• HABARI MPYA

    Tuesday, October 02, 2012

    KASEJA NA MECHI 24 ZA WATANI, NANI KAMA YEYE?

    Kaseja kinara wa mechi za watani

    Na Mahmoud Zubeiry
    KAMA kesho atasimama kwenye milingoti mitatu, Juma Kaseja atatimiza mechi 25 za wapinzani wa jadi katika soka ya Tanzania kucheza, tangu ajiunge na Simba mwaka 2003, kati ya hizo moja tu, akiidakia Yanga mwaka 2009.
    Kama itakumbukwa Kaseja, alisajiliwa Simba mwishoni mwa mwaka 2002, akitokea Moro United na moja kwa moja akaachiwa mikoba na aliyekuwa Simba One, Mwameja Mohamed.
    Kwa kuwa Mwameja alikuwa Tanzania One pia, haikuchukua muda, Kaseja naye akawa Tanzania One, akirithi mikoba ya Manyika Peter, aliyekuwa kipa wa Yanga. Makipa wote hawa watatu, Mwameja, Manyika na Kaseja walikuwa mahiri wa kuokoa mikwaju ya penalti.
    Mechi ya kwanza ya watani Kaseja kucheza ilikuwa Aprili 20, mwaka 2003 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambayo Yanga ilishinda 3-0, mabao yake yakifungwa na Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
    Hii ilikuwa mechi maalum ya kirafiki, iliyoandaliwa na promota Dika Sharp kwa kushirikiana na Prime Time Promotions, ambayo ilipewa jina ‘Big Match’
    Mechi ya pili ikafuatia Septemba 28, mwaka 2003, katika Ligi Kuu ambayo iliisha kwa sare ya 2-2, mabao ya Simba yakifungwa na Emmanuel Gabriel dakika ya 27 na 36, wakati ya Yanga yalifungwa na Kudra Omary dakika ya 42 na Heri Morris dakika ya 55.
    Mechi ya tatu ilikuja Novemba 2, mwaka 2003 ya Ligi Kuu, marudiano ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana.
    Mechi ya nne iliikuja Agosti 7, mwaka 2004, ilikuwa ya Ligi Kuu pia, Simba ikashinda 2-1, mabao ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ dakika ya 64 na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 76, wakati la Yanga lilifungwa na Pitchou Kongo dakika ya 48.
    Mechi ya tano ilikuja Septemba 18, mwaka 2004 ya Ligi Kuu pia, bao pekee la Athumani Machuppa dakika ya 82, likiipa ushindi Simba.
    Mechi ya sita ilikuja Aprili 17, 2005 na Simba ikashinda tena 2-1, Ligi Kuu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, mabao yake yakifungwa na Nurdin Msiga dakika ya 44 na Athumani Machupa dakika ya 64, baada ya Aaron Nyanda kutangulia kuifungia Yanga dakika ya 39.
    Mechi ya saba, ilikuja Julai 2, mwaka 2005 ya fainali ya Kombe la Tusker, ilichezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Yanga ikalala 2-0, mabao ya Emmanuel Gabriel dakika ya 60 na Mussa Hassan Mgosi dakika ya 72.
    Mechi ya nane ilikuja Agosti 21, mwaka 2005 ya Ligi Kuu, ambayo Simba ilishinda 2-0, mabao yote yakitiwa kimiani na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nico Nyagawa katika dakika za 22 na 56 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Mechi ya tisa ilikuja Machi 26, mwaka 2006 ya Ligi Kuu, lakini hiyo iliisha kwa sare ya bila kufungana na mechi ya 10, ilikuja Agosti 15, mwaka 2006, Nusu Fainali ya Kombe la Tusker, ambayo iliisha kwa sare ya 1-1, Emanuel Gabriel akitangulia kuifungia Simba dakika ya 69 na Credo Mwaipopo akaisawazishia Yanga dakika ya 90. Simba ikashinda kwa penalti 7-6.
