• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2012

    NGASSA AAHIDI MAMBO YA HATARI SIMBA SC

    Mrisho Ngassa; Nipeni muda muone mambo ya hatari

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIUNGO Mrisho Khalfan Ngassa, amesema kwamba bado anaizoea taratibu staili ya uchezaji ya timu yake mpya, Simba SC na nafasi mpya anayopangwa kwa sasa na anaamini hadi Januari mwakani atakuwa ameizoea na kufanya ‘mambo ya hatari’.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Ngassa alisema kwamba Simba wanacheza mfumo tofauti na ambao ulikuwa unatumiwa na timu yake ya zamani, Azam FC hivyo anaendelea kujifunza na kuizoea.
    “Mchezaji unapoingia timu mpya, kawaida unakutana na mambo mengi mapya, inabidi sana ujifunze na kuzoea.  Unacheza na watu wapya, ambao inabidi ujifunze namna ya kucheza nao na kuzoeana nao,”alisema Ngassa.
    Ngassa alisema angalau anekutana na wachezaji ambao anacheza nao timu ya taifa, lakini safu ya ushambuliaji ya Simba inaundwa na wachezaji wengi wa kigeni kama Emmanuel Okwi, Daniel Akuffo na Felix Sunzu.
    “Inabidi sana nijifunze taratibu, hata hivyo najisifu kwamba naendelea vizuri na hadi kufika Januari hivi, nitakuwa nimekwishazoea na kufanya mambo ya hatari,”alisema Ngassa na kusistiza hajashuka kiwango, ni mazingira mapya tu.    
    Ngassa juzi alifunga bao lake la tatu tangu ajiunge na Simba Agosti mwaka huu, akitokea Azam FC wakati Simba ikilazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Kagera kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hiyo ikiwa sare ya pili mfululizo kwa Wekundu hao wa Msimbazi, baada ya Jumamosi pia kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union mjini Tanga.
    Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’ kutoka wingi ya kulia.
    Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa ni Simba walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’ zaidi.
    Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali lililowababatiza mabeki wa timu hiyo na kutinga nyavuni.
    Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia lango la Simba kupitia pembeni na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
    Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya kulishambulia lango la Simba na katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja, akiisawazishia Kagera.
    Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira ulinoga zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA AAHIDI MAMBO YA HATARI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top