![]() |
Athumani Iddi 'Chuji' akifumua shuti |
ATHUMANI Iddi Athumani ‘Chuji’, ni miongoni mwa wanasoka mfano wa kuigwa Tanzania kulingana na misukosuko aliyoipitia katika maisha yake ya soka na kumudu kusimama imara tena na tena, hadi leo anacheza kwa kiwango cha juu, akiwa mchezaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Ili kujua mengi juu ya kiungo huyo wa Yanga SC, fuatilia mahojiano haya na BIN ZUBEIRY.
![]() |
Athumani Iddi 'Chuji' |
BIN ZUBEIRY: Habari za leo Chuji
CHUJI: Nzuri tu kaka, mambo zaidi?
BIN ZUBEIRY: Shwari. Bila shaka hapa patatufaa kufanya mahojiano yetu.
CHUJI: Ndiyo, tuendelee tu kaka
BIN ZUBEIRY: Kwanza, niambie hili jina Chuji linatokana na nini?
CHUJI: Eee bwana hili jina mimi nilipewa siku nyingi sana bado nipo mdogo sana na wachezaji wa Kurugenzi (Dodoma)…Sielewi kwa nini, lakini walianza kuniita hivyo wakati dingi (baba) anacheza timu hiyo, alikuwa ananichukua tunaenda naye kambini kwao, ndipo wachezaji wenzake wakaanza kuniita hivyo.
BIN ZUBEIRY: Asante, Nikitazama kikosi cha Taifa Stars hivi sasa, katika wale vijana wa Serengeti Boys mwaka 2004, naona umebaki peke yako, unajisikiaje kwa hilo?
CHUJI: E bwana eee, kwanza hiki ni kitu ambacho huwa kinaniumiza sana, kwa sababu ukitazama umri wetu bado mdogo, na sijui wenzangu kitu gani kimewapoteza, kwa sababu katika ile timu kulikuwa kuna watu wana vipaji sana ambao wangeendelea, basi naamini hata timu yetu ya taifa ingefanya makubwa sana. Kwa kweli nasikitika sana na inaniumiza sana, tumepoteza wapiganaji wa maana sana kutoka ile timu ambayo tulifuzu Fainali za Mataifa ya Afrika za vijana, lakini tukapokonywa nafasi kwa sababu ya mkanganyiko wa umri wa mmoja wetu (Nurdin Bakari).
BIN ZUBEIRY: Lakini kwa nini wachezaji wa Tanzania ni nadra sana kucheza muda mrefu, nini tatizo?
CHUJI: Kitu kubwa ni kutokana na kutojitunza na kutojithamini, unajua mtu ukishaamua maisha yako ni soka, basi unatakiwa lazima ukomae, hata ikitokea ukapotea, lakini ukirudi lazima uchagame…
BIN ZUBEIRY: Tangu Polisi Dodoma huu ni mwaka wa tisa unacheza Ligi Kuu, si haba, nini siri ya mafanikio yako?
CHUJI: Ni mazoezi tu na kujitunza, pia kuheshimu kipaji chako alichokujaalia Mwenyezi Mungu. Na kama hivyo, unateleza, unaanguka, lakini unasimama tena unasonga…
BIN ZUBEIRY: Katikati uliyumba na mengi yalizungumzwa, lakini sasa umesimama imara tena na uko juu, wachache huwa wanaweza kurudi baada ya kupotea…uliwezaje?
CHUJI: Kwanza kabisa, napenda kumshukuru sana Mungu, ulikuwa mtihani mzito. Lakini pia kilichonisaidia ni kusikiliza mawazo ya watu tofauti, kama hivi mtu anakuita katika wakati mgumu, haumpuuzi, unakwenda kumsikiliza, katika ushauri wake unachukua mazuri, unaacha mabaya, wakatokea watu wawili watatu wa kunisaidia. Makosa ndio ubinadamu, siyo mtu ukikosea basi unajisusa, hapana, kuteleza ni jambo la kawaida kwetu binadamu, ukikosea unatakiwa kukiri kosa lako, kisha unajirekebisha. We mwenyewe tu unajifirkia, umepoteza muda kiasi gani na vitu vingapi umepoteza, unaamua kujiwekea malengo ya kupambana, ili kufidia vyote…na ili ukubalike tena, kwa kweli ni kazi ngumu na inachukua muda, ila mimi namshukuru Mungu haikuwa hivyo, nimerudi kwa urahisi na nimekubalika tena haraka.
![]() |
Athumani Iddi 'Chuji' wa nne kutoka kushoto waliosimama katika kikosi cha Yanga 2013 |
BIN ZUBEIRY: Unaizungumziaje soka ya Tanzania kwa sasa, ukiilinganisha na miaka mitatu iliyopita?
CHUJI: Kwa sasa kidogo soka imechangamka, ushindani unakuja, lakini lazima ziongezeke timu za ushindani hadi ziwe kama sita hivi…
BIN ZUBEIRY: Unadhani kwa nini
CHUJI: Ipo wazi, timu nyingi zinacheza kwa nguvu pale zinapokutana na Simba na Yanga, lakini zingekuwa zikikaza mechi zote, hata timu ya taifa ingekuwa bora.
BIN ZUBEIRY: Na unasemaje kuhusu wachezaji wa sasa uwezo wao?
