![]() |
Kali wa pili kutoka kulia, akiwa na Stewart Hall kocha Mkuu, kushoto kwake ni makocha wengine wasaidizi, Ibrahim Shikanda na Iddi Abubakar |
Na Prince Akbar
KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Kali Ongala amesema kwamba bado hawajakata tamaa ya ubingwa licha ya kuzidiwa pointi tano na Yanga zikiwa zimebaki mechi tatu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kumalizika.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Ongala alisema kwamba ni kweli sare ya 2-2 na Simba SC Jumapili imewavurugia, lakini hawajakata tamaa kwa sababu Ligi haijaisha.
“Sisi tuna mechi tatu, Yanga wana mechi nne, lolote linaweza kutokea katika mechi hizi zilizobaki, kwa sababu hata sisi hatukutegemea kutoa sare na Simba, tulitarajia sana kushinda, ila kama unavyojua mambo ya soka tena,”alisema.
Kali alisema hawezi kusita kusema Yanga wana nafasi kubwa, kwa sababu wanaongoza Ligi Kuu, lakini anaamini hata Azam FC bado ina nafasi.
“Hizi mechi za mwishoni huwa ni ngumu sana, timu zinapigana kuepuka kushuka Daraja, kwa hivyo hazikubali kufungwa kwa urahisi, ndiyo maana ninakuambia sisi bado hatujakata tamaa ya ubingwa,”alisema.
Baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Simba SC, Azam sasa inaiombea duwa mbaya Yanga katika mechi zake zijazo ili mchuano wa ubingwa uendelee.
Lakini kama Yanga watashinda mechi mbili, maana yake mbio za ubingwa zitakuwa zimefikia tamati na Azam FC watatakiwa kujiimarisha kwa ajili ya nafasi ya pili.
Ikumbukwe, Yanga SC ina pointi 52 kileleni, ikifuatiwa na Azam yenye 47, Kagera Sugar 37 na Simba SC 36, ambao tayari wamekwishautema ubingwa wa Ligi Kuu.
Kuelekea mwishoni mwa Ligi Kuu, nafasi ya pili ndiyo inaonekana kuwa na mvuto zaidi, ikiwania na timu tatu, Azam yenyewe, Kagera na Simba SC.