'Meja' Ally Mayay Tembele |
PINGAMIZI linaandaliwa na kambi ya mmoja wa wagombea wa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, dhidi ya mgombea wa nafasi hiyo, Ally
Mayay Tembele, beki na Nahodha wa zamani wa klabu hiyo.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata leo, zimesema
kwamba kambi hiyo inataka kuwasilisha pingamizi kwa Kamati ya Uchaguzi, kupinga
‘Meja wa Soka’, Mayay kugombea nafasi yoyote Yanga, kwa sababu uchaguzi
utakaofanyika Julai 15, mwaka huu ni wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu,
akiwemo Mayay mwenyewe.
“Mayay alikuwa kiongozi Yanga, akajiuzulu. Kutokana na
wajumbe wengine pia kujiuzulu, akiwemo Mwenyekiti na Makamu wake, safu ya
uongozi ikawa inapwaya, ndipo TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ikaagiza
ufanyike uchaguzi kujaza nafasi. Viongozi alioingia nao madarakani Ally ambao
hawajajiuzulu kama Mohamed Bhinda, bado wapo.
Sasa iweje Mayay agombee tena? Huku ni kuchezea Katiba ya
klabu. Maana yake hata gharama ambazo klabu inaingia kwa kurudia uchgauzi, yeye
hazizingatii,”alisema mtoa habari huyo, leo.
Juhudi za kumpata Mayay kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa
kwa haraka, inagwa bado BIN ZUBEIRY inamtafuta na
akipatikana tutapandisha maelezo yake.
Katika uchaguzi huo, Yussuf Mehboob Manji atachuana na John
Jambele, Edgar Chibura na Sarah Ramadhani kwenye nafasi ya uenyekiti, wakati wapinzani
wa Mayay ni Ayoub Nyenzi, Yono Kevela na Clement Sanga.
Katika nafasi za Ujumbe waliorudisha ni Lameck Nyambaya,
Ramadhani Mzimba ‘Kampira’, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Said, Edgar Fongo, Beda
Simba, Ahmad Gao, Mussa Katabaro, George Manyama, Aaron Nyanda, Abdallah Bin
Kleb, Omary Ndula, Shaaban Katwila, Jumanne Mohamed Mwammenywa, Abdallah
Mbaraka, Peter Haule, Justin Baruti na Abdallah Sharia.
0 comments:
Post a Comment