• HABARI MPYA

    Wednesday, April 17, 2013

    VAN PERSIE ANGECHEZA YANGA MECHI 10 BILA KUFUNGA, BAHANUZI...



    “Alikaribia kuniua kwa ushangiliaji wake, alisahau kama mimi ni mzee wa miaka 71!,” hayo ni maneno aliyoyasema Sir Alex Ferguson, kocha wa Manchester United ya England, baada ya Robin Van Persie kufunga bao la pili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Stoke.
    Mshambuliaji huyo wa Kiholanzi alicheza mechi za mashindano ya nyumbani ndani ya miezi miwili bila kufunga bao na mwishoni mwa wiki baada ya kufunga kwa mpira kutengewa, alikaribia kuwa kichaa kwa kushangilia.
    Kaifunga Stoke, tena kwa penalti, RVP ni wa kushangilia kwa wazimu namna ile? Ndiyo, amekaa uwanjani muda mrefu bila kufunga.

    Ukame wa mabao ni kitu ambacho huwatokea wachezaji wengi tu duniani wakubwa na si Fernando Torres peke yake. Hata Wayne Rooney kuna wakati alikuwa halioni lango.
    Van Persie alifunga mfululizo mabao 19 katika Ligi Kuu England na baada ya hapo, akaingia katika wakati mgumu hadi Jumapili alipofunga tena baada ya miezi miwili. Tena alifunga kwa penalti. Sir Ferguson anaamini juu ya uwezo wa mchezaji huyo na alikuwa akiamini anakosa bahati tu uwanjani, ndiyo maana aliendelea kumpa nafasi.
    Na kweli, japokuwa hafungi, lakini shughuli ya Mholanzi huyo uwanjani inaonekana- anawapa wakati mgumu mabeki na pia kuwepo kwake tu uwanjani, kunaisaidia timu kushinda japo kwa mabao ya wachezaji wengine.
    Hivi sasa mashabiki wa Yanga wanamkandia Said Rashid Bahanuzi, eti ameisha- kisa tu alifunga kwa mara ya mwisho katika mchezo wa Simba na Yanga mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, tena kwa penalti.
    Mimi napita, nawasikiliza, naachana nao- kwa sababu mashabiki wengi uelewa wao ni mdogo na mbaya zaidi ni wabishi. Said Bahanuzi ‘Spider Man’, hajaisha na hataisha leo wala kesho, labda itokee bahati mbaya ya kupata maumivu makubwa ya kumuweka nje ya Uwanja muda mrefu.
    Kwa nini nasema hivyo? Staili yake ya uchezaji ni nzuri na pia hata rekodi yake ya mazoezi ni nzuri, kuanzia ya timu hadi binafsi. Anapoachana na Mholanzi Ernie Brandts, Bahanuzi amekuwa na programu yake ya mazoezi ya gym tena kwa kujilipia mwenyewe fedha.
    Na siku zote, uliza mabeki wa Yanga, Bahanuzi ni mtu anayewapa  mtihani mzuri sana wa kukabiliana na mshambuliaji hatari. Jamaa ni hatari.
    Kweli, bado hajarudi katika kiwango chake kile kilichomfanya asajiliwe Yanga kutoka Mtibwa Sugar na pia alichoanza nacho katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana akiibuka mfungaji bora.
    Na hiyo ni kwa sababu maumivu aliyoyapata yalikuwa ni makubwa. Alikaa nje ya Uwanja kwa takriban mwezi mzima bila kugusa mpira wala kukimbia hata hatua moja. 
    Huyu anahitaji muda kabla ya kurudi katika hali yake ya kawaida na pengine ni hadi msimu ujao, ndipo makali ya Spider Man yatarudi. Lakini unaweza kuona anavyolihemea lango katika mechi zote anazopangwa akitokea benchi siku za karibuni na bado amekuwa akitoa pasi kwa wenzake kufunga.
    Ni mtu mwenye kiu ambaye hata ukikutana naye nje ya Uwanja sura yake inakueleza hivyo na unaweza kuwa na matumaini naye kama atarudisha tu makali. Atarudi hadi timu ya taifa wakati ukifika.
    Tatizo moja tu katika soka ya Tanzania, viongozi wetu wengi nao ni kama mashabiki, hawajui vyema soka na wamekuwa wakivuruga wachezaji na makocha. Huu ni mtihani mwingine ambao unakwamisha maendeleo ya soka yetu kwa kiasi kikubwa.     
    Ni bahati nzuri kwake sasa hivi Yanga hata washambuliaji wengine hawafanyi vizuri, ndiyo maana anapata fursa ya japo kutokea benchi kuingia kucheza.
    Lakini kama Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza wangekuwa wanafunga vizuri, Bahanuzi angekuwa katika wakati mgumu zaidi ya aliokuwa nao sasa Yanga SC.
    Hii ni kwa sababu klabu zetu hazina mipango wala utaratibu wa kutambua, kuheshimu na kuthamini uwezo wa mchezaji na ndiyo maana wanawachukulia kulingana na wakati unaowakabili tu. Hafungi basi. Hawana kumbukumbu nao hata chembe.
    Hawakumbuki kwa nini waliwasajili. Hawakumbuki walifanya nini jana.
    Na pamoja na misukosuko yote aliyopitia, hadi sasa Bahanuzi ndiye mshambuliaji aliyeifungia Yanga mabao mengi msimu huu, 13 katika mechi 23, akifuatiwa na Didier Kavumbangu mabao 10 katika mechi 27. Unasemaje? 
    Umefika wakati lazima viongozi wa klabu zetu wabadilike na kuanza kutambua uwezo wa wachezaji wao hata wanapokuwa katika wakati mgumu.
    Bahanuzi alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Kagame, tena akifunga mabao bora sana ambayo hadi watangazaji na wachambuzi wa Super Sport TV ya Afrika Kusini walikuwa wanayasifia sana. Aliendelea kufunga karibu katika kila mechi hata baada ya Kagame kabla ya kuumia katika mechi na Kagera Sugar tena kipindi cha kwanza tu.
    Alichanika nyama za paja- jamani haya ni kati ya maumivu mabaya sana kwa wachezaji. Ipo haja ya kumpa muda Spider Man na iko siku atawapa raha tena wana Yanga na sijui atashangiliaje hilo bao la kwanza atakalofunga mwaka huu kama Van Persie aliyekosa mabao miezi miwili tu alitaka kumuua babu Ferguson. Alamsiki.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: VAN PERSIE ANGECHEZA YANGA MECHI 10 BILA KUFUNGA, BAHANUZI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top