Na Prince Akbar
KWA asilimia 80, Simba itaachana na kocha Mfaransa, Patrick Liewig baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na sababu mbili kubwa, BIN ZUBEIRY inakuhafamisha.
Habari kutoka ndani ya Simba SC, zimesema kwamba, kwa kuwa kuna dalili za klabu hiyo kukosa nafasi yoyote ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika mwakani, hakutakuwa na sababu ya kuwa na kocha wa kigeni msimu ujao, anayelipwa mshahara mkubwa.
Lakini pia, inaelezwa Simba SC wangevumilia kuendelea na Mfaransa huyo, anayelipwa dola za Kimarekani 5,000 kwa mwezi (zaidi ya Sh. Milioni 8 za Tanzania) kama asingekuwa na matatizo kadha wa kadhaa.
“Hapa alipo amekwishagombana na wachezaji wengi, wengine kwa sababu na wengine bila sababu za msingi. Lakini pia, amegombana hadi na sisi viongozi. Ni mtu ambaye tumeona hatuwezi kuendelea kufanya naye kazi,”alisema kiongozi mmoja wa Simba SC.
Lakini inaonekana wapo baadhi ya viongozi ndani ya Simba SC wanavutiwa na utendaji wa Liewig pamoja na falsafa zake na wana matumaini naye makubwa.
Liewig ambaye ni kocha wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa, anaonekana kuamini zaidi juu ya wanasoka vijana na anataka kujenga Simba SC ya hivyo.
Pamoja na kuikuta Simba SC inaundwa na wachezaji wazoefu wenye majina makubwa katika soka ya Tanzania, lakini Mfaransa huyo hivi sasa anatumia vijana wengi aliowapandisha kutoka kikosi cha pili.
Ni vijana hao hao, waliokaribia kuifunga Azam FC Jumapili baada ya kuongoza 2-0, 2-1 na baadaye 2-2 katika mchezo wa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hadi sasa, Liewig amekwishaiongoza Simba SC katika mechi 22, akiiwezesha kushinda saba, sare nane na kufungwa saba tangu aanze kazi Januari mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick.