• HABARI MPYA

    Thursday, October 18, 2012

    KIIZA DIEGO AREJEA KUONGEZA NGUVU YANGA

    Kiiza

    Na Mahmoud Zubeiry
    HAMISI Friday Kiiza maarufu Diego Milito, amerejea jana Dar es Salaam na leo anaingia kambini, Uplands Hotel, Changanyikeni kuungana na wenzake kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kiiza alikuwa Uganda, kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
    Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
    Pamoja na kuweka kambi Changanyikeni, lakini Yanga inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, anaendelea vizuri na mazoezi mepesi sawa na mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
    Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
    Simba iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIIZA DIEGO AREJEA KUONGEZA NGUVU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top