CHUJI: Wapo wapo, ila inasikitisha vijana wengi wanaochipukia, hawaendelezwi, wanapotea, yaani ili tuwe na wachezaji wengi wazuri katika nchi hii, lazima tutilie mkazo soka la vijana na pia kuwaendeleza vijana wanapoibuka. Lakini kwa sasa, taifa linaibua vipaji vingi, ila kwa kuwa haviendelezwi, vinapotea tu…
BIN ZUBEIRY: Yanga SC mnaongoza Ligi Kuu, lakini Azam haiku mbali nyinyi, unatabiri nini mwisho wa mbio hizi dhidi yenu na Azam?
CHUJI: Mimi nasema tusubiri hadi mwisho tuone, lakini sisi lengo letu ni kuchukua ubingwa.
BIN ZUBEIRY: Unadhani Taifa Stars inaweza kuipiku Ivory Coast katika mbio za kwenda Brazil 2014?
CHUJI: Mpira huu ndugu yangu, na ukiangalia umoja uliopo ndani ya timu kwa sasa, mimi nasema inawezekana.
BIN ZUBEIRY: Kuna ushindani mkubwa wa namba katika nafasi yako, kuanzia Yanga hadi Taifa Stars, unauzungumziaje?
CHUJI: Ukiangalia kwa upande wangu mimi nina uzoefu, ndiyo maana nataka sana vijana wapewe sapoti, ni kama sisi ilivyokuwa wakati tunaibuka, tulipewa sapoti na wakubwa waliokuwapo, tukafanikiwa. Binafasi mimi nawapa sapoti sana vijana.
![]() |
Chuji mzuzu |
BIN ZUBEIRY: Inaonekana makali yenu Yanga SC kama yanapungua, haswa katika safu ya ushambuliaji, nini tatizo?
CHUJI: Mimi naona tatizo ni umakini tu zinapotokea nafasi, na kwa bahati mbaya kuna watu wengine wakipoteza nafasi moja ya pili…basi wanakata tamaa, mpira ndivyo ulivyo, usitegemee mazuri kila siku, kikubwa ni kuendelea kupambana kwa umakini.
BIN ZUBEIRY: Kwa mwendo huu kweli, mashabiki wa Yanga watarajie zile 5-0 zitalipwa kweli?
CHUJI: Narudi kule kule, haya ni mashindano na ni ligi, ligi siyo Simba na Yanga tu eti kwa sababu ni wapinzani wa jadi, ligi ni kucheza mechi zote kwa matokeo mazuri, ili uwe bingwa. Kama ingekuwa bingwa anapatikana kutokana na mechi ya Simba na Yanga tu, sawa, sisi tunaichukulia mechi dhidi ya Simba kama nyingine zote, tunachotaka ni ushindi kwa mabao yoyote yale.
BIN ZUBEIRY: Umecheza, Simba, ukaja Yanga, ukarudi Simba na sasa umerudi tena Yanga, iko siku utarudi tena Simba SC?
CHUJI: (Kicheko). Kurudi tena Simba, sijui!
BIN ZUBEIRY: Kwa nini…
CHUJI: Haya maisha bwana, hakuna mtu anayeiona kesho yake na isitoshe mimi soka ndio taaluma yangu
BIN ZUBEIRY: Una muda gani zaidi katika mkataba wako na Yanga SC?
CHUJI: Mkataba wangu Yanga utaisha Juni mwakani.
BIN ZUBEIRY: Mmekwishafanya mazungumzo ya kuongeza mkataba?
CHUJI: Bado kwa kweli, lakini naona muda bado upo sana. Nina msimu mzima mwingine hapa.
BIN ZUBEIRY: Na ikitokea timu ikakupa ofa nzuri kuliko Yanga, utaamua nini?
CHUJI: Safi tu… nitaangalia maslahi tu
BIN ZUBEIRY: Ukiwa na umri wa miaka 25 sasa, bado una matarajio ya kucheza Ulaya?
CHUJI: Yapo, tena sana tu. Mimi ninaweza kucheza popote, niko vizuri.
BIN ZUBEIRY: Ni mchezaji gani anayekuvutia zaidi Tanzania kwa sasa na kwa sababu gani?
CHUJI: Kwa kweli wapo wengi, ila mmojawao ni Kevin Yondan, ni mtu wa kazi na anatambua wajibu wake.
BIN ZUBEIRY: Duniani?
CHUJI: Kwanza lazima ujue mimi ni shabiki wa Liverpool, hivyo mchezaji ninayempenda ni Steven Gerrard.
BIN ZUBEIRY: Baada ya soka, huwa unajiliwaza wapi?
CHUJI: Kupumzika tu nyumbani, tunafanya kazi ngumu sana, inabidi tupumzike, zaidi zaidi napenda sana kuangalia sinema
BIN ZUBEIRY: Bila shaka Chuji sasa ni baba wa familia, je shemeji yetu anaitwaje na mtoto wetu naye anaitwaje na umri gani sasa?
CHUJI: Shemeji yenu anaitwa Pili, mtoto anaitwa Sabri ambaye kwa sasa ana mwaka mmoja na miezi miwili...
BIN ZUBEIRY: Utapenda naye acheze soka?
CHUJI: Elimu kwanza, shule kwanza, hayo mengine yatafuata na yatakuja yenyewe tu bila kulazimisha.
BIN ZUBEIRY: Shemeji huwa anakuja uwanjani kukutazama unapocheza?
CHUJI: Hata siku moja, hana mapenzi ya kutokea kwenye kadamnasi, yeye akitoka ofisini kwake, nyumbani tu.
BIN ZUBEIRY: Haya kaka, kwa leo nashukuru na nikutakie kazi njema, mafanikio na ufanisi katika mambo yako.
CHUJI: Amiin kaka, kazi njema na wewe
BIN ZUBEIRY: Asante.