• HABARI MPYA

    Tuesday, April 16, 2013

    UJUMBE WA FIFA TAYARI UPO NCHINI, WAKOSA FURSA YA KUKTANA NA WAZIRI WA MICHEZO

    Primo kulia akiwa na Mamelodi katikati na Edgar Watson kushoto, Mtendaji Mkuu wa  FUFA, walipokuwa Uganda hivi karibuni kutatua mgogoro wa shirikisho hilo. Sasa ni TFF.

    Na Mahmoud Zubeiry
    MKUU wa Idara ya Uanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Primo Corvaro amewasili jana nchini tayari kutatua mgogoro wa Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wiki ijayo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo amesema kwamba Primo amewasili kwa pamoja na Mkuu wa Kanda hii, Ashford Mamelodi jana jioni.
    Hata hivyo, Wambura amesema Ujumbe huo wa FIFA umeshindwa kukutana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kwa kuwa hivi sasa yupo Bungeni, Dodoma.
    Wambura amesema ratiba nyingine ya ‘wakubwa’ hao inabaki kama ilivyopangwa awali kwa siku tatu kuanzia jana kabla ya kuondoka Alhamisi.
    Ujumbe huo utakutana na wagombea uongozi walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF ambao waliomba mashauri yao yaangaliwe upya, wagombea ambao walikata rufani FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kamati ya Rufani na Sekretarieti ya TFF.
    Wagombea watakaosikilizwa na ujumbe huo wa FIFA ni Jamal Emil Malinzi: Mgombea wa nafasi ya urais wa TFF ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, hivyo kuondolewa kwenye mchakato. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini likakataliwa. Hata hivyo, alikuwa ameshakata rufani FIFA.
    Wengine ni Michael Wambura: Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na rufani yake kukataliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF. Hakuomba shauri lake liangaliwe upya, lakini alikata rufani FIFA.
    Farid Salim Mbaraka Nahdi: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alienguliwa na Kamati ya Uchaguzi na baadaye rufani yake kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kutupwa na hali kadhalika ombi lake la kutaka shauri lake liangaliwe upya, kukataliwa.
    Elliud Peter Mvella: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF na kukata rufani Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF kabla ya maombi yake ya kutaka shauri lake kuangaliwa upya, kukataliwa.
    Mbasha Matutu: Mgombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye alikatwa na Kamati ya Uchaguzi na kukata rufani ambayo pia ilitupwa kabla ya kuomba shauri lake liangaliwe upya, ombi ambalo lilikataliwa.
    Hamad Yahya: Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye alipitishwa na Kamati ya Uchaguzi, lakini mwekaji pingamizi akakata rufani ambayo ilikubaliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na kuondolewa. Aliomba shauri lake liangaliwe upya, lakini Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF ikatupa ombi lake.



    RATIBA YA UJUMBE WA FIFA NCHINI
    Tarehe /Muda

    Tukio
    15 Aprili 2013
    Saa 12:30 – 03:00
    Kuwasili kwa wajumbe wa FIFA
    15 Aprili 2013
    Saa 04:00 – saa 05:00 usiku
    Kikao na Rais wa TFF pamoja na Sekretarieti
    16 Aprili 2013
    Saa 05:30 – 06:30 asubuhi
    Kukutana na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kupata taarifa ya uchaguzi
    16 Aprili 2013
    Saa 06:30 – 08:00 mchana
    Chakula cha Mchana
    16 Aprili 2013
    Saa 08:00 – 12:00 jioni
    Kukutana na wagombea walioondolewa
    17Aprili 2013
    Saa 03:00 – 05:00 asubuhi
    Kukutana na Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF
    17 Aprili 2013
    Saa 05:30 – 06:30
    Mchana
    Kupewa taarifa zinazohusiana na mchakato wa uchaguzi, i.e., kesi zilizo mahakamani

    17 Aprili 2013
    Saa 08:00 – 10:00 jioni
    Kukutana na watu wengine ambao FIFA wanaweza kuomba kukutana nao
    17Aprili 2013
    Saa 10:30 – 11:00 jioni
    Mkutano na waandishi wa habari – kushukuru mamlaka na pande zilizohusika kwa ushirikiano
    18 Aprili 2013
    Saa 10:00 – 12:00 Alfajiri
    Kuondoka hotelini kwa ajili ya safari

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UJUMBE WA FIFA TAYARI UPO NCHINI, WAKOSA FURSA YA KUKTANA NA WAZIRI WA MICHEZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top