• HABARI MPYA

    Wednesday, October 17, 2012

    TFF ITUONYESHE DIRA, SI KWENDA KAMA GARI BOVU


    BAHATI iliyoje kwa Watanzania mwaka huu, timu yetu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imefuzu hadi hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Vijana wa umri huo Afrika, zitakazopigwa mwakani Morocco bila jasho.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Serengeti Boys ilikuwa icheze na Kenya Septemba 9, mwaka huu, mechi ya raundi ya kwanza ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika, lakini wapinzani wao wakajitoa na kuwapa makinda wa Tanzania tiketi ya kucheza na Misri katika raundi ya pili.
    Bahati kubwa, Misri nao wamejitoa na sasa Serengeti ambayo ilikuwa icheze na Misri mechi ya kwanza Oktoba 14, mwaka huu mjini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye, sasa itacheza Raundi ya Tatu dhidi ya mshindi wa mechi kati ya Zimbabwe na Kongo Brazzaville, mechi ya kwanza ikichezwa Novemba 18 mwaka huu mjini Dar es Salaam na marudiano wiki mbili baadaye ugenini.
    Zimbabwe na Congo Brazzaville zitapambana kati ya Oktoba 12-14 mwaka huu, Zimbabwe ikiwa mwenyeji wa mechi ya kwanza wakati ya marudiano itafanyika kati ya Oktoba 26-28 mwaka huu.
    Nasema hii ni bahati kwa sababu natambua umuhimu wa timu yetu ya vijana kushiriki fainali hizo za michuano ya Afrika kwa mustakabali wa soka yetu.
    Kupeleka timu ya vijana katika fainali za vijana ni mwanzo mzuri wa kuwa na timu bora ya taifa ya baadaye, ambayo pengine itafuta kilio cha muda mrefu cha Watanzania, kulilia matokeo mazuri na mafanikio katika soka ya kimataifa.
    Sote tunafahamu, Zimbabwe na Kongo Brazzaville wote wako vizuri kisoka na wana msingi mzuri wa soka ya vijana, hivyo ili kukabiliana nao, tunahitaji kuiandaa vema timu yetu.
    Niliwahi kumsikia, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah Malabeja anaisifia Rwanda, timu yao ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, baada ya kuwafunga mara mbili mfululizo vijana wa Tanzania, Ngorongoro Heroes katika mechi za kujipima nguvu Dar es Salaam.
    Sisi tulianza kucheza mechi za kimataifa miaka ya 1960, wakati Rwanda walianza mwaka 1998 na mwaka jana timu yao ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ilishiriki fainali za vijana wa umri huo za Kombe la Dunia.
    Katika fainali hizo zilizofanyika nchini Mexico, Rwanda haikuvuka hatua ya makundi, lakini ilipigana kiume, ilifungwa mechi mbili, 2-0 na England U17 na 1-0 na Uruguay U17 kabla ya kutoa sare ya bila kufungana na Canada U17 katika mechi ya mwisho.      
    Kwa ujumla hivi sasa Tanzania tumeachwa mbali kisoka na Rwanda, katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wapo nafasi ya 125 wakati Desemba mwaka 2008, walipanda hadi nafasi ya 78 na sisi tupo nafasi ya 128 wakati kupanda zaidi kwetu ilikuwa Desemba 2007, nafasi ya 89 na Oktoba mwaka 2005 tuliporomoka hadi nafasi ya 175.
    Mara kadhaa nimewahi kuandika umuhimu wa kuwekeza kwenye soka ya vijana na nikaelezea faida za kuomba kuandaa fainali za vijana za Afrika badala ya haya mabonanza ya Kombe la Challenge la CECAFA, lakini nadhani kwa wakubwa bado hiyo haina maana kwao na kwa sababu hiyo, tutaendelea kuburuza mkia.
    Sioni sifa za Rwanda hata watuzidi kisoka leo- nchi ndogo na imeingia kwenye soka ya kimataifa juzi juzi tu na hata Ligi Kuu yao haina ubora na ushindani kama ligi yetu- lakini kwa sababu ya mipango yao thabiti ya uwekezaji katika soka la vijana, wametuacha na watatuacha sana iwapo hatutobadilika.
