• HABARI MPYA

    Monday, October 15, 2012

    MILOVAN AMPA 100 OCHIENG

    Ochieng katika mechi ya juzi

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA wa Simba SC, Mserbia Profesa Milovan Cirkovick amesema kwamba amevutiwa na uwezo wa beki Mkenya, Paschal Ochieng katika mechi ya juzi dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bila kufungana, Milovan alisema kwamba amevutiwa mno na uwezo wa Ochieng na kwamba sasa anaweza kuendelea kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
    Lakini Milovan alisema hakuvutiwa kabisa na uchezaji wa mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Ghana.
    “Sikuvutiwa kabisa na Akuffo,”alisema Cirkovick ambaye pia alisikitika kuwakosa wachezaji wake watatu nyota, Mrisho Ngassa, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ambao ni wagonjwa na Okwi, aliyekwenda kuichezea timu ya taifa ya Uganda, dhidi ya Zambia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.
    Simba iliorejea Dar es Salaam jana na leo inatarajiwa kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Kagera Sugar Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake watatu iliyowakosa kwenye mechi ya juzi, Okwi, Ngassa na Redondo.
    Okwi anatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo, wakati Ngassa na Redondo tayari wamepona na leo wanaanza mazoezi na timu hiyo. 
    Mechi nyingine za Jumatano zitakuwa kati ya Prisons na Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Polisi Morogoro na JKT Ruvu Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mgambo JKT na Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na JKT Oljoro dhidi ya African Lyon Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
    Simba bado ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi saba pia. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MILOVAN AMPA 100 OCHIENG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top