• HABARI MPYA

    Wednesday, September 11, 2013

    KAMA MARADONA NA HENRY WANGEFUNGA MABAO HAYA TAIFA…

    IMEWEKWA SEPTEMBA 11, 2013 SAA 1:08 ASUBUHI
    KOMBE la Dunia, bila shaka ndio mashindano makubwa zaidi ya soka duniani- na unapozungumzia michuano hiyo moja kati ya kumbukumbu nyingi na za kihistoria ni bao la ‘Mkono wa Mungu’ alilofunga Diego Armando Maradona katika mchezo dhidi ya England mwaka 1986.
    Hilo lilikuwa bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 na Argentina ikatinga Fainali, ambako pia chini ya Unahodha wa Maradona, ilifanikiwa kuifunga Ujerumani na kutwaa Kombe. 

    Lakini bado watu wa kweli wa soka hawawezi kusahau Ufaransa ilipataje tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010. Ufaransa ilisotea tiketi ya fainali za michuano hiyo ya kwanza kufanyika Afrika baada ya kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Serbia na ikalazimika kucheza mechi mbili maalum dhidi ya Jamhuri ya Ireland kuwania tiketi ya ziada kuja Afrika. 
    Huku timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, katika mchezo wa marudiano, Thierry Henry alishiriki kuipatia Ufaransa bao la utata kwenye Uwanja wa Stade de France, Novemba 18 mwaka 2009 baada ya kutumia mkono wake mara mbili kuuweka sawa mpira kabla ya kumimina krosi iliyounganishwa kimiani na William Gallas kuifungia timu hiyo bao la ushindi lililowaleta Afrika.
    Kwa tukio hilo, watu walimkandia sana Henry ingawa kocha wake wa timu ya taifa wakati huo, Raymond Domenech na kocha wa klabu yake ya zamani, Arsenal, Arsene Wenger walimtetea. Chama cha Soka Ireland kilikata rufaa kikiomba mechi irudiwe, lakini FIFA, ilikataa.
    Henry mwenyewe aliamua kustaafu soka ya kimataifa baada ya tukio hilo, ingawa wakati huo alisema hakudanganya, lakini saa chache baada ya FIFA kuitupilia mbali rufaa ya Ireland, akasema; "Uamuzi wa haki ulikuwa ni mechi kurudiwa ".
    Unaweza kupata picha hapa katika matukio yote mawili, kwamba Argentina walibeba ‘Kombe haramu’ la Dunia mwaka 1986 na Ufaransa walipata ‘Tiketi haramu’ ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2010.
    Haya ni matukio makubwa ambayo unaweza kuyatolea mfano, lakini mara ngapi wachezaji wanafanya makosa yenye kustahili kadi nyekundu na dhabu zaidi, ila wananusurika, au mara ngapi wachezaji wanapewa kadi na adhabu wasizostahili kwa makosa tu ya marefa?
    Bado hii haihalalishi uvunjaji wa amani viwanjani. Bado hii hairuhusu umwagaji damu viwanjani. FIFA imepiga hatua kubwa sana hadi kuamua kutumia teknolojia kwenye mchezo huu, ili kuwasaidia binadamu wenzetu, marefa- lengo tu kujaribu kupunguza makosa yanayoweza kuepukika.
    Na jitihada zote hizi lengo la FIFA ni kutilia mkazo kwamba soka ni mchezo wa kiungwana, ingawa ajabu kwetu, bodi yenye mamlaka ya kusimamia mchezo huo inaonekana bado kutoupokea msimamo huo wa FIFA kwamba mpira wa miguu ni mchezo wa kiungwana.
    FIFA inapambana sana, hadi kwenye matumizi mabaya ya fedha katika usajili wanaamini inaondoa maana halisi ya uungwana katika mchezo wao na kuhamia katika utwana.
    Vipi TFF, wanatambua jitihada hizi? Hakuna hakika. Jana, Kamati ya Ligi Kuu ya TFF ilitoa taarifa ya kuipiga faini ya Sh. Milioni 1, klabu ya Yanga, yaani Sh. 500,000 kwa kila kosa kutokana na washabiki wake kuwarushia waamuzi chupa za maji baada ya Coastal Union kusawazisha bao katika mechi baina ya timu hizo na kuwarushia chupa waamuzi wa mechi hiyo wakati wakirejea vyumbani baada ya pambano hilo.
    Lakini taarifa za vyombo vya habari baada ya mechi, zilisema mashabiki wa Yanga walipiga mawe basi la Coastal na kumjeruhi mmoja wa wachezaji wa timu hiyo. Huko Kamati haikugusia kabisa, bali ilimpiga faini ya Sh. Milioni 1 na kumfungia miezi mitatu kocha wa makipa wa timu ya Coastal Union, Juma Pondamali kwa kuwatukana mashabiki wanaominika kuwa wa Simba.
    Pamoja na hayo, refa Martin Saanya na msaidizi wake namba moja, Jesse Erasmo waliochezesha mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya 1-1, nao wamefungiwa mwaka mmoja kila mmoja kwa kutoimudu mechi hiyo, huku Coastal Union ikipigwa faini ya Sh. 100,000 baada ya kuchelewa kwa dakika 23 kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). 