    Mwaka 2011 Rwanda walikuwa wenyeji wa fainali za U17 za Afrika, ambazo walifanikiwa kuingia fainali na kufungwa mabao 2-1 na Burkina Faso.
    Awali ya hapo, mwaka 2009, Rwanda walikuwa wenyeji wa fainali za Afrika za U-20 na japokuwa hawakufanikiwa kutoka kwenye kundi lao, A, lakini walionyesha soka ya kuvutia, nachoweza kusema bahati haikuwa yao.
    Walishika nafasi ya tatu nyuma ya Ghana na Cameroon zilizosonga mbele, na wao wakawa juu ya Mali iliyoshika mkia. Walishinda mechi moja (2-1 dhidi ya Mali) na kutoa sare mechi moja, (1-1 na Cameroon) wakati moja walifungwa (2-0 na Ghana), iliyokwenda kuchukua hadi Kombe la Dunia, ikiifunga Brazil kwa penalti 4-3 nchini Misri, baada ya sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
    Faida ya uwekezaji huo ni timu imara ya taifa tuliyoishuhudia mwaka jana ikicheza soka safi katika Kombe la Challenge na kufika fainali, ambako ilifungwa kwa taabu na Uganda. 
    Kikosi cha Rwanda katika fainali za U20 mwaka 2009, kiliundwa na akina Jean-Luc Ndayishimiye, Aimable Rucogoza, Annuar Kibaya, Arafat Serugendo, Michel Hitimana, Jean-Claude Iranzi, Jean Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Elias Uzamukunda, Herman Ngoma, Ernest Kwizera, Yussuf Ndayishimiye, Jean Bosco Ngaboyisibo, Robert Muvunyi, Aboubakar Nshimiyimana, Bonfils Christian Twahirwa, Eric Habimana na Emery Mvuyekure ambao wengi wao wanaibeba Amavubi hivi sasa.
    Wakati huo huo, vijana waliocheza Kombe la Dunia la U17 Mexico mwaka jana wanakuja vizuri kueleeka kuunda timu bora ya kizazi kipya cha Rwanda.
    Msingi wa mwisho mzuri wa soka ya vijana Tanzania uliokaribia kuzaa matunda ulikuwa ni timu ya mwaka 2004, enzi za Muhiddin Ndolanga pale TFF, timu ambayo ilikuwa inaundwa na akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Juma Jabu, Amir Maftah, Omary Matuta, Nurdin Bakari, Adam Matunga na wengineo, ambao sasa hivi wakicheza wanaitwa ‘babu’.
    Timu hiyo ilifuzu kucheza fainali za vijana Afrika zilizofanyika Gambia, lakini ikaenguliwa kutokana kashfa ya kufoji umri wa Nurdin Bakari na nafasi wakapewa Zimbabwe ambao kwa pamoja na Rwanda na Zambia, walitolewa na Serengeti Boys yetu iliyokuwa chini ya makocha Abdallah ‘King’ Kibadeni na Sylvester Marsh.
    Baada ya hapo, kwa muda mrefu chini ya utawala wa Leodegar Chilla Tenga, hatukushiriki mashindano ya vijana hadi mwaka 2010 kama sikosei tulipoanza kurudi taratibu, tena baada ya kelele nyingi za wadau. 
    Kwa kuwa tuna misingi mizuri ya awali ya uibuaji wa vipaji vya vijana, mara zote hatukosi timu, tatizo letu ni kukosa programu nzuri endelevu na kwa ujumla namna ya kuandaa timu. Hapo bado tuna ‘0’ mbaya. 
    Kwa sasa, Serengeti Boys imefuzu katika Raundi ya Tatu na ya mwisho kuwania kucheza fainali za mwakani nchini Morocco na itacheza na Zimbabwe au Kongo Brazzaville, baada ya kupita bila jasho kutoka Raundi ya kwanza na ya pili, kufuatia kujitoa kwa Kenya na Misri.
    Wachezaji wanaounda kikosi cha Serengeti Boys ya sasa chini ya Kocha Mdenmark, Jakob Michelsen ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu), mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).
    Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu) na washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).
