TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilipigana
kiume katika mchezo wa kwanza wa Kundi C ugenini wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali
za Kombe la Dunia mwaka 2014 dhidi ya wenyeji Ivory Coast, ikifungwa mabao 2-0
kwa taabu.
Nasema kwa tabu, kwa sababu bao la pili la Ivory Coast
lililofungwa na Nahodha wao, Didier Drogba, lilipatikana dakika 10 baada ya
beki wa Stars, Aggrey Morris kutolewa nje kwa kadi nyekundu, zikiwa zimebaki
dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika.
Lakini pia mechi kama hizi zina mahesabu yake na mavuno zaidi
huwa ni kwenye mechi za nyumbani, wakati ugenini matokeo mazuri ni sare au
ukimkuta mwenyeji amechoka unamachapa, lakini bado pointi za nyumbani ndio
huzibeba timu nyingi kufuzu.
Kuanza vizuri kwa Stars katika mechi za makundi kuwania
kucheza michuano mikubwa ya kimataifa limekuwa jambo la kawaida kwa takriban
miaka sita sasa, lakini ajabu mechi zinazofuata Stars hudorora kabla ya
kuzinduka mwishoni tena.
Nitakumbusha; kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika Ghana
mwaka 2008, Stars ilianza kwa kuifunga Burkina Faso 2-1 katika mchezo wa kwanza-
lakini baadaye katika mechi ya tatu ilifungwa na Senegal 4-0, ikalazimishwa
sare ya 0-0 nyumbani na Simba hao wa Teranga kabla ya kufungwa mechi ya mwisho
na Msumbiji 1-0, ambao mechi ya kwanza ilitoka nao sare ya bila kufungana kwao.
Tukakosa tiketi ya kwenda Ghana- wakati kuelekea Angola na Afrika
Kusini 2010, tuliboronga vibaya, tukilazimishwa sare mbili nyumbani na Mauritius
1-1 na Cameroon 0-0, tukafungwa ugenini na Cameroon 2-1 na Carpe Verde 1-0, wakati
ugenini tulishinda mechi moja tu na Mauritius 4-1- na nyumbani tukashinda pia mechi
moja na Carpe Verde 3-1.
Tukakosa tiketi ya kwenda Angola au Afrika Kusini,
tukafukuza kocha, Mbtrazil Marcio Maximo na kuajiri Mdenmark, Jan Borge
Poulsen. Tukaingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya Gabon na Equatorial
Guinea 2012, ambako pia nako tulianza vema kwa sare ya ugenini ya 1-1 na
wenyeji Algeria.
Wengi wakiamini timu imeimarika, mechi ya pili tukafungwa
nyumbani 1-0 na Morocco na mechi iliyofuata tukaenda kufungwa tena na Jamhuri
ya Afrika ya Kati 2-1 wakati, mechi pekee tuliyofanikiwa kushinda nyumbani ni
dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-1, huku mechi mbili nyingine tukifungwa na
Morocco 3-1 na moja na Algeria tukitoka sare tena 1-1.
Sasa tumeanza na kipigo cha 2-0 ugenini na Jumamosi tuna
mechi ya nyumbani dhidi ya Gambia katika Kundi letu. Timu imerejea jana na leo
inaanza maaoezi rasmi kwa ajili ya mechi hiyo na Watanzania wana kiu kweli na
kucheza fainali za 2014 Brazil, ambazo kama tukifanikiwa zitakuwa za kwanza
kwetu.
Ni vigumu, lakini sioni kwa nini tushindwe ikiwa Angola
walicheza fainali za mwaka 2006 Ujerumani. Ni mipango tu ambayo sisi bado
hatuna.
NINI TATIZO LETU?
Hilo ndilo swali ambalo tunapaswa kujiuliza, soka yetu
imekuwa kama homa za vipindi inapanda na kushuka. Haina matokeo ya kufululiza iwe
mabaya au mazuri. Tatizo nini, wachezaji, makocha, au uongozi mbovu wa TFF?
Tumekwishafukuza makocha wawili, Maximo na Poulsen na
wachezaji wamebadilishwa sana. Nini bado tatizo?
Kujitambua na kukosa maono ya mbali kwa wachezaji wetu, ni
moja ya matatizo, ambalo leo nitalizungumzia, ingawa yapo mengine kama uongozi
mbovu wa TFF yetu ya sasa chini ya Leodegar Chilla Tenga.
Kwa nini wachezaji? Beki
wa zamani wa Chelsea, Mnigeria Celestine Babayaro alipokuwa Nairobi miezi miwili
iliyopita katika ziara ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, alisema kwamba
tatizo la soka ya Afrika ni uongozi mbovu. Kumbe tatizo hili ni la Afrika nzima
na si Tanzania pekee, lakini nchi nyingine, wachezaji wake wanapiga hatua na
kwa uwezo wao, wanazisaidia hadi timu zao za taifa kupata matokeo mazuri, mfano
Zambia mabingwa watetezi wa Afrika.
Hiyo ni kwa sababu wachezaji wa nchi hizo, kwanza wanakuwa
na ndoto binafsi za kutimiza kisoka na wanapigana kutimiza ndoto zao- kubwa
kucheza Ulaya kwa ajili ya kunufaika kifedha.
Katika kuelekea kwenye safari hiyo, wanajikuta wanajituma
katika timu zao za taifa, ili kutafuta vigezo vya kucheza Ulaya na hapo ndipo timu
zao za taifa zinanufaika nao na wao wananufaika pia kwa kutimiza ndoto zao.
