• HABARI MPYA

    Wednesday, July 17, 2013

    KWA MTAJI HUU, HUYO MSHAMBULIAJI WA KUTUFUNGIA MABAO STARS ATATOKA WAPI?

    IMEWEKWA JULAI 17, 2013 SAA 2:00 ASUBUHI
    TANZANIA ni moja kati ya nchi zilizoweka historia ya kuwa timu za kwanza kushiriki michuano mipya ya CAF, CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
    Wakati huo ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo, Tanzania ilifuzu kwa kishindo bila kupoteza hata mchezo mmoja katika mechi za mchujo.
    Ilianza kwa kuifunga Kenya nyumbani kwake Nairobi, mabao 2-1 na katika mchezo wa marudiano ikawafunga tena Harambee Stars 1-0.

    Ikahamia kwa Uganda, mchezo wa kwanza Taifa Stars ikashinda 2-0 nyumbani na ugenini kwenye mchezo wa marudiano ikatoa sare ya 1-1 nakumbuka bao la Stars lilifungwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ Uwanja wa Mandela, Namboole, lilikuwa bonge la bao la shuti la mbali.
    Taifa Stars ikamalizia kazi vizuri katika mechi za mwisho za kufuzu, baada ya kuitoa Sudan kwa jumla ya mabao 5-2, ikianza kushinda nyumbani 3-1 na kwenda kushinda ugenini pia 2-1, bao la pili akifunga Nurdin Bakari kwa kichwa cha rasta zake.
    Wakati huo, safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars ilikuwa inaongozwa na washambuliaji viongozi wa klabu zao, Mussa Hassan Mgosi wa Simba SC na Jerry Tegete wa Yanga na ndio waliokuwa wanapokezana kufunga katika mechi za kufuzu.
    Bado walikuwepo wachezaji wengine hodari waliokuwa wanaongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji kama Mrisho Ngassa na Haruna Moshi ‘Boban’ ambao wote walikuwa wako sawa sawa wakati huo.
    Katika fainali zenyewe za CHAN tulikaribia kuingia Nusu Fainali kama si kukosa ujanja kwa kipa wetu Shaaban Dihile wa kucheza na muda zikiwa zimebaki dakika tano tunaongoza bao 1-0 dhidi ya Zambia, hadi wapinzani wakakomboa bao na kuwa 1-1. 
    Kwenye michuano hiyo tuliwafunga wenyeji 1-0, Ivory Coast bao pekee la Ngassa baada ya kufungwa 1-0 katika mchezo wa kwanza na Senegal.
    Mwaka huu katika mechi za kufuzu za CHAN, Raundi ya kwanza wapinzani Kenya walijitoa na raundi ya Pili Stars ikaanza kwa kufungwa 1-0 nyumbani na Uganda na sasa inajiandaa kwenda kupanda mlima Kampala katika mchezo wa marudiano, ikitakiwa kushinda 2-0 ili ifuzu.
    Baada ya kufungwa 1-0 nyumbani, mengi yamezungumzwa tangu Jumamosi juu ya kipigo hicho, zaidi wachezaji wakisukumiwa lawama kwamba hawakujituma na wengine wakimshutumu kocha Mdenmark, Kim Poulsen kwamba hana mipango mbadala.
    Ukweli ni kwamba kipigo cha nyumbani kimewauma wananchi, kwani walikuwa wana matumaini makubwa na timu yao baada ya kuishuhudia ikicheza vizuri katika mechi ngumu za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia licha ya kutopata matokeo mazuri sana.
    Lakini ukiurejea mchezo ule kwa umakini, unagundua tatizo lilikuwapo katika safu ya ushambuliaji- mategemeo yalikuwa kwa Mrisho Ngassa na John Bocco ambao kwa bahati mbaya walidhibitiwa kwa urahisi. Amri Kiemba ambaye amekuwa akitumika kama mchezaji huru uwanjani mwenye jukumu la kucheza zaidi kuelekea kwenye eneo la wapinzani, siku hiyo hakuwa vizuri sana.
    Saumu ya mfungo wa mwezi mtukufu Ramadhani, nayo ikatajwa kama sababu ya kuidhoofisha Stars siku hiyo. Wengine nikiwamo mimi, tunaamini Stars walifungwa kwa sababu ya kujiamini kupita kiasi na kuidharau Uganda, baada ya kuona imetunishiana kifua na timu kama Morocco na Ivory Coast zenye wachezaji bora.
    Lakini bado katika timu yetu kuna matatizo ya msingi- safu ya ushambuliaji ya Stars kwa sasa inawategemea wachezaji wawili wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao kwa kuwa CHAN inahusu wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, wao hawaruhusiwi kucheza.
    Sasa ni akina nani washambuliaji wetu wengine kwa sasa? Kwa kiasi kikubwa Stars inaundwa na wachezaji wa Azam, Simba na Yanga na huko kuna washambuliaji gani wazawa waliofanya vizuri msimu uliopita? Hakuna. 
    Jerry Tegete shughuli inaelekea ukingoni, John Bocco pale Azam tumeshuhudia akimaliza msimu vibaya tofauti na msimu uliotangulia alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu. Nani sasa mwingine?
    Pale Yanga safu ya ushambuliaji iliongozwa na wageni Hamisi Kiiza na Didier Kavumbangu, wakati kinara wa mabao wa Azam alikuwa Kipre Tchetche na SImba SC mshambuliaji tegemeo alikuwa Felix Sunzu.
    Unaweza ukaona tofauti ya sasa na wakati tunafuzu CHAN ya kwanza Ivory Coast, kwamba tulikuwa tuna wachezaji ambao ni viongozi katika timu zao.
