• HABARI MPYA

    Saturday, September 07, 2013

    MIEMBENI YACHARAZWA 1-0 LIGI KUU ZANZIBAR

    Na Nurat Mahmoud, Zanzibar, IMEWEKWA SEPTEMBA 7, 2013 SAA 3:37 USIKU
    TIMU ya Mtende Rangers, leo imeidhihirishia Miembeni SC kwamba mchezo wa soka hauchezwi kwa mdomo baadaya kuwatandika bao 1-0 katika mfululizo wa michuano ya ligi kuu ya Zanzibar Grand Malt inayoendelea kwenye uwanja wa Mao Tsetubg Unguja na Gombani Pemba.
    Pambao hilo lilikuwa kali na lenye upinzani mkubwa huku likitawaliwa rafu za hapa na pale, ambapo vijana wa Mtende kutoka Wilaya ya Kusini walianza kwa kulishambulia lango la wapinzani wao mfululizo katika dakika za kwanza.
    Miembeni imepigwa 2-0 na Mtende leo

    Mashambulizi hayo yalizaa matunda katika dakika ya nane baada ya mchezaji wa Miembeni Salum Juma kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari katika harakati za kuokoa, na mwamuzi Makame Haji Mpoma akaizawadia Mtende mkwaju wa penalti.
    Mchezaji Ali Juma alipiga vyema mkwaju huo na kuipatia timu yake ya Mtende bao hilo pekee.
    Mbali na kufungwa Miembeni pia ilipata pigo katika dakika la kwanza za mchezo baada ya mchezaji wake wa kutumainiwa Amour Omar Janja, kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Salum Awesu katika dakika ya sita.
    Pamoja na hali hiyo, Miembeni al maaruf Kwala, hawakukata tamaa na wakajipanga upya na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa walima viazi hao kwa lengo la kutafuta bao lakini ukuta wa vijana wa Mtende uliokaa imara kuzuwia hatari zote zilizoelekezwa langoni kwao.
    Kipindi cha pili kilianza kwa kila upande kuongeza nguvu kwa kufanya mabadiliko na kuingiza wachezaji kadhaa lakini bado matokeo yalibaki kama yalivyo.
    Hata hivyo mchezo huo uliingia dosari na kulazimika kusimama kwa dakika kadhaa mnamo dakika ya 52, baada ya mwamuzi wa kati Makame Haji Mpoma kuumia bega baada ya kugongana na mchezaji wa Miembeni Mohammed Salum, katika purukushani za mtanange huo.
    Mpoma alishindwa kuendelea na mchezo na kukimbizwa hospitali kwa matibabu na nafasi yake kuchukuliwa na mwamuzi wa akiba Issa Haji.
    Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja katika uwanja wa Mao Tsetung, ambapo mabingwa watetezi wa ligi hiyo KMKM baada ya kujipima na Simba juzi na kufungwa mabao 2-1 jijini Dar es Salaam, wataanza kutetea taji lao kwa kuvaana na maafande wenzao timu ya Zimamoto.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MIEMBENI YACHARAZWA 1-0 LIGI KUU ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top