Lakini kwa wachezaji wetu wa Tanzania, hali ni tofauti sana-
mchezaji hujituma mwanzoni tu, ila akishaandikwa na magazeti ya kibongo na
kusifiwa kidogo, anavimba kichwa na kiwango kinaanza kushuka hata kabla
hakijapanda.
Sitaki kuuliza nani yuko wapi- ila turejee kikosi
kilichocheza na Cameroon katika sare ya 0-0 Dar es Salaam, kati ya 11 walioanza
siku hiyo, wangapi wataanza tena Jumamosi na Gambia?
Wachezaji wetu wanachoka haraka sana. Kwa nini? Ule usemi wa
wahenga sifa zinaua, tena zinawaua kweli wachezaji wetu. Wakisifiwa kidogo tu wanavimba
vichwa, wanaota ‘majipu’ kwapani, hata salamu inakuwa taabu sana, juhudi
mazoezini inashuka na siku mbili tu naye soka inamtoroka mguuni, anabaki mtu wa
kelele.
Nimesikitika sana, Nizar Khalfan anasema amesaini Yanga,
akitokea Ligi Kuu ya Marekani na wakati huo huo, leo Danny Mrwanda anaweza
kusaini Simba. Wachezaji wetu hawawezi hata kucheza nje!
Angalau siku hizi wanasema ukweli, zamani walikuwa wana tabia
wakienda nje, wakirudi na kukutana na Waandishi wanasema, wamerudi mara moja
kwa matatizo ya kifamilia na watarejea muda si mrefu, mwishowe unamsikia
amesaini hapa hapa tena.
Siku hizi wanasema, mkataba wangu umeisha, sijaongezewa,
nimerudi nyumbani. Nakumbuka mwaka 1999 katika hafla za tuzo za TASWA, rais
Jakaya Kikwete wakati huo akiwa bado Wizara ya Mambo ya Nje, alizungumzia matatizo
ya wachezaji wetu kushindwa kucheza nje, na akatoa mfano huo huo wanaporudi,
husema wamekuja mara moja.
Wakati umefika sasa, wachezaji wetu wa kizazi kipya akina
Shomary Kapombe, Jonas Mkude na Juma Abdul, wajifunze kutokana na makosa ya
kaka zao, ili miaka ijayo tuwe na aina mpya ya wachezaji.
Wachezaji ambao, kwanza watakuwa ndoto na matarajio na pili
kuwa na kiu ya kweli na dhamira ya dhati ya kutimiza ndoto na matarajio yao. Wachezaji
ambao watakuwa na maono ya mbali, ambao hawatavimbishwa vichwa na ‘headlines’
za Mwanaspoti, zinazosifia ‘mpaka basi’.
Lakini, hata kwa wachezaji wa sasa wa timu ya taifa, wanapaswa
kujua siri ya kufanya vizuri uwanjani ni kujituma mazoezini na kusikiliza kwa
makini mafundisho ya makocha. Ajabu wachezaji wa siku hizi wana dharau,
hawajitumi mazoezini, hawasikilizi makocha, halafu wanasema makocha siyo
wazuri.
Unakuta Stars hii iliyopo kambini hivi sasa, kuna wachezaji
wanamheshimu kocha Mkuu tu, Mdenmark, Kim Poulsen tu, hawawaheshimu makocha wasaidizi
akina Sylvester Marsh na Juma Pondamali wala Meneja wao, Leopold Mukebezi. Namna
hii utategemea nini?
Lazima wachezaji wabadilike na wawe na nidhamu- kwani huo
ndio msingi wa mafanikio. Pia, wachezaji wetu kwenye mechi hawana juhudi
zozote. Hawajitumi. Hawapigani. Wanacheza utafikiri waliingia kwenye kambi ya
timu ya taifa wakitokea Borussia Dortmund, FC Twente, Napoli, Marseille, Spurs
au Bilbao, kumbe wametokea kwa Mnyamani wengine kwa Tumbo tu hapo na wana
safari ndefu kuelekea kwenye kilele cha mafanikio. Wanaridhika nini? Sijui!
Bado naamini maisha yako unayakwamisha au kuyafanikisha wewe
mwenyewe kulingana na akili, fikra na jitihada zako. Kama wachezaji wetu
wanaona kucheza TP Mazembe ni kilele cha mafanikio yao, basi itakuwa hivyo,
lakini kama watataka kuvunja rekodi ya Sunday Manara, au Kassim Manara, basi
watafanikiwa.
Nataka nimzungumzie mchezaji mmoja wa Stars hivi sasa, Mbwana
Ally Samatta ‘Sama Goal’ kama mfano- kwa sasa anakabiliwa na changamoto kubwa
ya kufanya mageuzi kwa wachezaji wa Tanzania- kwa kuhakikisha anakuwa mfano wa
wachezaji watakaotimiza ndoto za kufika mbali.
Kivipi? Dogo dizaini ametosheka fulani hivi na maisha ya
Lubumbashi- lakini hapana. Anatakiwa kufunguka zaidi na kutafuta nafasi ya
kucheza Ulaya ndani ya miaka hii miwili ajiwekee malengo ya kuhakikisha amekwishatoka
Afrika.
Hawezi kutoka kwa maneno, atufungie mabao pale Taifa Stars
kwa juhudi zake binafsi watu wakiri kijana ni hatari kwa uwezo wa soka yake
uwanjani na si minyoo ya kisasa na mitindo ya mavazi nje ya uwanja.
Samatta anacheza hapo tu DRC, lakini Nizar alikuwa Marekani
na amecheza Ligi Kubwa zaidi dhidi ya wachezaji wakubwa zaidi- leo amerudi nyumbani
kusaini Yanga. Mimi sitapenda kuona Samatta naye akirejea nyumbani karibuni,
nataka afike mbali. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment