![]() |
Wachezaji wa Mtibwa |
Na Prince Akbar
MTIBWA Sugar ya
Morogoro wamezinduka katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibuka
na ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja Chamazi, Dar es Salaam, dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.
Mechi hiyo ilitakiwa
kuchezwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi lakini kwa sababu ya kuonyeshwa
moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport ya Afrika Kusini imechezwa Uwanja
wa Azam.
Katika mchezo huo
uliokuwa mkali na wa kusisimua, mabao ya Wakata Miwa wa Manungu, yalitiwa
kimiani na Hussein Javu dakika ya 13, Awadh Juma dakika ya 16 na Shaaban Nditi dakika
ya 62, wakati ya Ruvu yalifungwa na Paul Ndauka dakika ya 30 kwa penalti na Abrahman Mussa dakika ya 64.
Ushindi huo, unaifanya
Mtibwa ifikishe pointi saba na kupanda hadi nafasi ya tatu, wakati Ruvu
inabakia ‘danger zone’.
Katika mchezo wa jana wa ligi hiyo, Yanga ilishinda
mabao 3-1 dhidi ya African Lyon Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, shukrani kwake
kiungo anayecheza kwa nadra kwenye timu hiyo, Nizar Khalfan aliyefunga mabao ya
ushindi dakika ya 65 na 88, akitokea benchi kuchukua nafasi ya Frank Domayo.
Nizar alifunga bao la pili, sekunde chache baada ya
Benedictor Mwamlangala kuisawazishia African Lyon bao lililodumu tangu dakika
ya 17, baada ya Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kutangulia kufunga dakika
ya 17.
Ushindi huo, uliifanya Yanga ifikishe pointi saba,
baada ya kucheza mechi nne na kupanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa
ligi, ikiwa inalingana na Coastal kwa pointi na wastani wa mabao, ingawa
Coastal wako nyuma kwa mechi moja, ingawa kwa matokeo ya leo, inashuka hadi
nafasi ya tano.
Simba juzi iliichapa Prisons ya Mbeya iliyorejea
Ligi Kuu msimu huu mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Felix Mumba Sunzu na Mrisho
Ngassa, wakati la Prisons lilifungwa na Elias Maguri.
Simba bado inaongoza ligi hiyo, kwa pointi zake 12,
ikifuatiwa na Azam iliyoifunga JKT Ruvu 3-0 Ijumaa, mabao ya John Bocco ‘Adebayor’,
Kipre Herma Tchetche na Kipre Michael Balou yenye pointi 10.
0 comments:
Post a Comment