![]() |
Mafisango katika picha tofauti |
MWILI wa kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Mutesa
Mafisango ulitarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao mjini Kinshasa, Jamhuri ya
Kidemokrsaia ya Kongo (DRC).
Mafisango alifariki dunia kwa ajali ya gari, usiku wa
kuamkia Alhamisi, maeneo ya VETA, Dar es Salaam, akiwa anatoka disko, Club
Maisha na gari lake kuacha njia na kutumbukia mtaroni wakati akimkwepa dereva
wa pikipiki.
Kifo chake kimeacha pengo katika klabu yake, Simba SC na
timu yake ya taifa, Amavubi Stars. Hakuna anayekufa kwa taarifa, lakini kwa
kuwa Mafisango hakuugua bali ajali tu imechukua uhai wake, kifo chake ni aina
ya vifo vinavyoitwa vya ghafla.
Amefariki katika wakati ambao, klabu yake ilikuwa inatarajia
mengi kutoka kwake. Huyu alikuwa mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Simba na
hakuna kingine kilichokuwa kinamfanya awe tegemeo zaidi ya jitihada zake uwanjani.
Makala nyingi ziliandikwa kwa ajili yake mwezi uliopita
wakati aliposimamishwa na uongozi wa klabu yake kwa utovu wa nidhamu, kabla ya
kusamehewa siku moja baadaye kabla ya timu kwenda kurudiana na ES Setif ya
Algeria katika Kombe la Shirikisho.
Wachambuzi wa nyumbani waliandika wakisema, kweli nje ya Uwanja
Mafisango anaweza kuwa mtovu wa nidhamu, lakini uwanjani ni ‘habari nyingine’. Walimsifu
kwa soka yake na kuusihi uongozi wa Simba kutafuta namna ya kuendelea kuishi na
mchezaji huyo.
Huyu ni mchezaji ambaye amefunga mabao 11 katika Ligi Kuu
msimu huu, pamoja na kwamba katika kipindi hicho alisimamishwa mara mbili kwenye
klabu hiyo na kukosa mechi zisizopungua tano.
Huyu ni mchezaji wa nafasi ya kiungo, ambaye tena mara
nyingi hucheza kama kiungo mkabaji. Huyu ni mchezaji ambaye alikuja nchini kama
beki wa kushoto akisajiliwa na Azam FC mwaka juzi.
Azam FC ilimuacha aende Simba, baada ya kushindwa kuvumilia
utovu wake wa nidhamu. Na ni utovu upi wa nidhamu alikuwa nao Mafisango? Pombe.
Jamaa alikuwa anapenda pombe na kujirusha hivyo wakati mwingine kuingilia programu
za mazoezi za makocha.
Alikuwa anaweza akaenda kustarehe, kesho yake akachelewa
kuamka na kuchelewa mazoezini, jambo ambalo lilikuwa linawakera makocha kuanzia
Mganda Moses Basena aliyempokea Simba hadi sasa Mserbia, Milovan Cirkovick.
Lakini akishaomba radhi, Mafisango alikuwa mtu safi sana. Alikuwa
anaweza kumfanya mwalimu asahau yote anapokuwa uwanjani. Rage alisema huyo
alikuwa mchezaji wa kipekee, hakukosea- kwa kumlinganisha na wachezaji wengi wa
Tanzania, Patrick alikuwa wa kipekee mno.
Alikuwa anajituma mno uwanjani. Alikuwa mchezaji wa timu kwa
ajili ya ushindi. Anapopanda kutoka kwenye dimba dogo kwenda kwenye D ya
wapinzani kusaidia mashambulizi, akipoteza au mpira ukipotea alikuwa akirudi kwa
kasi na kwa mipango kuziba nafasi yake.
Alikuwa ana akili sana ya mpira. Hakuwa fundi sana, ila
alikuwa ana jitihada mno uwanjani.
Anapofanya kosa, ambalo kwa namna moja au nyingine anaweza
kuhisi amewaudhi mashabiki, Patrick alikuwa anahakikisha kabla ya kipyenga cha
mwisho mashabiki wamefurahi kwa ajili yake.
