• HABARI MPYA

    Thursday, October 04, 2012

    YONDAN NJE WIKI MBILI AKIUGUZA MAUMIVU YA BOBAN

    Kitu hicho!

    Na Mahmoud Zubeiry
    BEKI Kevin Yondan wa atakuwa nje kwa wiki mbili, kutokana na kuumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Daktari wa Yanga, Sufiani Juma ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba beki huyo tegemeo wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, tangu jana alikuwa anasikia maumivu makali na baada ya kufanyiwa vipimo katika Kitengo cha Mifupa cha Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili (MOI), imeelezwa anatakiwa kupumzika wiki mbili.
    Lakini Yondan pia anaweza kukaa nje ya Uwanja kwa zaidi ya muda, huo kwani majibu hayo yanatokana na uchunguzi wa awali.
    Yondan aliumizwa jana wakati Yanga ikitoka nyuma na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
    Yanga ambao walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri Kiemba.  
    Hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba dakika ya pili, wakati Yanga ilisawazisha dakika ya 63, baada ya beki Paul Ngalema kuunawa mpira katika harakati za kuokoa na refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Katika dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’. Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na hasira za kitoto.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YONDAN NJE WIKI MBILI AKIUGUZA MAUMIVU YA BOBAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top