• HABARI MPYA

    Saturday, April 18, 2015

    VIBABU VIWILI VYA RIKA MOJA VINAVYOZIPAMBANISHA YANGA NA ETOILE LEO TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    VIBABU viwili vyenye umri wa miaka zaidi ya 60, leo vitakuwa kwenye mabenchi mawili tofauti kuziongoza timu zao zikimenyana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Babu wa Kiarabu, Faouzi Benzarti atakuwa kwenye benchi la Etoile du Sahel ya Tunisia, akipambanisha timu yake hiyo na wenyeji, Yanga SC walio chini ya babu wa Kizungu, Hans van der Pluijm.
    ‘Vibabu’ vyote hivi, vichezaji vya zamani vina uzoefu mkubwa na soka ya Afrika na leo vinakutana katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika. 

    Faouzi Benzarti atakuwa kwenye benchi la Etoile du Sahel ya Tunisia leo dhidi ya wenyeji, Yanga SC

    FAOUZI BENZARTI NI NANI?
    Faouzi Benzarti aliyezaliwa Januari 3, mwaka 1950 mjini Monastir, ni mwanasoka wa zamani nchini Tunisa, ambaye kwa sasa ni kocha mkubwa. Mdogo wake, Lotfi Benzarti pia ni kocha.
    Faouzi Benzarti ni kocha mzoefu ambaye amefundisha timu kibao Tunisia, akianza na Etoile du Sahel kati ya 1986–1987 mara tu baada ya kustaafu soka klabu US Monastir aliyoichezea kati ya 1979 na 1982. 
    Kutoka Etoile, akachukuliwa na Club Africain mwaka 1989 hadi 1990, kabla ya kurejea Etoile mwaka 1991 hadi 1992 akarejea US Monastir hadi 1993 alipohamia Esperance ya Tunis.
    Mwaka 1994 alifundisha timu ya taia ya Tunisia hadi 1995 alipohamia CS Sfaxien, aliyofundisha hadi 1999 aliporejea Club Africain, alikopiga kazi hadi 2002 akahamia Stade Tunisien hadi 2003 akarejea Esperance alikofundisha hadi 2005 akarejea US Monastir.
    Mwaka 2006 alirejea Etoile hadi 2007 akarejea tena Esperance, ambako hakudumu akaenda kufundisha timu ya taifa ya Libya. 
    Mkataba wake na Libya ulimalizika mwaka 2009 akajiunga na timu ya taifa ya Tunisia miezi kadhaa baadaye. Pia aliifundisha Tunisia katika Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2010 nchini Angola.
    Mei 17 mwwaka 2011, Benzarti alisaini Mkataba wa miaka miwili kuifundisha Club Africain kwa mara ya tatu, wiki moja baada ya klabu hiyo kumfukuza kocha wake, Kais Yacoubi.
    Machi 26, mwaka 2012, Faouzi Benzarti akachukua nafasi ya Bernd Krauss Etoile, kocha huyo ‘Mtanga na Njia’ akirejea mjini Sousse kwa mara ya nne, huku Mjerumani Bernd Krauss akirejeshwa katika nafasi yake ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Soka ya Vijana. Krauss kwa sasa mi kocha wa Raja Casablancan yan Morocco.
    Mwaka 2012 Benzarti alihamia Al-Shabab alikofanya kazi hadi 2013 akarejea Club Africain alikofundisha kwa muda kabla ya kwenda Raja Casablanca na ni mwaka huu amereja Etoile du Sahel.
    Babu huyo wa umri wa miaka 65 hakika ana uzoefu wa kutosha na soka ya Afrika.  

    Hans van der Pluijm ataiongoza Yanga SC dhidi ya Etoile leo

    HANS VAN DER PLUIJM NI NANI?
    Hans van der Pluijm aliyezaliwa Januari 3, mwaka 1949 ni kocha wa Kiholanzi na kipa wa zamani nchini humo, ambaye amechezea FC Den Bosch kuanzia mwaka 1967 hadi 1986. 
    Baada ya kutungika glavu zake akawa kocha wa Den Bosch hadi mwaka 1995. Baada ya hapo, akaenda kufundisha kwa msimu mmoja SBV Excelsior kabla ya kuhamia Ghana mwaka 1999.
    Mafanikio yake makubwa akiwa kocha ni kucheza Fainali ya Kombe la Uholanzi mwaka 1991, ambayo Den Bosch ilifungwa 1-0.
    Pluijm aliyeidakia mechi 338 FC Den Bosch kuanzia
    1967 hadi 1986, alitua Yanga SC kwa mara ya kwanza Januari mwaka 14 mwaka 2014 na Juni 14, mwaka huo akaondoka kwenda Al Shoalah FC ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
    Alikwenda huko na aliyekuwa Msaidizi wak Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa- lakini baada ya miezi kadhaa, wawili hao waliacha kazi Uarabuni na Desemba mwaka huu wakarejea Yanga SC. 
    Kabla ya hapo, akiwa nchini Ghana, Pluijm alifundisha timu za Ashanti Gold SC kuazia Julai 1, mwaka 2000 hadi Juni 30, mwaka 2002, Heart of Lions Kpando kuanzia Julai 1, mwaka 2002 hadi Julai 20, mwaka 2003. 
    Akarejea Ashanti Gold SC kuanzia Julai 1, mwaka 2004 hadi Oktoba 5, mwaka 2005, akarejea Heart of Lions Kpando kuanzia Julai 1, 2010 hadi Septemba 20, mwaka huo, akahamia Berekum Chelsea kuanzia Novemba 1, 2011 hadi Julai 16, mwaka 2013.
    Julai 16, mwaka 2013 akahamia Medeama SC hadi Oktoba 24, mwaka huo, kabla ya kutua Yanga SC mwaka jana.
    Pluijm  amekubalika mno Yanga SC, hasa baada yaa mwaka jana kuingoza timu hiyo kwa mara ya kwanza kupata ushindi dhidi ya timu ya Kaskazini mwa Afrika.
    Yanga SC iliifunga 1-0 Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ingawa ilikwenda kutolewa kwa mikwaju ya penalri, baada ya kufungwa nayo 1-0 katika mchezo wa marudiano.
    Yanga wana imani sana na babu wa Kiholanzi Pluijm, mwenye umri wa miaka 66 na wanatarajia matokeo mazuri leo dhidi ya Etoile. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIBABU VIWILI VYA RIKA MOJA VINAVYOZIPAMBANISHA YANGA NA ETOILE LEO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top