umuhimu wa kuwepo, kwa sababu wana Yanga wote wangeamua kufanya shughuli zao na kutokuwa karibu na timu yao, sidhani kama ingekuwa sahihi. Lazima kuwepo na watu wanaojua mambo ya kila siku kuhusu klabu na idadi iliyopo pale Yanga si mbaya kwa kweli.
Kama tunaamini kuwepo kwao pale wananufaika katika njia zisizo rasmi, basi hakuna sababu ya kutoleana kashfa, bali kutafuta namna iliyo rasmi juu ya maslahi yao. Pamoja na yote umuhimu wa mabadiliko unabaki pale pale.
Nilimsikiliza kwa makini, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akijibu hoja za wazee wa klabu hiyo kupinga kuajiriwa kwa Mkenya, Patrick Naggi kwamba si mwanachama wa klabu hiyo kwa kusema watu wengi wameajiriwa na klabu hiyo wakiwa si wanachama na kupewa uanachama baadaye.
Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam Ijumaa, Sanga alisema kwamba pia ni vigumu kutambua kwa haraka nani ni mwanachama na nani si mwanachama kwa kuwa klabu imetoa kadi nyingi za uanachama katika siku za karibuni na nyingi amezisaini yeye mwenyewe.
Sanga amemtolea mfano kocha Mkuu wa klabu, Mholanzi Ernie Brandts aliajiriwa akiwa si mwanachama na akapewa uanachama baadaye.
Pamoja na hayo, Sanga amekanusha habari kwamba Yanga imekwishamuajiri Ofisa huyo Mtendaji Mkuu wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya (FKL) na kusema kwamba mchakato huo bado unaendelea na watu wengi wamejitokeza.
Sanga amesistiza nia ya Kamati ya Utendaji kutaka kuboresha Sekretarieti ya klabu kwa kuwa hayo ni maazimio yao katika kuiboresha klabu kwa ujumla iwe na mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja.
Kuhusu mustakabali wa aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako, Sanga alisema naye yumo katika mchakato wa wanaoomba ajira Yanga na hatima yake itategemeana na matokeo ya mchakato huo, unaoendeshwa na kampuni waliyoipa tenda.
“Moja ya maazimio makubwa ambayo klabu ya Yanga sisi kama viongozi tulikubaliana, ni kuona kwamba tunaiboresha Sekretarieti yetu na kuona kwamba inaendana na uboreshaji wa timu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunakuwa na mafanikio ya ndani na nje ya Uwanja,”.
“Na kwa hali hiyo, tulikubaliana katika Kamati ya Utendaji kwamba kuna nafasi kadhaa katika klabu yetu zinatakiwa kuimarishwa, ikiwemo ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mkurugenzi wa Fedha, na kwa ujumla Sekretarieti nzima kwa ajili ya kuifanya iwe katika ubora unaostahili,”.
Sanga alisema kwamba waliona ingekuwa vigumu kwa zile nafasi kutangazwa kwenye magazeti na Kamati ya Utendaji ikaona njia nzuri ni kutafuta kampuni ya uwakala kwa ajili ya kutafuta wafanyakazi, iendeshe mchakato huo kwa ajili ya Yanga.
“Kwa hiyo kuna kampuni ambayo tuliingia nayo makubaliano, kututafutia wafanyakazi wa klabu ya Yanga ambayo ilianza mchakato wa kutuletea watu mbalimbali. Lakini labda niseme, kitu kimoja kilichokuwa kimejitoeza zaidi ni kwamba tukiwa ndani ya mchakato huo, mmoja wa watu ambao walikuwa wanawania nafasi mojawapo (Naggi) ilijitokeza kwamba alifika klabu,”.
“Na tukapata taarifa alipofika kulikuwa kuna mahojiano na watu wa hapa (klabuni) kuweza kujua uhalali wake wa kufika hapa, jambo hilo sisi wengine hatukuwepo kwa hivyo hatujui nini kilichojiri, hali ambayo ilisababisha taarifa mbalimbali kutolewa na vyombo vya habari,”.
“Lakini mimi nimesimama hapa kwa niaba ya Kamati ya Utendaji kusema kwamba watu wengi wamejitokeza na mchakato haujakamilika, umefikia kwenye hatua mbalimbali. Kwa bahati mbaya tu imepokelewa vibaya na tofauti na kutangazwa kwamba tayari Yanga imekwishampata mtu fulani, jambo ambalo halikuwa sahihi,”alisema.
Kwa maelezo ya Sanga unaweza kuona wazi nini kinanukia Yanga SC kutokana na msimamo wa Wazee- lakini sisi wa vyombo vya habari tunalipokeaje suala hili na tunasimamia upande gani katika kuhakikisha mambo yanakwenda sawa pale Jangwani?
Vyombo vya habari vimekuwa vikiimba mabadiliko katika hizi klabu (pamoja na Simba) na kila siku kutolea mifano timu kama TP Mazembe ya DRC yenye mafanikio ndani na nje ya Uwanja, lakini kama havitaunga mkono michakato ya mabadiliko, ndoto hizo zitatimia saa ngapi?
Lazima wanachama wa Yanga waelimishwe, Usimba na Uyanga unaishia ndani ya mipaka ya Tanzania- unapotoka nje kule hakuna Usimba wala Uyanga, hivyo kutumia itikadi za Usimba na Uyanga kuzuia kuajiriwa mtaalamu mgeni, bila kuzingatia ataisaidia klabu kwa kiasi gani si sahihi.
Muingereza Peter Kenyon amefanya kazi katika klabu mbili kubwa pale England, akianza na Manchester United na kwa utendaji wake mzuri na mafanikio aliyozalisha Old Trafford, bilionea Mrusi, Roman Abramovich alipoinunua Chelsea akamchukua na kuamuajiri Stamford Bridge ambako huwezi kuuliza, anafanya nini- kwa kuwa The Blues sasa ni timu kubwa Ulaya na duniani tofauti na ilivyokuwa awali.
Tanzania ipo katika kipindi cha marekebisho ili iwe na uchumi wa kati na kwa sababu hiyo, si wana Yanga tu, bali Watanzania wote hivi sasa wanatakiwa wawe na fikra za kukimbia badala ya kutembea.
Natambua tuna tamaduni, zetu mila na desturi, lakini nchi imebeba falsafa ya ‘Big results now’ (matokeo makubwa sasa) na Yanga wanatakiwa kuwa na matokeo makubwa, ambayo bila mabadiliko hayatapatikana. Niishie hapa. Wasalam, Bin Zubeiry.

.png)