    Mechi ya 11 ilikuja Oktoba 29, mwaka 2006, Ligi Kuu ambayo iliisha kwa sare tasa, yaani 0-0 na mechi ya 12 ilikuja Julai 8, mwaka 2007, Fainali ya Ligi Ndogo, ambayo matokeo yalikuwa 1-1 ndani ya dakika 120, Moses Odhiambo akitangulia kuifungia Simba penalti dakika ya pili, kabla ya Said Maulid ‘SMG’ kusawazisha dakika ya 55 na Simba ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Mechi ya 13, ilikuja Oktoba 24, mwaka 2007, Ligi Kuu na ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na bao pekee la Ulimboka Mwakingwe, dakika ya 14, lilipa Simba ushindi. Mechi ya 14 ilikuja Aprili 27, ya Ligi Kuu pia, mwaka 2008, ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, wakati mechi ya 15, ilikuja Aprili 19, mwaka 2009, Juma Kaseja akiwa katika mkataba wa mwaka na Yanga.
    Aliidakia Yanga siku hiyo na mechi hiyo ya Ligi Kuu ikaisha kwa sare ya 2-2, mabao ya Simba yakifungwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ dakika ya 23 na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 62, wakati ya Yanga yalifungwa na Ben Mwalala dakika ya 48 na Jerry Tegete dakika ya 90.
    Mechi ya 16 ilikuja Oktoba 31, mwaka 2009, Kaseja akiwa tayari amerejea Simba SC na akaiongoza timu yake kipenzi kuilaza Yanga 1-0, bao pekee la Mussa Hassan Mgosi dakika ya 26 katika Ligi Kuu.
    Mechi ya 17, ilikuja Desemba 25, mwaka 2009, Nusu Fainali ya Kombe la Tusker na Yanga ilishinda 2-1, mabao ya Jerry Tegete dakika ya 67 na Shamte Ally dakika ya 120, wakati la Simba lilifungwa na Hillary ‘Ford’ Echesa dakika ya 78 kwa penalti.
    Mechi ya 18, ilikuja Aprili 18, mwaka 2010 na Yanga ilichapwa mabao 4-3, Ligi Kuu pia, mabao ya Simba yakifungwa na Uhuru Suleiman dakika ya tatu, Mussa Mgosi dakika ya 53 na 74 na Hillary Echesa dakika ya 90 na ushei, wakati ya wana Jangwani, yalifungwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 30, Jerry Tegete dakika ya 69 na 89.
    Mechi ya 19 ilikuja Oktoba 16, mwaka 2010, Ligi Kuu pia, Yanga ikishinda 1-0 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, bao pekee la Jerry Tegete dakika ya 70, wakati ya mechi ya 20 iliyokuja Machi 5, mwaka 2011, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Stefano Mwasyika akitangulia kuifungia Yanga kwa penalti dakika ya 59, kabla ya Mussa Mgosi kuisawazishia Simba dakika ya 73, ilikuwa ya Ligi Kuu pia.
    Mechi ya 21 ilikuja Julai 10, mwaka 2011, Yanga ilishinda 1-0, Fainali Kombe la Kagame, mfungaji Mghana Kenneth Asamoah dakika ya 108, wakati mechi ya 22 ilikuja Agosti 17, mwaka 2011, Simba ikishinda 2-0, mabao ya Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 15 na Felix Sunzu dakika ya 38 kwa penalti, kuwania Ngao Jamii.
    Mechi ya 23 ilikuja Oktoba 29, mwaka 2011 na Yanga ikashinda 1-0, bao pekee la Davies Mwape dakika ya 75, Ligi Kuu pia na mechi ya 24 na ya mwisho Kaseja kudaka hadi sasa katika mapambano ya watani ni ile ya 5-0.
    Mei 6, mwaka 2012, Ligi Kuu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabao ya Emmanuel Okwi dakika ya pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti dakika ya 67 na Patrick Mafisango (marehemu) kwa penalti pia dakika ya 72. Kesho akidaka, itakuwa mechi ya 25, nani kama Kaseja?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KASEJA NA MECHI 24 ZA WATANI, NANI KAMA YEYE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top