![]() |
Stars mazoezini |
TIKETI kwa za kushuhudia mechi kati ya timu ya soka ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars na Nge wa Gambia, zitaanza kuuzwa kesho (Juni 9 mwaka
huu) kuanzia saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa
Ohio na Samora, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Soko Kuu la Kariakoo na
Uwanja wa Taifa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace
Wambura Mgoyo amiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, mauzo yataendelea pia
hadi siku ya mechi kwenye vituo hivyo kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 6 mchana
kabla ya kuhamia Uwanja wa Taifa.
Ametaja viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa
viti vya rangi ya bluu na kijani ambavyo ni 36,693 kati ya jumla ya viti 57,558
vilivyopo katika uwanja huo wa kisasa. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa
ni sh. 5,000, wakati kwa upande wa VIP C watalipa sh. 10,000 wakati VIP B ni
sh. 20,000. Kiingilio kwa jukwaa la VIP A ambalo linachukua watazamaji 748 tu
ni sh. 30,000 kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni.
Nge wa Gambia waliwasili nchini jana saa 5.30 usiku kwa
ndege ya Kenya Airways tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars
itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Msafara wa timu hiyo wenye watu 31 wakiwemo wachezaji 22
unaongozwa na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo wan chi
hiyo, Malang Jassey.
Viongozi wengine ni Ofisa Utawala wa timu Modou Sowe, Kocha
Luciano Machini, makocha wasaidizi Peter Bonu Johnson na Lamin Sambou, Kocha wa
makipa Alhagie Marong, mtaalamu wa tiba mbadala (physiotherapist) Pa Matarr
Ndow, Mtunza vifaa Sanna Bojang na Daktari wa timu Kalifa Manneh.
Wachezaji ni Musa Camara, Abdou Jammeh, Momodou Futty Danso,
Lamin Basmen Samateh, Ousman Koli, Pa Saikou Kujabi, Mustapha Kebba Jarju,
Yankuba Mal Ceesay, Demba Savage, Saihou Gassama, Alieu Darboe, Momodou Ceesay,
Pa Modou Jagne, Tijan Jaiteh, Bubacarr Sanyang, Christopher Allen, Musa Yaffa,
Sulayman Marr, Mamut Saine, Hamsa Barry, Ali Sowe, Omar Colley na Saloum Faal.
Nge hao, watafanya mazoezi yao ya kwanza katika ardhi ya
Tanzania leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, wakati kesho
muda huo huo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa.
Wakati huo huo, kambi ya Taifa Stars inaendelea vizuri na jioni
hii timu itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, wakati kesho itafanya mazoezi kwenye
uwanja huo huo kuanzia saa 11 jioni baada ya Gambia kumaliza.
Jumamosi saa 4 kamili asubuhi kutakuwa na mkutano kati ya
makocha wa timu zote mbili; Mdenmark Kim Poulsen wa Taifa Stars na Mtaliano
Luciano Machini wa The Scorpions wakiwa na manahodha wao na Waandishi wa Habari
utakaofanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
0 comments:
Post a Comment