• HABARI MPYA

    Sunday, July 14, 2013

    BANDARI ZANZIBAR YAWAKANA AZAM MANUNUZI YA TIMU ZANZIBAR

    Na Salum Vuai, Zanzibar, IMEWEKWA JULAI 14, 2013 SAA 2:50 ASUBUHI
    HATIMAYE Shirika la Bandari Zanzibar, limekata mzizi wa fitina kwa kuthibitisha kuuza nafasi ya timu yake Bandari SC kwenye Ligi Kuu msimu ujao kwa klabu kongwe ya Malindi SC.
    Hatua hiyo inamaanisha ndoto za matajiri wa Azam FC ya Dar es Salaam kununua daraja la timu hiyo ambayo shirika linaloimiliki limedai kutomudu gharama za uendeshaji, sasa zimefutika.
    Wiki kadhaa zilizopita, uongozi wa Azam FC kupitia Katibu wake Mkuu Nassor Idrissa Mohammed, na Katibu wa Bandari SC Makame Silima Makame, walikaririwa wakisema tayari wamefanya mazungumzo na kukubaliana kwamba Bandari iuze nafasi yake Azam, makamu bingwa mara mbili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
    Kinachofuata? Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa, mmiliki wa kampuni ya S.S.B. iliyoinunua Bandari, ambayo imeuzwa pia kwa Malindi SC akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.  

    Mbali na makubaliano ya makatibu hao, baadae ilibainika kuwa, uongozi wa shirika ulikwishapokea shilingi milioni tano kutoka kwa klabu ya Malindi, kwa ajili ya kuwauzia nafasi yao kwenye ligi kuu ya Zanzibar.
    Malindi ambayo ni miongoni mwa timu kongwe na iliyowahi kufika nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika (sasa Kombe la Shirikisho), iliteremka daraja la ligi kuu hadi la kwanza, baada ya kushindwa kuhimili vishindo vya ligi hiyo msimu uliopita.
    BIN ZUBEIRY ilifanikiwa kuinasa nakala ya barua ya Bandari SC ya tarehe 11 Julai, mwaka huu yenye namba za kumbukumbu ZPC/BSC/VOL.1/42/2013 ambayo imesainiwa na Katibu wa klabu hiyo Makame Silima Makame kwenda kwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ikitaarifu kuridhia maamuzi ya uongozi wa shirika.
    "Kwa vile uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar ulikwisha kuamua kuuza daraja la Premiar League kutoka kwa timu ya Bandari Sports Club na kuiuzia klabu ya Malindi iliyoko daraja la kwanza hapa Zanzibar, uongozi wa Bandari SC umeridhia maamuzi hayo yaliyotolewa na uongozi wa Shirika", ilisema sehemu ya barua hiyo.
    Hata hivyo, pamoja na Bandari kuuza nafasi yake Malindi kwa shilingi milioni 5 tu, inakabiliwa na mtihani kwani kwa mujibu wa kanuni za ZFA zinazohusu biashara ya kuuziana daraja, shirika hilo linapaswa kukilipa chama hicho shilingi milioni saba.
    BIN ZUBEIRY iliwasiliana na Mkurugenzi wa Shirika la Bandari, Abdallah Juma kutaka kufahamu imelipokeaje agizo la kutakiwa kuilipa ZFA kiasi hicho cha fedha wakati wenyewe wameuza daraja kwa shilingi milioni tano tu, lakini katika hali ya kushangaza, alijibu ifuatavyo na kukata simu:
    "Mpigie Katibu wa timu au andika tu kama unavyoandika kila siku, si naziona makala zako". 
    Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Haji Salum, ameliambia gazeti hili kuwa, iwapo Bandari itashindwa kulipa fedha hizo, chama chake hakitatambua mauziano hayo, na pia itazuiwa kucheza katika daraja lolote lingine.
    Aidha amefahamisha kuwa, hali hiyo itaweza pia kuiathiri Malindi hadi Bandari itakaposawazisha deni hilo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BANDARI ZANZIBAR YAWAKANA AZAM MANUNUZI YA TIMU ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top