Mfano ni katika mechi ya kwanza na Al Ahly Shandy mjini Dar
es Salaam, Mafisango baada ya kukosa penalti, alipigana hadi akafunga. Alikuwa hata
akipoteza pasi, anahakikisha mpira unarudi tena kwenye himaya yao.
Alikuwa ni mchezaji ambaye kocha yeyote angependa kuwa naye
kwenye timu yake. Simba imepoteza mchezaji mmoja siyo tu mzuri, bali muhimu
kwenye kikosi chake. Felix Sunzu anaweza pia kuzungumza Kifaransa na Kilingala-
lakini bado Mafisango alikuwa ana faida za ziada ndani ya Simba SC.
Kila unapolitazama Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu
huu- kwa mabao yake 11, wazi Mafisango ana mchango mkubwa. Japokuwa, baada ya
kifo chake, Simba ilimtoa mchezaji wake Haruna Moshi ‘Boban’ na Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji, Kinesi wasindikize mwili wake DRC- lakini kwa soka yake
kama ingekuwa kusajiliwa ungekwenda Ujumbe mzito zaidi wa Simba kumfuata Kinshasa.
Basi tena, mwandamu ukishafumba macho watu wanasahau yote. Ilinipa
tabu kidogo kuelekewa, Mwenyekiei wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage, Makamu wake
Geoffrey Nyange ‘Kaburu kwa nini mmoja wao asiende na mwili wa marehemu DRC?
Ila, Rage alisafiri hadi Cerpe Verde kufuata ITC ya Gervais
Kago, kwa sababu alikuwa anataka mchezaji- Kaburu amekwishasafiri sana kufuata
wachezaji nchi za nje, lakini mwili wa marehemu aliyekuwa mpiganaji na mwenye
mchango mkubwa kwenye klabu, ilikuwa rahisi tu kuamua Boban na Kinesi waende.
Boban amekwenda na angekwenda tu, kwa sababu yule alikuwa
rafiki yake mkubwa- ila familia ya marehemu imeupokea mwili wa Mafisango kutoka
kwa Kinesi leo, Mjumbe tu wa Kamati ya Utendaji.
Si mada yangu hiyo leo. Nachotaka kuwaambia wachezaji wa
Tanzania, wamejifunza nini kutokana na Mafisango katika kipindi chake cha miaka
miwili ya kufanya kazi Tanzania?
Rais Jakaya Kikwete alisema wakati akitoa salamu zake za
rambirambi kwa Simba, kwamba mchezaji huyo amechangia maendeleo ya soka ya
Tanzania kwa kipindi kifupi cha kucheza nchini.
Hapewi sifa kwa sababu ni kawaida yetu kusifia wafu, lakini
takwimu zinasema alikuwa hodari kweli. Pasi ngapi za mabao, mabao mangapi
amefunga msimu huu akiwa Simba pamoja na kwamba alisimamishwa mara mbili kwa
utovu wa nidhamu?
Wale waliopata fursa ya kucheza msimu mzima watazame
wamezifanyia nini klabu zao? Lakini walikuwa wanamuona Mafisango uwanjani
anavyocheza, anavyojituma uwanjani- hili ni somo gani kwao?
Juma Seif ‘Kijiko’, alikuwa kiungo wa ulinzi wa Yanga siku
Mafisango akiiongoza Simba kushinda 2-0 na kuteuliwa mchezaji bora wa mechi ya
Ngao ya Jamii Agosti mwaka jana- amejifunza nini?
Si Kijiko tu, hata wachezaji wa Simba, akiwemo Boban mwenyewe
ambaye mara nyingi anapopoteza mipira hutembea, wamejifiunza nini kwa Mafisango?
Tumlilie Mafisango huku pia tukijifunza kutoka kwake. Hii ni kwa wachezaji wote
nchi nzima.
Kama ana dhambi, namuombea ahueni mbele ya Mwenyezi Mungu
Mafisango. Amuepushe na adhabu za kaburi na ampumzishe kwa amani. Amin.
0 comments:
Post a Comment