![]() |
Tegete kushoto akiwa na Kiiza |
Na Mahmoud Zubeiry
KUPANDA na kushuka kwa kiwango cha mwanasoka ni kawaida na
wengi wamepitia hali hiyo- Jerry Tegete akiwa miongoni mwao. Huu ni msimu wa
pili, Tegete amezimika, akiwa hatambi Yanga na hana nafasi hata timu ya taifa
japo ya Bara, Kilimanjaro Stars.
Vigumu kujua sababu za kushuka kwa kiwango cha Tegete, lakini
ukitulia na kufuatilia matukio yake ya siku za karibuni unaweza kubaini sababu.
Mkanganyiko wa mawazo- kitaalamu frustrations ndio kwa kiasi kikubwa ilimuondoa
mchezoni Tegete.
Itakumbukwa hadi misimu miwili iliyopita, Tegete alikuwa
mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na chaguo la kwanza kwenye
klabu yake, Yanga tena akiwa kipenzi cha wapenzi wa soka kuanzia klabu hadi
taifa.
Lakini ghafla mambo yakaanza kumbadilikia kuanzia Yanga,
ambako mashabiki walianza kumuona hafai wakidai anakosa sana mabao na timu ya
taifa akatemwa. Tegete alidhani labda kocha Mganda Sam Timbe alikuwa adui wa
kipaji chake, lakini hata baada ya kurejea Kostadin Papic, hakuna tofauti.
Awali, aliona kama anaonewa na akaanza kukata tamaa na hiyo
ikachangia zaidi kushusha kiwango chake, lakini baada ya kujiridhisha kiwango
chake kweli kimeshuka, Jerry alibadilika.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, Tegete amekuwa katika jitihada
nzito za mazoezi hali ambayo kwa sasa inawaridhisha hadi makocha wake, hususan
Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, ambaye kwa sasa anaiongoza timu wakati Mholanzi
Ernie Brandts akisubiri kukamilishiwa taratibu za kumuwezesha kufanya kazi
nchini.
Ni namna gani Tegete atawashika tena wapenzi wa Yanga? Ni
jinsi gani Tegete atarudisha heshima yake katika soka ya Tanzania- ili
kujitengenezea mazingira ya kurejeshwa timu ya taifa?
Jibu ni Oktoba 3, 2012- yaani leo, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kama atapewa nafasi kwenye kikosi kitakachomenyana na watani wa jadi,
Simba SC, Tegete anaweza kujiokoa au kujimaliza mwenyewe.
Tegete anafunga kwa kumpiga tobo kipa |
Atajiokoa kwa kucheza vizuri na kutimiza wajibu wake kama
mshambuliaji kufunga mabao. Atajimaliza iwapo ataboronga na kuzidi kuwakatisha
tamaa, wapenzi na wadau kwamba yeye basi tena.
Tegete ana uzoefu wa mechi za watani wa jadi, hadi sasa akiwa
amefunga mabao matano katika mechi za watani, tangu ajiunge na timu hiyo msimu
wa 2008/2009 akitokea sekondari ya Makongo na timu ya taifa ya vijana chini ya
umri wa miaka 20.
‘Bismillah’ Tegete anatikisa nyavu za Simba ilikuwa Aprili 19,
mwaka 2009 katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ya Bara, iliyoisha kwa sare ya
2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tegete alifunga bao ambalo liliinusuru Yanga kuzama kwenye
mchezo huo kwa 2-1.
Lilikuwa bao zuri na la utata dakika ya mwisho kabisa,
akiunganisha krosi ya Mkenya Michael Barasa kutoka wingi ya kulia, ilionekana
kama ameunganisha mpira nyavuni kwa kichwa, lakini kumbe alipiga mpira kwa
ngumi, kwa ujanja wa hali ya juu na si refa wala mashabiki waliobaini hadi
marudio ya Televisheni baadaye.
Awali kwenye mchezo huo, kiungo Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’
alitangulia kuifungia Simba dakika ya 23, kabla ya Mkenya, Ben Mwalala
kusawazisha dakika ya 48 na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kufunga la pili dakika
ya 62.
Tegete akatikisa nyavu za Simba kwa mara ya pili Desemba 25, mwaka
2009 katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker, Yanga ikishinda 2-1 kwenye
michuano ambayo pamoja na kuipa timu yake Kombe, ikiifunga Sofapaka ya Kenya 2-1
kwenye fainali, pia aliibuka mfungaji bpora.
Siku hiyo, Tegete aliwatungua Simba dakika ya 67 tu, lakini
kiungo Mkenya, Hillary ‘Ford’ Echesa akawasawazishia Wekundu wa Msimbazi dakika
ya 78 kwa penalti. Dakika 90 za mchezo ziliisha kwa sare ya 1-1 na mechi
ikahamia kwenye dakika 30 za nyongeza- na huko kiungo Shamte Ally Kilalile
akaifungia Yanga bao la ushindi, dakika ya mwisho kabisa Uwanja wa Taifa.
Tegete akawatungua tena mara mbili Aprili 18, mwaka 2010
katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, Yanga ikilala 4-3, dakika ya 69 na 89.
Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Suleiman Mwambungu dakika ya tatu, Mussa Hassan
Mgosi dakika ya 53 na 74 na Hillary Echesa dakika ya 90 na ushei, wakati bao
lingine la Yanga, lilifungwa na kiungo Athumani
Iddi Athumani ‘Chuji’dakika ya 30.
Tegete aliifunga Simba kwa mara ya mwisho Oktoba 16, mwaka
2010, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, dakika ya 70, Yanga ikishinda 1-0.
Siku hiyo, Yanga ilicheza soka mbovu, lakini nafasi pekee nzuri aliyoipata
kwenye mechi iliyochezwa katika viunga alivyokulia vya Kirumba mjini Mwanza,
Tegete aliitumia vizuri kwa kukwamisha mpira nyavuni.
Sasa ni miezi 24, yaani miaka miwili imepita Tegete hazijui
nyavu za Simba, vipi leo? Vipi kwa maana zote, atapewa nafasi na kama atapewa
atafunga?
Tegete anaweza kuwa mmoja wa wachezaji wanaowatia watu hamu
ya kwenda Uwanja wa Taifa, kushuhudia mpambano wa watani jadi, kwa shauku ya
kutaka kujua kama atapangwa na pia kama ataweza kufunga. Ndio, Yanga wanaye Said
Bahanuzi ‘Spider Man’, ila katika mechi za watani, Tegete simdharau hata
kidogo.
Tegete enzi zake...sasa hivi mambo kama haya nadra sana |
0 comments:
Post a Comment