![]() |
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam leo kuhusu Akrama. |
Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Simba SC imeshangazwa
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumpanga refa Mathew Akrama wa Mwanza kuchezesha
mechi mbili mfululizo za Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Simba
SC, Ezekiel Kamwaga amesema asubuhi ya leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu,Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam kwamba Akrama atakayechezesha pambano la watani wa jadi kesho, ndiye
aliyechezesha mechi iliyopita ya Yanga na African Lyon.
“Kwa nyinyi ambao hamna
taarifa labda, lakini sisi tulikuwa tuna taarifa kwamba, kuna refa mwingine
alipangwa kuchezesha mechi ya Yanga na African Lyon, lakini akabadilishwa
akawekwa Akrama,”alisema Kamgwa.
Aidha, Kamwaga aliitupia
lawama Sekretarieti ya TFF kwa kutowatendea haki kwenye mambo mengi, likiwemo
suala la usajili wa mabeki Kevin Yondan na Mbuyu Twite.
“Tunajua sekretarieti
ya TFF ndiyo huwa inahusika kupanga marefa, na ndiyo hii hii ambayo tunailalamikia
haitutendei haki, sasa sisi tunamuomba mambo mawili makubwa Akrama, kwenye
mechi ya Simba na Yanga; kuna watu huwa wanapoteza maisha wakifungwa. Kuna watu
huwa wanapoteza fahamu, wanaweka rehani nyumba zao, mali zao kucheza kamari, na
wanaliwa.kuna viongozi wengine wamewahi kutimuliwa madarakani kwa sababu ya
kufungwa na Simba na Yanga.
Kwa hiyo, hii mechi ina
mambo mengi sana, sasa sisi tunamuomba Akrama asiue watu, asifanye watu
wakaliwa, asifanye watu wakapata mateso yasiyo na sababu,”alisema.
Kamwaga alisema Simba haitaki
kutetewa na refa huyo na haitarajii upendeleo wowote kutoka wake na wala haitaki
upendeleo wowote kutoka kwa Akrama. “Ila tunachomuomba, atende haki. Achezeshe kwa
kufuata sheria 17 za soka,”alisema.
Kamwaga aliongeza kuwa,
kwa sababu hiyo itaonyeshwa na Televisheni ya Super Sport, ni vema Akrama
akaitumia fursa hiyo kujipromoti katika medani ya kimataifa ya soka kama refa
bora.
“Mwaka jana katika Fainali
za Kombe la Mataifa ya Afrika, Tanzania haikuwa na refa wala mshika kibendera
hata mmoja, kwenye Kombe la Dunia, ndiyo usiseme. Sasa inatia aibu kwa kweli
kwa nchi kubwa kama Tanania, ambayo ina historia kubwa lakini haina marefa
kwenye mashindano makubwa, Akrama kama atachezesaha vizuri kesho, itamjenga na
anaweza kubebwa kwenye mashindano makubwa ya FIFA na CAF,”alisema Kamwaga.
Ofisa Habari huyo wa Simba,
alilalamikia pia klabu yake kutopewa barua ya kudai fedha za Twite, kama
ambavyo Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) iliagiza.
“Tumepata barua ya Okwi
kufungiwa mechi tatu bila kuomba, lakini hadi leo, hatujapata barua ya kudai
fedha za Twite, tulituma barua ya kuomba kukazia maamuzi ya sheria. Hadi jana
tunauliza maamuzi ya Kamati kwa maandishi, lakini hadi sasa hayajaandikwa.
Basi watuandikie barua
ya kukata fedha zetu kwenye mechi ya kesho. Hiyo pia inawashinda kuandika. Mmoja
wa viongozi wa TFF, alituambia tuwaandikie barua Yanga, kuomba tukate fedha
zao. Tunaona hiyo siyo sahihi, tunaona Sekretarieti ya TFF haina dhamira ya
kututendea haki, maana yake siku 21 zilizotolewa kama muda wa sisi kulipwa fedha
zetu za Twite, zinaisha kesho na hakuna dalili za kupata hizo fedha,”alisema
Kamwaga.
Septemba 10, mwaka huu
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex
Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya
Twite na Yondan na sasa wanataka kulipeleka suala hilo CAS.
Kamati hiyo, iliitaka
Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya
malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya
44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote
katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema
mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka
nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake
kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za
kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
Kuhusu suala la Mbuyu
Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi
na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote
katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema kwa
vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri
kuzirejesha,kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe
imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita kati ya
saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa.
Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na
Omari Gumbo.
Siku 21 walizopewa
Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua Simba, zinamalizika kesho, siku
ambayo watani hao wa jadi katika soka ya Tanzania, watamenyana katika mchezo wa
Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza.
0 comments:
Post a Comment