• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2012

    BAHANUZI, YONDAN HAWAPO KESHO YANGA NA RUVU

    Bahanuzi

    Na Mahmoud Zubeiry
    BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi wataendelea kuwa nje ya Uwanja mwishoni mwa wiki, wakati timu yao, Yanga SC itakapokuwa ikiwania pointi tatu katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na hali zao kutoimarika.
    Wawili hao ambao ni majeruhi, wapo kwenye programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna mmoja kati yao aliyekuwa tayari kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
    Maana yake, Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika safu ya ushambuliaji.
    ‘Dogo’ Simon Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika mechi dhidi ya Simba na Hamisi Kiiza amerejea kutoka Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
    Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
    Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
    Simba iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BAHANUZI, YONDAN HAWAPO KESHO YANGA NA RUVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top