    Kulingana na msingi mzuri wa kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi uliopo nchini hivi sasa, kuanzia Copa Coca Cola, Airtel Rising Star, mashindano ya shule za msingi na sekondari na hata akademi, au vituo kadhaa vya soka tulivyonavyo kwa sasa Tanzania- hakuna shaka juu ya timu hii ni nzuri.
    Lakini je, tujiulize tuna dira mwafaka ya kutufikisha Morocco mwakani?
    Timu hiyo ilikwenda Mbeya kwa mwaliko wa Chama cha Soka Mbeya Mjini (MUFA), ambacho, kiliihudumia kwa malazi, chakula na huduma nyingine ndogondogo na kucheza mechi kadhaa za majaribio ikiwemo dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons.
    Niliwahi kuuliza, kambi ya Mbeya ni kwa kuwa MUFA wamejitolea kuihudumia timu ndiyo maana imepelekwa Mbeya, au ni programu ya maandalizi ndiyo imeipeleka timu Mbeya? Haya timu imerudi Dar es Salaam, ikacheza tena Ashanti na baadaye Yanga B, kisha ikavunja kambi.
    Sioni nini kinaendelea hapa, zaidi ya maandalizi ya zimamoto tu ambayo miaka nenda, rudi yametufanya tumekuwa wasindikizaji na tunapitwa na vi- nchi vidogo vidogo kama Rwanda.
    Naamini, huu ni wakati mwafaka sasa kuwekeza katika maandalizi ya kisayansi kwa Serengeti Boys, ambayo inaundwa na vijana wasio na majukumu kwa klabu yoyote, ambao kuwandaa ni jambo jepesi mno.
    Tuna Idara ya Ufundi, timu ina kocha wa kigeni, anayesaidiwa na kocha mzoefu tu, Jamhuri Kihwelo, je, iko wapi programu yao ya maandalizi?
    Lazima tukubali, tumekuwa na bahati nzuri sana katika mashindano ya U17 ya mwaka huu na kama kuna bajeti ilitengwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Kenya na Misri, sasa itumike kwa maandalizi madhubuti ya kucheza na mshindi kati ya Zimbabwe na Kongo Brazzaville
    Tuondoe fikra kwamba, kujitoa kwa Kenya na Misri sisi ‘tume save’ bajeti, hapana- lazima fedha hizo zitumike kwa maandalizi mazuri zaidi kwa ajili ya mtihani huo wa mwisho. Upo umuhimu wa kuwa na programu kuelekea mechi hiyo ambayo lazima ifanyiwe kazi.
    Vijana wanahitaji japo michezo miwili ya kimataifa- dhidi ya timu nyingine za vijana zinazowania nafasi hiyo, ambazo si Kongo Brazzaville na Zimbabwe. Ni kazi rahisi tu, nazo zipo kwenye maandalizi ya kucheza, hivyo ni suala la viongozi wetu wa TFF kuwasiliana na viongozi wenzao wa FA za nchi ambazo tunataka kucheza nazo na kupanga.
    Nimesema fedha ambazo zilitengwa katika bajeti ya kucheza na Kenya na Misri zitumike sasa kuiandaa timu kwa ajili ya mtihani huu wa mwisho, kwa sababu najua katika kutafuta mechi tunaweza kukosa timu ya kuja kucheza na timu yetu hapa, lakini ni vigumu kukosa nchi ya kutukaribisha nchini mwake kucheza na U17 yao.
    TFF iseme hata kama tatizo ni fedha za kuiandaa timu, turejee mafanikio ya Serengeti ya akina Chuji na Nizar- harambee ya wananchi iliiwezesha, basi TFF ishirikiane na vyombo vya habari kuanzisha kampeni ya kuichangia timu, iweze kupata maandalizi mazuri, dira yetu ikiwa ni kucheza Fainali za Kombe la Dunia za vijana wa umri huo mwakani Falme za Kiarabu (UAE).
    Umefika wakati sasa TFF lazima iwe na dira na si kwenda tu kama gari bovu, na kwa kuanzia iwaonyeshe Watanzania kama kweli ina dira ya kutufikisha UAE mwakani. Wasalam.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TFF ITUONYESHE DIRA, SI KWENDA KAMA GARI BOVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top