![]() |
Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry
MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia
Hans Poppe amesema kwamba hadi sasa klabu yake haijapata barua ya hukumu ya
pingamizi zao dhidi ya wachezaji Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuidhinishwa
kuchezea Yanga kutoka Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Kapteni huyo wa
zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba anashangaa kwa nini
barua hiyo inachelewa, wakati barua ya hukumu ya Emmanuel Okwi kufungiwa mechi
tatu wamekwishaipata.
“Mpaka leo barua kuhusu maamuzi ya Twite na Yondan
kuidhinishwa kucheza Yanga hatujapata, ila ya Okwi tumepata, sijui hii inamaanisha
nini,”alisema Hans Poppe.
Alisema sasa Simba wanaamini TFF inahofia wakikata rufaa,
Mahakama ya Usuluhishi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), CAS wataaibika
kwa uamuzi waliochukua.
“Tumekwishawaandikia barua ya kuwaomba hati ya hukumu siku
nyingi, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa tunashindwa kuelewa nini lengo
lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda, sasa wamejawa hofu na
wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans Poppe.
Septemba 10, mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo
hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka
kulipeleka suala hilo CAS.
Kamati hiyo, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya
kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati
hiyo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji
za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni
mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini
mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na
baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa
madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
Kuhusu suala la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa
mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa
Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite,
hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo
alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya
Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho
chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani
Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Siku 21 walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua
Simba, zinamalizika keshokutwa, siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya
Tanzania, watamenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza.
0 comments:
Post a Comment