Na Mahmoud Zubeiry
KIUNGO wa Yanga SC, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima ameondoka Dar es Salaam jana kwenda Tanga, akiwa anasumbuliwa na homa na amesema kwa hali yoyote kwa sasa atapambana kuhakikisha anaipa timu yake ubingwa kwanza.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Nahodha huyo wa Rwanda, alisema kwamba pamoja na kujisikia dalili za homa, lakini hatakubali kulala, bali anakwenda kuitumikia klabu.
“Hizi ni dakika za lala salama, tumepigana msimu mzima na ilikuwa ni vita kubwa, kuna kuchoka, lakini tutaendelea kupambana hadi tupate ubingwa. Napuuza hali yoyote, naenda Tanga,”alisema.
![]() |
Haruna Niyonzima; Ubingwa kwanza |
Akizungumzia mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya JKT Mgambo, Haruna alisema kwamba utakuwa mgumu kwa sababu wanacheza ugenini na pia kiuzoefu hali ya viwanja vya mikoani si nzuri.
“Najua tunakwenda kucheza katika Uwanja mbaya, wale wenzetu watakuwa wameuzoea kwa sababu wanacheza mechi zao zote pale, utakuwa mchezo mgumu lakini tutapigana kushinda,”alisema.
Haruna amesema wanataka kutangaza ubingwa ndani ya mechi mbili tu zijazo na baada ya hapo wacheze kushinda mechi zilizobaki ili kuhakikisha wanamaliza na rekodi nzuri kuliko timu nyingine zote.
“Hata tukifanikiwa kupata ubingwa baada ya mechi mbili, hatutahesabu tumemaliza, tutaendelea kutilia mkazo ili tushinde mechi zote tuwe na rekodi nzuri,”alisema.
Yanga SC imeondoka Dar es Salaam jana kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo dhidi ya JKT Mgambo inayopigana kuepuka kushuka Daraja, ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 22 katika nafasi ya 10.
Yanga inahitaji pointi sita katika mechi zake mbili zijazo, ili itimize 58 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote, maana yake kujihakikishia ubingwa mapema.