![]() |
Boban akihojiwa na Waandishiwa Habari |
Na Mahmoud Zubeiry
KIUNGO Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ alitokea benchi na moja
kwa moja kwenda kumuumiza beki kizingiti wa Yanga, Kevin Yondan hadi akashindwa
kuendelea na mchezo wa wapinzani wa jadi, jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kweli Yanga ilipata pigo kumpoteza beki wake mahiri, Yondan,
lakini kwa mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts timu hiyo
iliimarika zaidi.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, aliyeng’ara
kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978, alimuingiza Juma Abdul badala ya
Yondan.
Abdul akaenda kucheza beki ya kulia alikokuwa anacheza Mbuyu
Twite, ambaye alihamia katikati kuziba pengo la Yondan.
Kutoka hapo Yanga, ilianza kucheza vizuri kila idara
ikionyesha mchango wake uwanjani. Kwa nini? Yanga wamekuwa wakilazimisha
kumpanga Mbuyu, wakati huo huo inataka kutumia mabeki wengine wa kati ilionao,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Yondan.
Haikuwa vibaya Yanga kumsajili Mbuyu Twite, kwa sababu baada
ya Cannavaro na Yondan, beki mwingine wa kati waliyekuwa naye ni Ibrahim Job
pekee.
Niliamini kusajiliwa kwa Twite, maana yake Yanga itakuwa na mabeki
wawili wa kati uwanjani na wawili benchi, lakini sasa si hivyo.
Ni kama Yanga imeridhika na uchezaji wa pamoja wa Yondan na
Cannavaro, lakini inalazimisha na Twite acheze.
Mwanzoni, Twite alikuwa anapangwa kama kiungo mkabaji, lakini
akashindwa kucheza kwa ubora wa Athumani Iddi ‘Chuji’, hivyo akahamishiwa beki
ya pembeni.
Morogoro dhidi ya Mtibwa alipangwa beki ya kushoto, akawa
uchochoro wa Hussein Javu na mechi nyingine zilizofuata amekuwa akicheza beki
ya kulia- pia uchezaji wake hauridhishi kama ambavyo wanacheza Juma Abdul,
Godfrey Tauta, au Nahodha Nsajigwa Shadrack wenye nafasi yao.
Jana hilo limedhihirika, wakati anacheza beki ya kulia, Twite
pamoja na kusaidia sana mashambulizi, lakini alikuwa anashindwa kumdhibiti
Edward Christopher, ila alipoingia Juma Abdul alitekeleza jukumu hilo vema,
akizuia na kusaidia mashambulizi.
Hata Twite alipohamia katikati, alicheza vizuri na ubora wake
ule uliofanya agombewe na Simba na Yanga ulionekana.
Twite ni beki wa kati na naamini anaweza kucheza vizuri
nafasi hiyo tu, hizo nyingine analazimishwa kwa sababu ni mchezaji nyota na
wenye timu yao hawataki aanzie benchi.
Lakini wapo watu waliosajiliwa maalum kwa ajili ya nafasi
hizo, tena wengi mno. Katika nafasi ambazo Yanga imewekeza vizuri kwenye timu
yake, basi ni mabeki wa pembeni.
Kulia peke yake wapo watatu, Nsajigwa, Abdul na Taita na
kushoto pia wapo watatu, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika, sasa
kama beki wa kati anapelekwa pembeni, hawa waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza
nafasi hizo wacheze wapi?
Hapa sasa unaweza kuona Twite anaivuruga Yanga kwa
kulazimishwa kucheza na kitu kingine ambacho sielewi Yanga ni kuwachezesha
mbele mabeki wa pembeni, wakati timu ina viungo wengi tu wa pembeni.
Mara nyingi makocha wengi duniani hutumia mabeki mbele katika
kujihami na sana hutokea katika mechi ngumu, kama fainali kocha anajua
anakutana na timu yenye kushambulia sana, hivyo anaongeza wakabaji uwanjani.
Kweli Boban alipomuumiza Yondan, aliiathiri Yanga, lakini upande
wa pili aliisaidia sana. Kwa sababu asingemtoa uwanjani Yondan, ina maana Twite
angeendelea kuwa uchochoro kule kulia na lolote lingetokea.
Ila kwa sababu Yondan alitoka, yakafanyika mabadiliko
yaliyoisaidia Yanga.
Mbuyu Twite |
0 comments:
Post a Comment