• HABARI MPYA

    Monday, October 15, 2012

    YANGA WAINGIA KAMBINI CHANGANYIKENI LEO

    Said Bahanuzi

    Na Mahmoud Zubeiry
    KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam, inatarajiwa kuingia kambini leo kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga ambayo katika mechi yake ya mwisho iliifunga Toto Africa mabao 3-1 mjini Mwanza, itaweka kambi kwenye hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam uku ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Jijini.
    Yanga itaendelea kuwakosa mazoezini wachezaji wake wawili majeruhi, beki Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi. 
    Bahanuzi ‘Spider Man’ anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi leo kufuatia kuchanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Daktari wa Yanga, Sufiani Juma aliiambia BIN ZUBEIRY mwishoni mwa wiki kwamba, mfungaji huyo bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, anaendelea vizuri baada ya kuchanika nyama za paja la mguu wa kulia.
    “Lini haswa ataingia kwenye programu kamili ya mazoezi, itategemea na maendeleo yake atakapoanza mazoezi mepesi,”alisema Sufiani.
    Kuhusu beki Kevin Yondan aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kugongwa na Haruna Moshi ‘Boban’, Sufiani alisema naye anaendelea vizuri na wakati wowote wiki hii ataanza mazoezi mepesi.
    Zaidi ya hao, Sufiani alisema Yanga ina majeruhi mwingine mmoja tu, ambaye ni Salum Telela ambaye naye anaendelea vizuri.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
    Simba iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAINGIA KAMBINI CHANGANYIKENI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top