    Jose Mourinho, kocha mpya wa Chelsea anapambana kuinasa saini ya Wayne Rooney wa Manchester United na turufu anayotaka kuitumia sasa ni umuhimu wa mshambuliaji huyo katika kikosi cha England. Mreno huyo amesema; “Ikiwa Wayne atakuwa chaguo la pili Man United (baada ya Mholanzi Robin van Persie), basi timu ya taifa ya England itaathirika,”.
    Mwisho wa siku Waingereza wanaipenda timu yao na wataona umuhimu wa Rooney kuwa mchezaji chaguo la kwanza na hapana shaka Mourinho anaweza kushinda vita ya kumnasa mchezaji huyo licha ya sera ngumu ya United kutouza wachezaji wake kwa wapinzani wao.
    Tunapojadili matatizo ya timu yetu ya taifa, tunahitaji kuweka kando jazba na kuwa makini mno na kutazama maeneo tofauti ili kupata suluhisho la kweli na si kusukumwa na hasira za kufungwa tu. Stars bado ina nafasi ya kufuzu na inaweza kuitoa Uganda, iwapo Kim na vijana wake watajipanga vizuri kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
    Lakini hata kama itafuzu, itakuwa imepita katika wakati mgumu na itahitaji kujipanga mno kabla ya Fainali za CHAN Afrika Kusini mwakani.
    Ubora wa timu ya taifa unatokana na klabu imara za nchi husika- wazi Tanzania kwa sasa tunazitegemea mno Azam, Simba na Yanga kupata wachezaji bora wa taifa. 
    Kocha Kim anatafuta wepesi kwa kuchukua wachezaji ambao anaamini wametafutwa kwanza kwa ubora wao na timu hizo tatu bora nchini na pili wakawekwa chini ya makocha wa kiwango cha juu na ndiyo maana Stars ni Azam, Simba na Yanga. Hilo halikwepeki.
    Mwaka 2000 nilifanya mahojiano Yussuf Macho akasema timu ya taifa inaundwa na wachezaji wa Dar es Salaam na Morogoro tu- lakini wakati huo baada ya Simba na Yanga timu nyingine ya ushindani Tanzania ilikuwa Mtibwa Sugar.
    Hali hii itaendelea, wachezaji wa timu ya taifa watatafutwa katika timu bora kwenye ligi yetu na timu nyingine zitaendelea kutoa mmoja mmoja, tena kwa nadra na hapa ndipo unapoweza kuuona umuhimu wa kuwa na ligi ya ushindani zaidi.
    Wakati tunaelekea msimu mpya, Simba imesajili mshambujliaji wa Burundi Amis Tambwe baada ya kumtema Felix Sunzu na inataka kuongeza mshambuliaji mmoja wa kigeni na bila shaka Mganda Moses Oloya atachukua nafasi.
    Azam ilimtegemea Kipre Tchetche msimu uliopita na itaendelea kumtegemea hata msimu ujao, lakini Brian Umony naye baada ya kuanza pole pole nusu ya mwisho wa msimu uliopita, sasa anaanza kuzoea hali ya soka ya Tanzania na ni matumaini msimu ujao atachomoa makucha yake.
    Yanga SC iliwategemea Kavumbangu na Kiiza msimu uliopita na tayari imesajili mchezaji mzuri kutoka Heartland FC ya Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi na wakati huo huo iko mbioni kuleta mshambuliaji Mbrazil, ambaye kama atakuja basi mmoja kati ya Kiiza au Kavumbangu atampisha.
    Unaweza kupata picha ya safu za ushambuliaji za timu hizo tatu bora nchini msimu ujao- zitaundwa na wachezaji wa kigeni, maana yake Samatta na Ulimwengu wataendelea kuwa mboni za jicho katika timu yetu ya taifa.
    Kim ataendelea kuwalazimisha wachezaji wenye maumbo madogo na wa pembeni kuwa washambuliaji wa kati- au kama anavyowatumia sasa viungo Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba na dhahiri hatutakuwa na safu imara ya ushambuliaji.
    Kabla ya kwenda DRC, Samatta alikuwa African Lyon baadaye Simba SC  na Ulimwengu alikuwa Moro United maana yake wanaweza kupatikana wachezaji wengine kama hawa, iwapo kwanza watatafutwa na pili watapewa nafasi ya kucheza ili kujifunza zaidi na kukusanya uzoefu.
    Azam, Simba na Yanga zinaajiri makocha wa kigeni zinawalipa fedha nyingi, basi wawajibike kukuza viwango vya wachezaji wetu na si kuwa wepesi kuagiza viongozi watafute wachezaji nje. 
    Na wala wasitudanganye eti wachezaji wetu hawafundishiki, hapana kwa sababu Ulimwengu na Samatta ni Watanzania pia na kabla yao tulikuwa nao akina Abubakar Mkangwa, Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella, Peter Tino, Sunday Manara, Abdallah Kibadeni na wengine. 
    Azam, Simba na Yanga lazima zitambue zenyewe ndizo tegemeo katika soka ya Tanzania na zina wajibu mkubwa wa kusaidia ustawi wa soka ya nchi hii- na kama kila klabu itaendelea kukwepa jukumu la kumuandaa mshambuliaji Mtanzania awe tegemeo la timu yake, huyo mshambuliaji wa timu ya taifa atatoka wapi? Ramadhan Kareem.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KWA MTAJI HUU, HUYO MSHAMBULIAJI WA KUTUFUNGIA MABAO STARS ATATOKA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top