![]() |
Marais; Ndolanga kulia, akisalimiana na rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga |
Na Mahmoud Zubeiry
RAIS wa heshima wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alhaj Muhiddin Ahmad Ndolanga jana alitoa maoni yake kwa Mkuu wa Idara ya Uanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Primo Corvaro juu ya mgogoro wa uchaguzi wa TFF katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zinasema kwamba pamoja na Ndolanga, wagombea pia walioathiriwa na uamuzi wa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake, Iddi Mtiginjola wakiwemo Jamal Malinzi na Michael Wambura, nao walihojiwa pia.
Primo aliwasili juzi nchini kwa pamoja na Mkuu wa Kanda hii, Ashford Mamelodi kwa ajili ya kutatua mgogoro wa uchaguzi wa TFF.
Wagombea wangine waliokuwamo katika orodha hiyo mbali ya Malinzi anayegombea Urais na Michael Wambura, Makamu wa Rais ni Farid Salim Mbaraka Nahdi, Elliud Peter Mvella, Mbasha Matutu (Ujumbe wa Kamati ya Utendaji) na Hamad Yahya (Uenyekiti wa Bodi ya Ligi).
Leo Primo na Mamelodi wanatarajiwa kukutana na Kamati ya Rufaa baaada ya kuwasikiliza wagombea walioenguliwa na baada ya hapo watapeleka ripoti Zurich, Usiwsi yalipo makao makuu ya FIFA kwa ajili ya tathmini kuchanganua kabla ya kutoa majibu.
TFF inakabiliwa na mgogoro wa uchaguzi, baada Kamati ya Rufaa kuwaengua wagombea wagombea kadhaa akiwemo Malinzi katika mazingira ya mizengwe na kumuacha Makamu wa sasa wa kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee katika nafasi ya Urais.
Malinzi alikata rufaa FIFA na uchaguzi ukasimamishwa hadi suala hilo lichunguzwe. Katikati ya sakata hilo, Serikali nayo ikasimamisha Katiba mpya ya TFF iliyopitishwa mwaka jana kwa njia ya waraka, kwa sababu ni kinyume cha katiba ya mwaka 2006 na kuagiza iitishe Mkutano Mkuu kupitisha Katiba mpya kwa mwongozo wa Katiba iliyopo mezani.
Hata hivyo, baadaye pande hizo mbili, Serikali na TFF ziliketi meza moja na kufikia makubaliano ya kuwaacha kwanza FIFA waje kutatua mgogoro wa uchaguzi ndipo masuala mengine yataendelea.