    Swali la kujiuliza hapa, marefa waliofanya makosa hadi Argentina ikabeba Kombe haramu la Dunia mwaka 1986 na Ufaransa ikapata tiketi haramu ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2010 na hawa walioshindwa kumudu mechi ya Yanga na Coastal akina nani wamefanya makosa yenye kuonekana?
    Lakini FIFA iliyachukulia yote haya kama makosa ya kibinadamu na ndiyo maana imeendelea kupambana kupunguza makosa kwa kuleta sheria mpya hadi za kutumia teknolojia. Leo ukiwauliza watu wa Kamati ya Ligi juu ya sababu za kuadhibiwa kwa marefa hawa, unaweza kutajiwa makosa mawili matatu walioyofanya mchezoni, je kuna uhakika hayakuwa ya kibinadamu?
    Tatizo ni fikra na hisia zetu, kwamba marefa wanapokea hongo, basi hata wakifanya makosa ya kibinadamu, wanapewa adhabu kubwa, au wakati mwingine unazi tu wa watu ndani ya Kamati ndiyo unaleta yote haya. Lakini hiyo si mada yangu kwa leo, je kuna kosa gani hapa la kuruhusu umwagaji damu uwanjani? 
    Wiki mbili zilizopita mara tu baada ya mechi hiyo, niliandika kwamba; tahadhari ni bora kabla ya hatari na samaki mkunje angali mbichi. Nilikataa kuzungumzia malalamiko ya Yanga kuonewa na refa- na nikalaani kwa nguvu zangu zote vurugu walizofanya mashabiki wa timu hiyo na nikatoa, maoni yangu kwamba wakati umefika sasa TFF ichukue maamuzi magumu dhidi ya klabu hiyo, ili iwe fundisho.
    Kwani hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa Yanga kufanya fujo uwanjani na kusababisha uharibifu wa mali na hata kujeruhi na kwa ujumla kuhatarisha amani, kwa sabau wenye soka yao, FIFA wanauita mchezo wa kiungwana- hawataki uhuni hata kidogo na TFF kama wasimamizi wakuu wa soka nchini, wanapaswa kulizingatia hilo.
    Lakini tatizo kubwa, TFF wanashindwa kuchukua adhabu ambazo zitakuwa fundisho kwa mashabiki wa Yanga na wengine wote, kwa sababu wameweka mbele fedha kuliko utu na thamani ya mchezo wenyewe.
    Ulikuwa wakati kwa Yanga kupewa adhabu ya kucheza mechi bila mashabiki uwanjani, japo tatu tu na bila shaka baada ya kukosa fedha, viongozi wake wataona umuhimu wa kuwasihi mashabiki wao wawe wastaarabu.
    Lakini kama tutaendelea na ile desturi ya faini Sh. 500,000 na kutakiwa kufidia gharama za uharibifu na tiba za waliojeruhiwa, hakika iko siku litakuja kutokea kubwa kutokana na mashabiki hawa wa Yanga.
    Nilikumbushia mechi ya Machi 31, 2002 wakati Simba SC inaifunga Yanga 4-1 katika Fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la Tusker, mabao ya Mark Sirengo dakika ya tatu na 76, Madaraka Selemani dakika ya 32 na Emanuel Gabriel dakika 83 upande wa Simba na Sekilojo Chambua wa Yanga dakika ya 16.
    Mbele ya mgeni rasmi, rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu mechi hiyo ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa aweze kupiga. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa na mashabiki wa Yanga. 
    Refa wa mchezo huo, Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. 
    Baada ya hapo, adhabu waliyopewa Yanga ni faini na Tarimba alifungiwa kwa sababu alionekana chanzo cha vurugu zilizotokea. Lakini Yanga wamerudia, na wameendelea tena kuhatarisha amani viwanjani, na unaweza kuona wazi kwa adhabu wanazopewa, hawataacha na wataendelea.
    Wazi, kama tunataka kuivusha soka yetu katika hatua nyingine, lazima kwanza tukubali kujivua ushabiki na kuchukua hatua ambazo moja kwa moja zitalenga maslahi na ustawi wa mchezo huu nchini. 
    Nasistiza, wakati umefika sasa, tuondoe dhana kwamba Yanga chini ya utawala Leodegar Tenga na Athumani Nyamlani haiwezi kuchukuliwa hatua kali hata ikifanya kosa kubwa kiasi gani, kwa sababu viongozi wote hao wawili ni Yanga wazuri. Si sahihi.
    Tunakumbuka, wakati fulani mashabiki wa Ashanti walifanya vurugu katika mechi dhidi ya Yanga SC na wakafungiwa kucheza Uwanja wa Taifa. Lakini ni mara ngapi Yanga wamefanya vurugu na wamechukuliwa hatua kama hiyo angalau, au ilionewa Ashanti tu?  
    Ndiyo, Ashanti haina mashabiki wa kuingiza hata Milioni 1 na mchezo mmoja wa Ligi Kuu wa Yanga wenye kiwango kidogo kabisa cha fedha ni Sh. Milioni 40, sasa bila shaka hili nalo linachangia kwa kiasi kikubwa, lakini kwa nini tuweke fedha mbele kuliko utu na thamani ya mchezo wenyewe? Tutambue, tusipoziba ufa, tutajenga ukuta siku moja. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KAMA MARADONA NA HENRY WANGEFUNGA MABAO HAYA TAIFA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top